Jumatano, 30 Desemba 2015

HILA NO.11

SEHEMU YA KUMI NA MOJA JOPO la madaktari wenye asili ya kihindi liliingia katika chumba cha ambacho Yakubu Gama alikuwa amelazwa. Walikuwa wameng’ara katika sare zao rangi ya bluu. Waliweza kuongea maneno machache tu ya kiingereza, asili yao ilikuwa uhindini. Baada ya kuingia katika kile chumba milango ilifungwa huku wakitoa agizo kuwa haruhusiwi mtu yeyote kuingia katika chumba kile. Askari wakabaki kufanya ulinzi! Baada ya milango kufungwa, daktari mmoja alitwaa simu yake na kupiga namba kadhaa, sekunde chache mbele simu ikapokelewa. “Tupo ndani ya chumba tayari!” alizungumza kwa kiingereza kibovu. “Kumbuka kufanya upesi na kwa usahihi kama nilivyowaeleza….” “Hakuna mashaka!” Akakata simu na kuwafanyia wale wenzake kama ishara! Wakakizunguka kitanda kama wakizungukavyo kitanda cha mgonjwa mahututi. Mgonjwa alikuwa ana majeraha makubwa ya kuunguzwa na moto na pia alikuwa amevunjika mkono na mguu. Naam! Gama aliyejeruhiwa katika mlipuko wa bomu. Wakamtundika mipira mingine katika mishipa yake na kisha kuruhusu dawa zimwingie kwa kasi. Wakati huohuo daktari mwingine akiuamsha moyo wa mgonjwa kwa kutumia mashine. Hatimaye akakohoa, wakaendelea na jitihada zao hadi fahamu zikamrejea.  Wale madaktari wakafanya kama walivyoagizwa wakaanza kumuhoji mgonjwa kitandani. Maswali yao yote yalikuwa juu ya tukio lililopita na kumfanya awe pale kitandani hoi. Walimuuliza alichokuwa anakumbuka lakini hapakuwa na majibu, yule bwana hakuonekana kukumbuka jambo lolote lile. Walimuuliza jina lake akajitambulisha kuwa yeye ni Hasani Hasani. Madaktari waliyarekodi majibu yote hayo, kama walivyoagizwa kuwa kwa majibu yoyote atakayoyatoa yule bwana ambaye walimtambua kwa jina la Gama Yakubu. Baada ya kurekodi kilichokuwa kinafuata ni kuuondoa uhai wa mtu yule aliyesadikika kuwa na lolote ajualo kuhusiana na mkakati mahususi wa siri!! Naam! Wakamwondoa uhai wake kwa kumchoma sindano yenye sumu kali. Kisha wakatoka ndani ya kile chumba huku wakitikisa vichwa vyao. Wakasikitika na kutoa majibu kuwa haikuwezekana kuokoa uhai wa Gama kwani damu ilivilia katika ubongo wake. Pia wakasisitiza zaidi kuwa mwili wa marehemu umeharibika vibaya hivyo ni vyema uzikwe mapema. Taarifa za Yakubu Gama kupoteza uhai zikamfikia IGP na mrakibu msaidizi Robert. Kila mmoja akaipokea katika namna aijuayo mwenyewe. IGP akampigia simu mzee Matata na kumshukuru kwa jitihada kubwa alizoonyesha, akamsifu kwa uzalendo wake katika nchi isiyokuwa yake. Lakini hakusahau kumkandia bwana Robert kuwa kwa kuchelewa kwake kuwaruhusu madaktari basi amechangia kifo cha Yakubu Gama. Mwisho akamweleza Mzee Matata kuwa raisi atasimamia safari nzima ya madaktari wale kurejea nchini India. Mzee Matata akashukuru na kisha simu ikakatwa. Gama akahesabika kuwa kijana wa pili muhimu kabisa katika usalama wa taifa kupoteza uhai katika kipindi cha mwezi mmoja.. Mzee Robert alipewa taarifa ile ya kifo na mkewe kama ushuhuda juu ya alichomweleza usiku juu ya madaktari hao feki. Bwana Robert alimkumbatia mkewe na kumshukuru kwa ushauri wake lakini akabaki kusikitika kuwa yeye hakuwa juu ya IGP hivyo asingeweza kuwazuia madaktari wale kuingia katika kile chumba alichokuwa amelazwa Gama. Mke akatoa pole na kumtia moyo mume wake.  Mzee Robert akashukuru! Na baada ya hapo akamuaga mkewe na kuelekea hospitali ya Lugalo. Huko akaenda kukutana na Daktari Macho. Bwana ambaye walisoma naye shule moja ya msingi hadi chuo kikuu, na hapo wakatengana mmoja akisomea udaktari na mwingine akisomea uhasibu!  Taaluma zikawatenganisha lakini baadaye zikawakutanisha tena, Dokta Macho akiwa anafanya kazi katika hospitali ya jeshi na Robert akiwa na cheo cha Mrakibu mkuu wa polisi. Usiku ule thamani ya urafiki wao iliendelea kuonekana huku wakiwa wanaaminiana kwa silimia kubwa. Dokta Macho aliyasikiliza mashaka ya Robert na kuamua kutii alichosisitizwa, akamuhamisha chumba Yakubu Gama kisha katika kile kitanda akawekwa bwana aliyeshukiwa kuwa ni mwizi, wananchi wakachukua sheria mikononi na kumchoma moto. Lakini kabla mambo hayajawa mabaya sana akaponea chupuchupu na kuwahishwa hospitali. Majeraha katika mwili wake na yale ya Yakubu Gama baada ya mlipuko yalifanana sana maana yote yalikuwa majeraha ya moto. Wale madaktari kutoka India wakakutana na mchezo ndani ya mchezo waliopanga kuucheza. Wakachezewa shere na mwisho wa siku wakaumalizia uhai wa yule kibaka. Wakajisifu kuwa wamemuua Yakubu Gama. *** Kwa kitendo kile cha kuwarubuni madaktari, bwana Robert alitambua vyema kuwa amejiingiza katika vita na IGP pamoja na mkuu wan chi maana hawa walikuwa hawaambiliki kwa lolote juu ya mtu wa kuitwa mzee Matata. Hofu kubwa aliyokuwanayo Robert ni juu ya usalama wake na daktari aliyeshiriki katika tukio lile.  Na hapo akatambua kuwa hatakiwi kulala kitandani na kupeleka mambo taratibu taratibu. Badala yake alitakiwa kufanya mambo kwa kasi ya ajabu ili hata siku wakimlaza usingizi wa milele basi neno lake liendelee kuishi huku likiwaumbua wote waliokuwa wakijificha huku kiuhalisia walikuwa wauaji. Kwa kufikiria ni namna gani anaweza kuchakarika kwa kasi bila uoga. Robert akaamua kuyahamishia mambo yaliyokuwa katika kichwa chake akayaweka katika maandishi. Neno kwa neno kuanzia mashaka yake juu ya mzee Matata, pia lawama zake juu ya IGP na kisha akagusa mamlaka kuu ndani ya nchi akapagusa Ikulu. Akapataja kuwa panahusika kumficha mzee Matata. Baada ya kuandika kurasa nyingi sana akautuma ujumbe ule mahali ambapo aliamini kuwa ni sahihi kabisa na wala hatakuwa amepotea kufanya vile. Hakujitambulisha yeye ni nani wala cheo chake katika uongozi wa jeshi la polisi. Harakati zikazidi kupamba moto!! ***** MOROGORO MJINI AKILI za kuzaliwa za Atuganile ama maarufu kama mama lao zilimfaa mara nyingi sana. Hata katika maisha yake ambapo alikuwa ameishia darasa la saba hakubabaika na kuyaogopa maisha. Alipambana kwa mafanikio jijini Mbeya na kisha kuingia jijini Dar es salaam huku akiwa hana mwenyeji hata mmoja. Lakini licha ya hayo bado aliweza kupambana bila kuwa ombaomba. Kilichokuwa kinambeba katika maisha yake ni siri zake kwa jambo ambalo anatarajia kulifanya. Kila wakati alikuwa akihofia kuwaambia watu mipango yake kwa kuhofia kukatishwa tama. Hivyo aliiongoza serikali ya maisha yake kwa kutumia kichwa chake mwenyewe. Tabia hiyo iliendelea hata siku ile ambapo alipandishwa gari na Sam kwa ajili ya kwenda Mbeya. Naam! Alihitaji Sam atambue kuwa yupo Mbeya, ili ikitokea siku moja Sam amekamatwa na kubananishwa ipasavyo ajikute akiisaidia ;polisi upelelezi wa kumtafuta mama lao Mbeya. Msako ambao ungewachukua miaka zaidi ya kumi bila mafanikio yoyote. Wangedumu wakimsaka mama lao jijini Mbeya wakati mipango yake ilikuwa tofauti kabisa. Mama lao kwa utashi wake mkubwa gari lilipofika Morogoro akashuka, bila kutoa taarifa. Gari likaondoka huku siti yake ikibaki wazi, kondakta akajisikia vibaya sana kuwa amemuacha abiria wa kwenda Mbeya stendi ya Msamvu Morogoro. Wakati kondakta akifadhaika na kumuuliza jirani yake juu ya yule abiria wa Mbeya aliyeachwa njiani. Mama lao alikuwa ameshikilia gazeti ambalo lilikuwa likimtangaza kuwa anasakwa kwa mauaji. Alitabasamu kisha akacheka kwa nguvu! Hakuwa na wasiwasi hata kidogo. Hakika alikuwa na jina kubwa lakini bahati nzuri iliyoje hakuwa na kumbukumbu ya kuwahi kupiga picha jijini Dar es salaam. Mazingira aliyofanyia kazi hayakuwa mepesi kupiga picha, alikuwa ni mtu wa kutingwa masaa yote. Nani angekuja kumpiga picha!! Ungekuwa mgahawa wa watu wa kifahari walau wangepata huo muda wa kuchukua kumbukumbu. Lakini waliohudhuria mgahawa ule wengi wao walikuwa mafukara tu ambao msongo wa mawazo ni kipande kimoja katika maisha yao ya kila siku. “Wali nyama, niwekee wa kushiba!” hizi nd’o zilikuwa lugha zao. Baada ya hapo ni malipo na kukutana tena ni kesho yake. Magazeti yakabaki kuandika jina la mama lao tu! Bila picha wala jina halisi hawakulijua. Tanzania nzima kuna akina mama lao wangapi?? Bahati iliyoje kwa mama lao Atuganile kuonyesha makucha yake pasipo kujulikana. ***** KATIKA Mji ambao aliishi mama lao kwa wakati ule, ulikuwa ni mji wa maficho pia kwa kijana Yakubu Gama ambaye alikuwa amehifadhiwa kwa ajili ya matibabu.  Fahamu zilikuwa zimerejea tayari na damu yake ilikuwa inachemka haswa kwa ajili ya mapambano. Alikuwa na kiu ya kujua kunani hadi mambo haya yote yanatokea. Na kubwa zaidi alitamani kumjua muuaji wa Steven Marashi ambaye alikuwa pacha wake katika kazi kabla hajahamishiwa kazi maalumu ya upelelezi, kazi ambayo ilimfanya ajikute katika sanaa ya maigizo na hatimaye kuanza kucheza katika filamu. Hakuna hata muigizaji mmoja aliyetambua kuwa Steven Marashi alikuwa kijana wa usalama wa taifa. Kwa tukio lile la kulipukiwa na bomu ambalo lilikuwa katika mwili wa kijana aliyeagizwa na BVB kulizidi kumtamanisha kutambua kuwa ni kitu gani ambacho kinafichwa. Hisia zake kubwa zikajijenga juu ya upelelezi ambao Steven Marashi alikuwa akiufanya kimyakimya dhidi ya kigogo wa serikali. Upelelezi alioubatiza jina oparesheni tokomeza. Alichotaka kukitokomeza alifahamu yeye mwenyewe.. jambo la muhimu alimsihi Gama kuwa mtulivu ayangoje majibu. Hivyo kama Steve ameuwawa bila shaka ule upepelezi wake ambao alikuwa hajaukabidhi ofisi kuu ulikuwa katika mikono ya mtu mwingine ambaye amezing’amua siri nzito za usalama wa taifa.  Kitendo cha kutaka kuuwawa akiwa hospitali kilimsababisha apigie mstari mashaka yake na kuamini kuwa anatakiwa apambane upesi ili kuupata ukweli. Na aliamini hilo linawezekana sana kwa sababu tayari alitambulika kuwa amekufa. Na vile mwili wake haukuagwa kwa sababu kuwa ulikuwa umeharibika sana.  Akabaki kujulikana yu hai kwa watu wasiozidi wanne! Hakuna hata mmoja kutoka katika familia yake aliyetambua kama yu hai mjini Morogoro. Gama alijaribu kutembea kwa kujivutavuta hadi akakifikia kioo. Akajitazama! Lahaula! Hakuwa yeye, sura yake iliunda mfano wa mapunye na ngozi yake ilikuwa imechubuliwa vibaya sana na lile bomu. Akajaribu tena na tena kujitazama hakuwa yeye! Hasira zikamjaa kifuani akaubamiza ukuta kwa ngumi nzito! Na hapo mwenyeji wake ambaye ni daktari akaingia na kumsihi ajipumzishe kwani hakutakiwa kujihangaisha kwa lolote hadi pale atakapopona! Gama alirejea kitandani akajilaza lakini ni kwa kupumzisha mwili tu na sio akili. Akili ilikuwa inapanga mikakati kabambe! Akamfikiria sana hayati Steven Marashi, akakifikiria kifo chake kilivyokuwa cha upesi, na tetesi zake ambazo hazikuwa zinaeleweka. Mara ameuliwa kishirikia na mpenzi wake, mara amejiua. Gama akaufikiria ukakamavu wa Steve, akafikiria ni jinsi gani alikuwa na uwezo wa kupambana na maadui zake, akaitambua misimamo yake. Hapa zile tetesi za kujiua akazifutilia mbali. Akamkumbuka tena namna alivyokuwa bingwa wa mapambano ya ana kwa ana. Pia alivyoweza kupambana na mtu mwenye silaha…. Hakika Steven alikuwa mwiba! Kuhusu mtu yeyote kuweza kumuua kirahisi vile labda kwa kumnyonga ama kumpa sumu. Hili nalo akalifutilia mbali! Angeweza kufa mtu mwingine kizembe namna ile lakini sio Steve!! Gama alipingana kabisa na hisia za Steve kuuwawa kizembe. Mara ghafla akayafikiria MAPENZI. Na hapo akaketi kitako. Akajenga picha ya mfanyakazi mwenzake huyo ambaye tayari ni marehemu.  Akamkumbuka jinsi alivyokuwa anakosa raha pale anapokerwa ama anapomkosea mpenzi wake. Alikuwa anashindwa kufanya kazi kabisa na wakati mwingine hata kufanya chini ya kiwango! Yawezekana mapenzi yamemuua Steven!! Gama alijisemea huku akitikisa kichwa chake kuuunga mkono hoja ile. “Lakini mapenzi kivipi?” akajiuliza…. Akawafikiria baadhi ya wasichana ambao walikuwa wakijihusisha kimapenzi na Steve. Mariam, Subira, Recho….. Akayamaliza majina yote yale aliyokuwa akiyafahamu, akampa kipaumbele Mariam. Huyu ndiye alikuwa akitumia naye muda mwingi mara kwa mara kwa sababu Subira na Recho hawa walikuwa wake za watu hivyo ndoa zao ziliwakosesha muda wa kuwa na Steve mara kwa mara. Lakini Mariam hakuwa ameolewa na mpenzi pekee aliyekuwanaye kiuwazi alikuwa ni Steve, penzi lilianza kwa kasi kubwa lakini baadaye penzi likashuka thamani, ikawa linapita hadi juma moja bila Steve kutoka na kwenda mahali na Mariam, lawama zikaanza na mwisho zikapoa. Mariam akawa hawezi tena kumwendesha Steve! Sasa nani alikuwa akimwendesha?? Akajiuliza! Huyu nd’o anayetakikana nijue nini kimemuua Steven Marashi! Hapa kama si mapenzi basi kuna HILA zimefanyika, aidha Mariam alimuua kulipiza kisasi ama.. ama….. Gama akakosa lolote la kutabiri! Akajipa siku tatu za ziada mbele ili aweze kuanza rasmi kazi nzito kupita zote alizowahi kufanya. Kujua ni kipi kimemuua rafiki yake na kuna njama gani zinaendelea asizozijua!! Kubwa zaidi kuhusu ripoti ya hujuma ambayo anaamini Steve alikuwa ama ameikamilisha ama alikuwa amekaribia kuikamilisha. Gama akatabasamu kisha akajilaza tena. Wakati huu ni mwili na akili. Akasinzia huku fikra ya mwisho kabisa akiwa amemfikiria mtu wa kufanya naye hiyo kazi. ***** MIAKA MINNE ILIYOPITA ILIKUWA imebaki miaka minne kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tena. Chama tawala kilitarajiwa kusimamisha mgombea mpya baada ya yule wa awali kuwa anaelekea kumaliza miaka yake kumi kama katiba isemavyo hawezi tena kugombea. Anatakiwa kuwaachia wenzake. Tofauti na miaka mingine ambapo mgombea anaandaliwa mapema kabisa. Lakini hii ya wakati huu ilikuwa kinyume kabisa. Wagombea wenye sifa walionekana kuwa wawili na wote walikuwa wenye nguvu sana hivyo likawa ni jukumu la chama tawala kufanya uchaguzi sahihi ili nchi iendelee kuwa chini ya utawala wao. John Masele, waziri wa mambo ya ndani na nje ya Tanzania alikuwa ameitangaza nia yake mapema kabisa kuwa anataka kuingia ikulu. Wafuasi wake wakaanza kumuita raisi mtarajiwa, jina likazoeleka huku akionekana kukosa kabisa dosari yoyote ya kupata nafasi hiyo. John Masele alikuwa akikubalika hata kwa wapinzani, alikuwa na sera za peke yake ambazo zililenga katika kumkomboa mtanzania kiuchumi, kiutamaduni na kifikra. Raisi aliyekuwa madarakani hakufanana misimamo na Masele, hivyo alitambua wazi kuwa hataishi kwa raha tena wakati akiitwa raisi mstaafu. Alihofia bwana Masele anaweza kutumia utawala wake kumsababisha yeye aonekane hakuna lolote alilofanya wakati akiwa ikulu. Jambo ambalo kwake lilikuwa fedheha kuu. Raisi akamshawishi, Mathias Obhare, waziri wa nishati na madini atangaze nia ya kugombea pia. Huku akimsisitiza kuwa asimuhofie Masele na siasa zake kwani yeye ana watu wenye ushawishi mkubwa na pia wenye pesa nyingi, hivyo watashinda. Na hapo akamwambia kuwa mzee Matata atakuwa nyuma yake kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho watakapokuwa wakipongezana wakiwa ikulu huku yeye akiwa ni raisi. Kumsikia mzee Matata pekee haikutosha kumshawishi Mathias kukubaliana na wazo la raisi. Kitu kikubwa kilichokuwa kinamkwamisha katika hilo ni ukaribu aliokuwanao kwa John Masele kuanzia chuo kikuu walipokutana, John akawa raisi wa chuo huku Mathias akiwa makamu wake. Ukaribu huu ukaunda kama undugu, na hatimaye wakajiunga na chama tawala. Sasa John ni waziri wa mambo ya ndani na nje wakati yeye ni waziri wa nishati na madini. Raisi anataka kuwafanya maadui kwa mara ya kwanza!!! Mathias hatimaye anashawishika, waandishi wa habari wanaitwa katika mkutano. Mathias Obhare anatangaza nia ya kuwania nafasi ambayo John Masele alikuwa anawania. Kujitangaza kwa Mathias Obhare kulimshtua sana Masele, akajiuliza ni lini Obhare akawaza upinzani kama ule. Kwanza ni yeye alikuwa wa kwanza kumshawishi atangaze nia, in akuwaje sasa na yeye atangaze nia. Si bure kuna kitu hapa! akajisemea Na hapo akatambua wazi kuwa kuna hila imefanyika dhidi yake ili asiweze kuleta mapinduzi kwani alikuwa na misimamo tofauti kabisa na chama tawala japo naye alikuwa ndani yake. Kwa utulivu kabisa akaamua kukutana na Obhare na kumshawishi asigombee nafasi ile kwa sababu kwa namna moja ama nyingine ingeweza kuwaingiza katika malumbano makubwa na kuutia doa urafiki wao. Akamsihi kuwa iwapo ataachia nafasi ile basi atamchagua kuwa makamu wa raisi kama walivyofanya wakati wakiwa chuo kikuu Obhare hakutoa jibu palepale, akayafikisha yale yote kwa raisi.  Mtukufu Raisi akatumia huo mwanya kuanza kumchafua Masele mbele ya wananchi. Akasambaza maneno makali kwa wajumbe juu ya uoga wa kushindwa alionao Masele pia akaelezea juu ya tamaa ya madaraka aliyokuwa nayo bwana yule. Na hapo baraza la chama tawala likatangaza rasmi kuliondoa jina la waziri wa mambo ya ndani na nje katika kinyang’anyiro kile. Fukuto likaanzia hapo! Baada ya juma moja, jambo jingine kubwa likazuka. Mathias Obhare akatekwa na kuibiwa gari lake kisha akapigwa sana. Kipigo kilichosababisha akimbizwe Afrika kusini upesi kwa ajili ya matibabu. Zikasemekana ni hila za Masele baada ya kuzidiwa kete na mpinzani wake kisiasa. Baraza likaketi tena na kumweka kitimoto Masele ambaye alikataa kata kata kujihusisha na tukio lile, huku akisisitiza kuwa amebariki bwana Obhare kuwania kiti kile. Lakini maneno yake hayakutosha kutengua kilichokuwa kimepangwa tayari. Akiwa ameketi nyumbani na familia yake, mara akaisikia taarifa ya habari kuwa Raisi amemvua nyadhifa za uwaziri wa mambo ya ndani na nje….. huku sababu kuu ya kufanya vile ikisemekana ni kwa maslahi ya wananchi na sio chama. Jina la Masele likazidi kuchafuka huku Mathias Obhare akianza kukaa katika damu za raia wema. Wachache wenye kujitambua walihisi kuna jambo linatokea hapo katikakati. Lakini hawakuwa na pa kusemea. Lakini mtanzania mmoja ambaye alikuwa masomoni nchini uingereza alitamani sana amalize masomo yake ili aweze kuingia katika upelelezi juu ya kipi kinachotokea maana naye alitilia mashaka matukio yale mfululizo. Huyu alikuwa ni Steven Marashi, mwanausalama wa taifa aliyekuwa ameenda kuongeza elimu yake nchini uingereza. Akiwa huko akajiunga katika vikundi vya kiafrika vya kucheza ngoma na kufanya michezo ya majukwaani, fani aliyokuwa akiipenda tangu utoto wake alipokuwa shuleni. Fani ikanoga na kung’ara zaidi katika ukubwa wake. Aliporejea nchini Tanzania, akaingia rasmi katika sanaa ya maigizo. Ungeanza vipi kujua yule bwana alikuwa mwanausalama wa taifa na mpelelezi aliyekubuhu? Safari ikaanzia hapo!!! Alipojiunga na sanaa mtu mmoja tu ndiye aliyejua ni kwanini anajiunga katika sanaa, huyu alikuwa ni rafiki yake kikazi na hatimaye hadi mtaani wakawa marafiki na kushirikishana mambo yao mengine. Alikuwa ni Yakubu Gama, zao la usalama wa taifa lenye asili ya Naijeria lakini mwenye uraia halisi kabisa wa Tanzania kwa kuzaliwa. Na baada ya miaka minne Steven anakufa katika mazingira ya kutatanisha!!!  Na baada ya kifo chake mambo mengi yanajitokeza hapo katikati, Gama hakupata hata fursa ya kuonana na Sam yule mwandishi ambaye alikuwa rafiki wa karibu sana wa Steve! Hadi usiku ule aliokwenda kumwekea dhamana.  Dhamana iliyotoka wa mtukufu raisi moja kwa moja, kupitia amri ya IGP. Dhamana iliyokuwa na makusudi ndani yake! Kuna kitu kilikuwa kinatafutwa na Sam alidhaniwa kuwa anaweza kuwanacho ama kuwezesha kupatikana kwacho! Ni kitu gani hicho? Hili swali linabaki katika kichwa cha Yakubu Gama ambaye yu hai sasa lakini akiwa amejeruhiwa! Yakubu Gama anaapa kuwa atapeleleza hatua kwa hatua hadi ajue ni kitu gani kilimuua Steve! Huenda katika utafiti huo akatambua pia ni nani anayeitwa BVB. ****

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni