Alhamisi, 24 Desemba 2015

HILA NO.2

SEHEMU YA PILI Tina kwa upande wake hakuweza kabisa kupambana na kitanda ili kimpe usingizi, alikuwa na wasiwasi uliosababishwa na kutoweka kwa Sam huku akiongozwa na maaskari, kila mara aliitazama simu yake kama vile muda wowote ule inaweza kutoa mlio wowote ambao utamaanisha kwa Sam anampigia simu kumjuza kuwa yu njiani anarudi mahala walipokuwa wameamua kujipumzisha siku hiyo. Alisubiri kwa dakika arobaini na tano bila majibu yoyote zikaongezeka nyingine kumi na tano likawa saa zima bila dalili zozote za simu ile kuita. Uvumilivu ukaanza kutoweka wivu ukazidi kumtafuna na sasa akajihisi hasira kwa mbali. Akazibonyeza namba za Sam kama vile anayejaribu kujionyesha ni jinsi gani ana kipaji cha kukariri. Baada ya zoezi hilo akavutiwa na kitufe cha kijani ambacho kama akikibonyeza mwenye namba zilizopo mbele ya kioo cha simu yake atapokea simu yake. “Simu unayopiga….inatumika kwa sasa…the number you are dialing is busy” Tina akasubiri sekunde kadhaa akapiga tena simu ya Samwel jibu likawa hilo hilo, akajisikia kama anakabwa kooni na kitu kutoka katika mwili wake. Zilikuwa ni hasira.  Samwel anaongea na wanawake zake!!! Aliwaza kisha akaitupa simu yake kitandani. Akaitazama kwa jicho la hasira jinsi ilivyokuwa ikiviringika, lakini ghafla akaikodolea macho makali, akakitazama kishikio chake kisha akaikwapua kama vile alikuwa katika kunyang’anyana na mwenzake. Akatoa tabasamu la kujilazimisha kisha akapumua kwa nguvu. Lile donge la hasira likalegea kidogo.  Ile simu haikuwa ya kwake, kumbukumbu za kumbadilishia Samwel simu wakati akiwa mlangoni akizungumza na polisi walioondoka naye. Simu zao zilikuwa zinafanana kila kitu na zilinunuliwa siku moja, kama zisingekuwa na vishikio basi ilikuwa ngumu kuzitofautisha ni kishikio hiki kilimfanya Tina kugundua tendo alilolifanya tendo ambalo kwa namna yoyote lazima lingekuwa kero kwa Samwel iwapo ataligundua, na ilikuwa lazima aligundue. Wakati wote Tina alipokuwa akimpigia Samwel kumbe alikuwa anajipigia mwenyewe na hata Samwel wakati anampigia Tina na yeye alikuwa anajipigia mwenyewe. Tina alirekebisha makosa yake na kubonyeza namba zake katika simu ile ili aweze kuzungumza na Sam lakini alikuwa amechelewa simu ilikuwa imezimwa tayari. Tina akataharuki asijue la kufanya!!! Alikuwa amefanya kosa moja kubwa sana. Kosa ambalo lingeweza kumgharimu kwa muda mrefu. Kosa lililosababishwa na wivu wa kimapenzi. Ni wivu huu sasa unamwingiza matatani!!! __________ Katika chumba cha mahojiano, chumba kilichokuwa na faragha kuu kuliko vyumba vingine ambavyo Samwel Mbaule aliwahi kufanyiwa mahojiano. Faragha hii ilimshangaza sana lakini bado hofu kwake ilikuwa ni ndoto ya kufikirika na kusadikika. “Samwel Mbaule!! Mwandishi wa kujitegemea aliyebobea” sauti ya bwana aliyekuwa anamuhoji Sam ilikoroma katika hali ya ujivuni. Sam akatoa tabasamu la kinafiki bila kutia neno juu yake. “Mbona mmemuua bado mapema?” swali hilo likamshtua Sam lakini hakutaka kuutangaza mshtuko huo, akaendeleza tabasamu lake lile le kughushi lakini safari hii akauliza kidogo, “Nani huyo?” Mpelelezi wa kesi hiyo akatoa kicheko cha kusanifu. Huenda alikuwa akilipiza karaha alizozipata kutokana na tabasamu la Sam. “Bwana Samwel…hii ni simu yako sivyo!” “Kama hakuna ujanja wowote uliofanyika hiyo ni simu yangu!” “Ujanja gani wa kukufanyia wewe, kwa lipi ulilotukosea.” “Lolote ambalo silijui.” Alijibu kwa kiburi kiasi. “Kwa hiyo hii simu ni yako.” “Nilikwishajibu swali lako.” “Na tangu umuazime mtu ni masaa mangapi yamepita?.” “Sina kumbukumbu ya kumuazima mtu yeyote yule.” “Vizuri sana..aah!! umesema hujaazima mtu eeh!!” “Hukunisikia nikikujibu??” alijibu kwa kukaripia Bwana yule mwenye nywele nyingi zilizoota bila utaratibu maalum akashtushwa na jibu hilo, akamkodolea macho Sam. Kiburi chako kimefikia tamati!!! Aliwaza huku akijikuna kwa kutumia kalamu yake isiyokuwa na wino wa kutosha. “Hii ni simu yangu na hii ni simu yako uliyokiri kuitambua. Weka namba zako hapa na uipige simu yako.” Alitoa maelekezo hayo, Sam akayapokea kwa utulivu na kuyafanyia kazi. Aliingiza namba zake kwa utulivu. Akapiga na kisha akaweka katika sauti ya juu ili kila mmoja aweze kusikia. Simu ikaanza kuita. Sam macho yakamtoka lakini hayakufikia kiwango cha yule mpelelezi ya kwake yalitoka mara mbili na kuwa kama panya mkubwa aliyenaswa katika mtego uliowekewa nyama yenye harufu ya kuvutia na yeye akategeka. Asubuhi mtegaji anakutana na macho yaliyokodolewa yakisaidia kuielezea mauti yake ilivyokuwa ya kuogofya na kushtukiza. “Mbonaa….eeeh!! ina maana…hebu ngoja…” alizungumza huku akitweta mpelelezi wa kesi ile. Kisha akachomoka kama mshale akakifunga kile chumba cha mahojiano na kutimua mbio baada ya dakika mbili alirejea na askari wawili, Sam aliwakumbuka kuwa ni hao ambao walimweka mahabusu usiku uliopita, na hapo walikuja kumchukua tena akawa amerejeshwa mahabusu chini ya ulinzi mkali bila kufanyiwa mahojiano yoyote yale. Samwel bado hakujiruhusu kuogopa chochote, aliamini hakuwa na hatia ya aina yoyote.  **** “Hii ni simu yangu na hii ni simu yako uliyokiri kuitambua. Weka namba zako hapa na uipige simu yako.” Alitoa maelekezo hayo, Sam akayapokea kwa utulivu na kuyafanyia kazi. Aliingiza namba zake kwa utulivu. Akapiga na kisha akaweka katika sauti ya juu ili kila mmoja aweze kusikia. Simu ikaanza kuita. Sam macho yakamtoka lakini hayakufikia kiwango cha yule mpelelezi ya kwake yalitoka mara mbili na kuwa kama panya mkubwa aliyenaswa katika mtego uliowekewa nyama yenye harufu ya kuvutia na yeye akategeka. Asubuhi mtegaji anakutana na macho yaliyokodolewa yakisaidia kuielezea mauti yake ilivyokuwa ya kuogofya na kushtukiza. “Mbonaa….eeeh!! ina maana…hebu ngoja…” alizungumza huku akitweta mpelelezi wa kesi ile. Kisha akachomoka kama mshale akakifunga kile chumba cha mahojiano na kutimua mbio baada ya dakika mbili alirejea na askari wawili, Sam aliwakumbuka kuwa ni hao ambao walimweka mahabusu usiku uliopita, na hapo walikuja kumchukua tena akawa amerejeshwa mahabusu chini ya ulinzi mkali bila kufanyiwa mahojiano yoyote yale. Samwel bado hakujiruhusu kuogopa chochote, aliamini hakuwa na hatia ya aina yoyote.  **** Mkuu wa kituo cha polisi alikuwa amejiinamia huku akichokonoa meno yake kwa kutumia njiti ya kiberiti, mezani palikuwa na soda aina ya Sprite iliyokuwa ikitoka mfano wa jasho laini lenye kuvutia, hali iliyoonyesha kuwa ndani ya muda mfupi ilikuwa ikihangaika katika baridi kali kutoka katika jokofu. Aliitazama soda ile huku akiilani nyama iliyokuwa imejificha katika fizi zake na kumletea usumbufu. Baada ya kufanikiwa kuchokonoa na kutoa alichotoa, aliusogeza mkono wake ukaitwaa ile soda na kukiondoa kizibio cha juu, akapiga funda mbili kubwa, kisha akatulia kusikilizia utamu, akataka kuongeza funda jingine simu yake ya mkononi ikaita. Bwana Sabatho, alikuwa ni mtu anayependa sana kutilia maanani kila jambo linalokatiza mbele yake, hata kama litakuwa limeingiliana na chochote alichokuwa akifanya, tabia hii ilimfanya agombane sana na mkewe na hata watoto wake wangekuwa na uwezo wangemgomea asiwe anatoka hovyo nyumbani tena bila taarifa. Mkewe alihangaika na hatimaye akazoea.  Ilikuwa saa mbili na dakika kadhaa asubuhi, ilikuwa nadra sana mzee huyu kustafutahi pamoja na mkewe lakini siku hii waliifanya ya kukumbukwa. Baada ya mlo huu walikuwa na mazungumzo na mtoto wao wa kiume aliyekuwa anaingia kidato cha kwanza katika shule ya bweni, walihitaji kumpa nasaha za hapa na pale huku baba yake (Mzee Sabatho) akiwa ameahidi kumsindikiza kwa kutumia gari yake ya kazini hadi kituo cha mabasi ambapo alikuwa amekata tiketi. Huku mkewe akiwa chumbani akijiandaa na mtoto akiwa anakaribia kumaliza kufunga mkanda wa nguo yake. Simu ya mzee Sabatho iliita, akaahirisha kupiga funda la soda iliyokuwa mbele yake akapokea simu. “Simu aliyonayo sio ile inayohusika katika tukio, kuna jambo jingine jipya!!” alipewa maelezo hayo mafupi lakini akaelewa kwa kirefu. “Nakuja huko sasa hivi…fatilia ni wapi simu hiyo inapatikana na aliyenayo simu hiyo akamatwe mara moja!!!” “Sawa!!” upande wa pili ukajibu. “Na huyo Samwel asiachiwe huru kwanza mpaka afahamike aliyekuwa na simu hiyo.” Alitoa maelezo hayo kisha akakata simu. Fikra kuhusu mke na mtoto wake, alizisahau mara moja na hata ule utamu wa ile soda ukaishia pale pale. Mzee Sabatho akatoweka haraka, akiwa katika kuondoka mtoto na mkewe waliishia kuisindikiza gari yake kwa macho. Mama mtoto akazisikia dalili zote za kutoa machozi lakini alijikiza kwa kuwa alikuwa sambamba na mtoto wake. “Allen nakuja kukupeleka achana na babako tushamzoea” mama Allen aliaga na kukimbilia chumbani mwake. Huko alilia kilio cha kwikwi hadi akajiridhisha mwenyewe ndipo akatoka ndani akiwa tayari ameunawa uso wake vyema. **** Christina Elisha Prosper ama Tina kama alivyozoeshwa kuitwa tangu utotoni na sasa lilikuwa limezoeleka katika kila kinywa cha mwanadamu aliyemfahamu hata kwa muda mfupi, sasa alikuwa katika hofu kubwa sana simu ya Samwel ilikuwa mikononi mwake na hata ile ya kwake ambayo ilikuwa mikononi mwa Samwel sasa haikuwa ikipatikana, wivu haukuwa na nafasi tena bali uoga juu ya nini kimemsibu mpenzi wake huyo ambaye walikuwa katika hatua za kuitangaza siku yao ya kuutangazia umma kuwa wao ni mwili mmoja kikamilifu. Tina alikurupuka kitandani majira ya saa moja na nusu asubuhi. Mkononi alikuwa ameikamata kikamilifu simu ya Samwel, hakujua ni muda gani alipitiwa na usingizi lakini alitambua kuwa alisinzia. Alikimbilia bafuni akanza kujiuliza endapo aoge au asioge, kwani ni masaa kadhaa yaliyopita alikuwa ameoga akiwa na Sam wake. Akiwa katika kujiuliza simu ya Sam iliita, akapokea baada ya kuona jina. Akamtaka radhi mpigaji kuwa mwenye simu ameisahau nyumbani. Alidanganya!!!  Akaanza kuvua nguo zake ili aweze aidha kuoga ama kuyabadili mavazi yake kwani bado hakuwa na jibu muafaka. Aliposalia kama alivyozaliwa alisikia simu ikiita tena kisha ikakatika. Aliiendea na kuitazama akakuta ni namba mpya, akaanza kuuhisi usumbufu atakaoupata kutokana na kuwa na simu ya Sam. Akiwa katika kufikiria hilo mara ikaita tena akaipokea. “Samahani kaka naitwa ….” “Samahani, mwenye simu ameisahau nyumbani.” Akamkatisha. Mchezo huo ukaanza kumkera zaidi, akatamani kuizima simu ya Sam lakini uoga ukamwingia vipi kama Sam atampigia na amkose. Ama vipi kama ataiharibu miadi ya Sam. Aliamini atamkera mno. Akaiacha ilivyo akaamua kuingia kuoga. Ni heri angechukua maamuzi ya kumkera Sam kuliko kuiacha simu ile ikiwa hewani ama ni bora asingeoga aondoke tu, huenda angejiokoa na janga hili. Hakuzima simu na aliingia kuoga!!! Kosa kubwa lisiloonekana madhara yake mara moja!!! Tina akiwa katika hali ile ya kutaharuki alioga kwa pupa huku akisahau kuzifunika nywele zake ndefu zisiweze kuingiliwa na maji, alikuwa katika hali ambayo hakuwahi kuwa nayo hapo kabla. Hali ya hofu iliyopitiliza. Hakujiremba kama ambavyo hufanya siku zote, hakutumia dakika kumi na tano kuzichana nywele zake katika mitindo ya kisasa huku akifurahia lawama za mpenzi wake Samwel kuwa anamchelewesha kazini. Leo hii Tina alichomoka mbio mbio akiwa hajazipanga nguo zao chache katika mabegi yao kwa mpangilio maalum hivyo mabegi yale mawili kuvimba sana.  Alifika mapokezi akiwa katika hali ile ile ya ajabu ajabu, laiti kama dada wa mapokezi asingepigiwa simu kutoka vyumbani huenda angemuhoji Christina kulikoni akawa vile. Bahati mbaya hakupata nafasi hiyo. Tina akawa ametoweka baada ya kulipia bili za chakula walichokula usiku uliopita. Mwanga wa jua hafifu likiwa bado na rangi nyekundu nyekundu uliyasabahi macho yake makubwa mithili ya gololi ndogo. Akiwa katika kuyalazimisha macho yake yaizoee hali ya pale nje alijikuta akigongana na mwanaume mkakamavu sana kwa bahati mbaya. Maumivu ya bega aliyoyapata yalimfanya amlaani kimya kimya huyo mtu ambaye hakupata hata nafasi ya kumwangalia mara ya pili. Mabegi mawili moja kila mkono, jaketi moja pamoja na mkoba wake kwapani huku usoni akiwa hajiamini Tina alikuwa kama anayetoroka. Kelele za madereva teksi zikinadi biashara yao zilimchanganya sana dada huyu akajikuta akiwa njia panda, hata alipokwapuliwa begi lake na dereva mmoja kisha likaingizwa garini hakuwa na kipingamizi alijikuta amejitoma garini. "Wapi bosi??" Dereva alimuuliza abiria wake. Abiria akawa bubu kwa muda hakusema lolote. Dereva akamwacha afikiri. Hakuna alichokuwa anafikiri binti huyu. "Ndio dada!!" "Ehh!! unasema?" aliuliza Tina katika hali ya mshtuko. "Tunaelekea wapi?" aliuliza kwa ukarimu dereva huku akiitia moto gari yake kwa mbwembwe. "Mhhhh!!! ahaaa!! twende hapa nanii hapa.....Sinza Kamanyola" alijibu Tina baada ya kujiuma uma kwa sekunde kadhaa. Sinza Kamanyola palikuwa nyumbani kwa mama yake Tina, mama huyu licha ya kwamba hakuwa mama mzazi wa Tina ambaye alikuwa ni yatima, alikuwa anampenda Tina huenda kuliko mama yake mzazi aliyetangulia mbele ya haki. Ni eneo hili Tina aliamini lilikuwa sahihi kwa ajili ya pumziko na ushauri nasaha kutokana na jambo lililotokea. Mama huyu mpole aliyefahamika kwa jina la Mama Tina ama Naomi kwa waliyelingana naye umri alikuwa na historia ya kuwahi kuwasuluhisha Tina na Sam mara kadhaa walizokuwa katika mitafaruku. Hivyo Tina aliamini kuwa ulikuwa wakati muafaka kwa mkongwe huyu kutenda miujiza yake tena, kwani tayari Tina alikuwa na wasiwasi kuwa Sam atakuwa amekasirishwa sana na kitendo cha kubadilishiwa simu. Dereva alitii amri akajifunga mkanda lakini hakumsisitiza Tina kujifunga kama yeye. Safari ikaanza. Dereva huyu ambaye mwanzoni Tina alitegemea kumpa heshima ya shkamoo ila akajikuta amesahau kutokana na taharuki alikuwa mkimya sana lakini baada ya safari kunoga ni kama alikuwa na yeye ananogesha kwanza mdomo wake. Alianza kupiga stori za hapa na pale Tina alikuwa kimya akimsikiliza bila kumuelewa. Dereva hakuchoka kumburudisha abiria wake huyo katika gari yake hii isiyokuwa na redio. "Hatimaye wamemuua halafu mi nilijua tu!!! hafiki mbali huyu, hakujiwekea kinga tatizo.. yaani vijana wa siku hizi bwana" "Nani tena?" kwa mara ya kwanza Tina akajikuta amevutiwa na hiyo mada akauliza swali. "Si huyu muigizaji wenu huyu....nani wanamuita...nani watoto wangu wanampenda sana huyuu...Steve...ewalaaa Steve Marashi" alijibu dereva huku akijikuna ndevu zake kwa fujo kulitafuta jibu. "Steven yupi??" "Huyu Steve Marashi huyu we hujasikia?" "Acha masihara wewe Steve amekufa lini?? mbona mi sijasikia wala..acha utani wewe!!!" Tina alibisha huku akihitaji maelezo zaidi. "Ndo nakwambia sasa waemuua jana mbona..mi nilijua tu…" alielezea kwa manung’uniko. Dereva akatoa tabasamu hafifu baada ya kuona sasa Tina anamuunga mkono maongezi yake. "Babu wewe Steve huyu ninayemjua mimi.." "Ndio huyo ameuliwa na huyu mtoto nani huyu.......", alitaka kuzungumza akakatisha maongezi yake kisha akaendelea, "Hiyo gari inatufata sisi au?? maana muda kweli" aliuliza yule dereva, Tina akageuka nyuma kutazama kwa ushahidi tu bila msaada. "Kata hapo kulia..." alitoa maelezo hayo bila kuujali wasiwasi aliokuwanao dereva. Dereva akatii amri, suala la gari kuwafuata kwa nyuma likaishia hapo. Baada ya dakika tatu tangu wakate kona gari ikasimama, Tina akamwona mama yake walipotazamana wakajikuta wanatabasamu, tabasamu lililoutangaza upendo wao. Japo macho ya mama yalikuwa, mekundu na yamevimba hali hiyo haikumshtua sana Tina. Tabasamu lile halikudumu sana, likayeyuka bila wao kujua kama limetoweka tayari na kuwa mshangao. Mshangao wao ukamezwa na vumbi kali lililotokana na breki kali za gari mbele ya nyumba ya mama yake huyo wa kufikia. Dereva aliyekuwa anasubiri malipo yake na yeye aliungana na wanawake hawa kushangaa lakini alikuwa ni Tina aliyezidi kushangaa zaidi baada ya wanaume waliojengeka miili kutoka katika ile gari aliyokuwa imehisiwa na dereva kuwa imewafungia mkia kumvamia na kumzingira. "Askari....upo chini ya ulinzi!!!" alipewa maneno hayo mafupi kisha bila kuuliza swali wakamtia katika bangili zisizopendwa na jinsia zote bangili hizi za rangi ya shaba zilibatizwa jina la 'pingu'.  Kwa mara ya kwanza katika mikono ya Tina. Bila maelezo wala majibu ya maswali yake ya 'nimefanya nini' aliongozwa hadi katika gari waliyokujanayo. Mama, damu ikawa nzito kuliko maji akawakimbilia polisi wale na kuwavamia akiwa na maswali mengi, hakujibiwa hata moja zaidi ya kusukumwa na kubaki akigaa gaa chini akilia bila msaada wowote. Dereva wa teksi hakukumbuka kama alikuwa anadai pesa ama la aliwasha gari lake akatokomea huku akiilani siku hii iliyoanza vibaya sana kwake. Aliondoka huku akiacha msiba mkubwa. Majirani ambao waliamkia kuzungumza habari juu ya msiba wa Steve sasa waliweka hayo makubwa yasiyowahusu wakavalia njuga suala hili zito linalowahusu la mama Tina!!!! ****** 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni