SEHEMU YA 8 MAMA LAO ni kama alimchezea shere mhanga wake kwa kujifanya kuwa hamtazami na wala hana muda naye hivyo alikuja kwa pupa na alipompita sekunde kadhaa tu upesi Yule mama akafyatuka na kumnasa Ninja mguu wake wa nyuma. Ninja asiyetarajia lile jambo akapepesuka na kisha akatua chini kama mzigo. Alipojaribu kusimama, Mama lao akawahi kumwamsha vyema kisha akiwa amemkwida shati lake vyema akampa shambulizi la kushtukiza. Akambamiza kichwa chenye uzito wa haja na palepale akapasuka vibaya sana. Yule bwana akiwa amepagawa alijaribu kujitoa mikononi mwa mama lao lakini haikuwa kwa wepesi kama alivyoweza kudhani. Mama lao alikuwa imara sana! Akamkata gwala akaanguka chini. “Wewe ni nani na aliyekutuma ni nani? Jibu mara moja ama napasua makende yako” Mama lao alifoka huku mkono wake ukiwa ukiwa umezikama sehemu za siri za Ninja. Yule mwanaume hakutegemea kujikuta katika suluba kubwa namna ile tena kutoka kwa mwanamke. Sam alikuwa amepigwa na bumbuwazi, akili ilikuwa imesimama akishuhudia undava wa yule mwanamke, miguu ilikuwa mizito sana na akili ilikuwa imesimama. Alikuja kushtushwa na watu ambao walikuwa wakishangilia ugomvi ule na yeye akaanza kupiga hatua kusogea alipokuwa mama lao. Lakini kabla hajafika likatokea jambo ambalo lilizua kizaazaa kilichoitikisa Magomeni na kufunga barabara kwa muda mrefu sana. Ukasikika mlio mkali sana wa bunduki, kikasikika kilio cha mama lao. Kisha damu ikatapakaa katika miili miwili iliyokuwa katika ugomvi. Polisi waliokuwa eneo la ajali walitoa bunduki zao upesi na kuanza kuangaza huku na kule waweze kutambua ni wapi shambulio lile lilitoka. Lakini hawakuambulia kitu chochote… Sam alipigwa butwaa miguu ikaishiwa nguvu, mwili ukamsisimka alivyotazamana ana kwa ana na lile dimbwi la damu. Huku mama lao na Ninja wakiwa wametulia tuli wakiwa wamekumbatiana. Kwa jicho la harakaharaka la kibinadamu ungetambua kuwa hawakuwa na chembe ya uhai. Sam, alitaka kuiruhusu akili yake ipagawe lakini akajionya na kulikumbuka lile angalizo alilopewa na yule bwana ambaye alimuwekea dhamana ya kimaajabu usiku wa manane. Akakumbuka alielezwa kuwa awe makini! Sam akajitoa ufahamu na kujifanya hamjui mama lao. Alijisikia vibaya kumsaliti yule mama lakini alitambua kuwa lile halikuwa tukio la kawaida na laiti kama angejiweka mbele lazima angejiingiza matatani, hasahasa akiikumbuka kamera yake ambayo ilikuwa na tukio la bwana Ninja kuunda kwa maksudi kabisa ajali ambayo sasa ilikuwa imeondoka na uhai wa mzee Marashi, baba mzazi wa Steven Marashi. *** MAJIRA yaa saa mbili usiku simu ya mkononi ilitoa mwanga kumaanisha kuwa kuna ujumbe ama simu inaingia, bwana Robert Massawe, mkaribu mkuu msaidizi wa jeshi la polisi aliitazama Katina namna ya kuvizia kana kwamba akiitazama upesi itazimika. Hiyo ilikuwa ni simu yake ya dharula sana ambayo walikuwa wakiifahamu watu wachache mno. Ilikuwa kawaida ya bwana huyu ambaye alikuwa na miaka arobaini na tano kuzima simu zake na kutafakari kwa kina kila linapotokea tukio ambalo linatatanisha. Alikuwa akiiacha wazi simu yake moja tu kwa ajili ya watu maalumu. “Goddamn! Shit!!” alifoka baada ya kutambua mpigaji wa ile simu. Alijua kuwa mpigaji alikuwa na kawaida ya usumbufu, na usumbufu huu ulikuwa na chanzo chake. Alitamani sana asiipokee simu yake, lakini ilikuwa lazima aipokee. “Naam! Mheshimiwa sana Matata…” alizungumza bwana Robert kwa nidhamu na sauti ya chini. “Pole sana nimekusumbua ulikuwa umelala… niwie radhi bwana…” sauti ya mzee Matata ilizungumza na kisha akashusha pumzi kumsikiliza bwana Robbert. “Usijali mkuu.. nilikuwa sijalala bado.” Alijibu kwa kuchangamka, changamko la kujilazimisha. “Pole sana kwa matukio mfululizo yanayolitokea jeshi la polisi, hakika mnapitia kipindi kigumu sana katika hili….” Akavuta pumzi kisha akaendelea. “Ehe! Nambie vipi nasikia leo kuna ajali imetokea na risasi zimerushwa huku watu wakipoteza uhai…” Kauli hii ilimkera Robert, lakini ilikuwa lazima ajieleze kitu ambacho alijua wazi kabisa kuwa alikuwa anaukiuka utaratibu wake wa kazi lakini angefanya nini mbele ya mzee Matata, tajiri ambaye analifadhili jeshi la polisi mara kwa mara. Robert akamueleza mzee Matata kuwa kijana asiyefahamika jina lake amepigwa risasi kifuani na kufa palepale huku yule mwanamke ambaye alikuwa akipambana naye bila kujulikana chanzo akiwa amepoteza fahamu. Mzee Matata akakata simu bila kuaga. Ilikuwa kawaida yake!! KILE kitendo cha mzee Matata kutawala baadhi ya mazingira katika idara mbalimbali serikalini ilimkwaza sana mzee Robert na kwa namna moja ama nyingine alihisi kuwa si jambo salama kabisa na linaweza kuzua madhara makubwa kwa serikali. Mzee Robert alitamani sana kurudisha siku nyuma ili arekebishe yaliyotokea hapo zamani kidogo lakini haikuwezekana. **** Mzee Matata alishusha pumzi zake kwa juhudi huku akiketi katika kiti chake cha kuzunguka. Akafanya mfano wa tabasamu na kisha akampigia kijana aliyeagizwa maalumu kabisa kwa ajili ya kufuatilia nyendo za Ninja aliyeagizwa kumuua mzee Marashi kwa ajali ya kukusudia. Tabasamu lake lilinoga zaidi alipoifikiria shabaha ambayo kijana yule aliwahi kumfyatua Ninja baada ya kuingia katika mtafaruku usiojulikana. Ni hivyo alikuwa amemuagiza afanye iwapo Ninja atasukwasukwa na jambo lolote. Mzee Matata alikikuna kipara chake, kisha akatoa cheko la dharau huku akiitazama picha ya mtukufu raisi iliyokuwa imebandikwa katika ofisi yake. “Congratulation Mr President….” Akaisemesha ile picha iliyokuwa inatabasamu wakati wote. Hakumkumbuka mama lao….. Labda kwa sababu hakujua nini kilitokea!!! **** Samwel Mbaule alitoweka eneo lile akiwa ametaharuki, mapigo ya moyo yalikuwa juu sana na alijihisi yu katika matatizo zaidi. Hakugeuka nyuma licha ya watu kadhaa ambao ambao awali walimuona akiwa na mama lao kumuita. Sam aliingia katika bajaji na ghafla akajikuta akimwamrisha mwenye Bajaji ampeleke ofisi za gazeti la HAKI, ofisi ambazo alikuwa akifanya kazi pale. Hakujua ni kwanini alifikiria kwenda huko lakini hakubadili maamuzi. Akaendelea kuamini kuna kitu huko ambacho kinaweza kumpa nafuu ya kimaamuzi. Majira ya saa sita mchana alikuwa amesimama nje ya ofisi za gazeti lao. Mlinzi ambaye alikuwa amezoeana naye sana leo hii alionekana mwenye wasiwasi. Hata wakati anaandika jina lake kuwa ameingia ndani ya ofisi hizo, mlinzi yule alikuwa mkimya sana. Hilo hakushtushwa nalo, akaingia mapokezi… ile anaonekana kwa yule dada wa mapokezi, macho yakamtoka pima yule dada na kujikuta akiliita jina la Sam zaidi ya mara mbili hovyohovyo. Sam akawa wa kushangaa tu…. Akamsalimia na kumpita, akafika ofisi kuu. Wafanyakazi walisimama kufanya kazi wakabaki kumtazama yeye….. alifadhaika sana na kujikuta akishindwa walau kutoa salamu. Alijitazama iwapo alikuwa na mapungufu yoyote lakini hakuambulia kitu chochote kile katika mwili wake. “Jamani, kwema?” alijikaza akasalimia. Lakini ni wafanyakazi wachache sana waliojibu tena kwa sauti ya chini mno. Akataka kupuuzia na hapa ili aweze kukiendea kiti chake. Jicho likawa la kwanza kuwa shuhuda, hapakuwa na kompyuta katika meza yake. Kiti kilikuwepo lakini pia lilikosekana koti lake ambalo alikuwa analiacha ofisini kila siku. Sam akapigwa bumbuwazi asijue ni kitu gani kinaendelea hadi ofisini. “Jamani mbona… eeh! Mbona kiti changu sikielewielewi ndugu zanguni…” alihoji lakini hakupata jibu. Kila mmoja alikuwa akimtegea mwenzake aweze kumjibu Sam, lakini hakuna aliyesema kitu. Walionekana kuwa waoga. Sam, akaona kwamba kuendelea kushangaana haisaidii kitu, akaufungua mlango wa mwanamke wa makamo kabisa ambaye alikuwa akiwazidi wafanyakazi wote wa gazeti la HAKI na hivyo wakazoea kumuita bibi, hata jina lake halisi lilisahaulika. “Shkamoo bibi…” Sam alimsalimia mwanamke yule ambaye alikuwa amejikita katika kompyuta akifanya kazi yake ya uchapishaji. “Marahaba….” Alijibu bila kunyanyua uso wake. “Bibi… ni nini kinatokea hapa… maana sielewi kitu.” Sam alihoji, na mara hiyo yule bibi akanyanyua uso. “Astakha Firullah” yule mama alibinuka na kiti chake kurudi nyuma huku neno lile likimtoka kwa sauti yenye kitetemeshi. Sam akamsogelea zaidi na kumuuliza nini kinasababisha yote hayo. Yule mama mtu mzima bado hakuweza kusema bali alikuwa anatetemeka tu. Wazo la upesi limkamvamia Sam, akauendea mlango na kuufunga kwa funguo, hakutabasamu tena badala yake macho yake makali yakamtazama yule mama. “Usiniue Sam usiniue” yule mama akajitetea huku hofu ikiwa imetanda waziwazi. Kauli ile ikamshtua Sam, lakini hakutaka kutetereka akaendelea kukazia. Hatimaye yule mama akatoa maelezo huku akitetemeka. Akamweleza Sam jambo ambalo lilizidi kumshangaza. Yule mama akamweleza Sam kuwa mkurugenzi wa kampuni yao aliwaeleza kwa kifupi kabisa kuwa wasijiweke karibu na Sam kwa sababu ni muuaji wa kutisha na anajihusisha na watu hatarishi sana. Pia amemuua Steve Marashi. Sam alibaki mdomo wazi, akarudi kinyumenyume akaufungua mlango na kutoka nje, hatua kwa hatua akaufikia mlango na kutoweka bila kuaga. Alipofika nje alijikuta asiyekuwa na uelekeo, aliyoyasikia ofisini yalikuwa yamemvuruga kupindukia. “Sasa kama mimi muuaji mbona sikamatwi tena, mbona hata taarifa zangu sizisikii kwenye vyombo vya habari… hawa watu ni akina nani wanaotaka kunichafulia jina namna hii jamani….” Alijiuliza kisha akajiona yu yatima haswa. Hatua kadhaa mbele akakutana na Bajaji, akapiga mluzi kumuita dereva mara akasikia mtu akiita jina lake. Akageuka na kumwona mtu akijaribu kumkimbilia, Sam akatambua kuwa atakuwa ni mfanyakazi mwenzake anataka kumuuliza maswali ya kipumbavu ambayo yanaweza kumkoroga zaidi. Akaingia ndani ya Bajaji upesi na kumuamuru dereva aondoe hakutaka kuzungumza na huyo bwana aliyekuwa akimuita, safari hii hakutaka kurejea nyumbani kwake moja kwa moja, bali alienda moja kwa moja nyumba ya kulala wageni. Akachukua chumba na kujipumzisha akiitafakari siku ilivyokuwa na mshikemshike na ni kwa namna gani ilikuwa inamalizika. Hakumkumbuka mtu aliyekuwa akimuita!! Amkumbuke ili iweje? Alibaki kumuwaza Tina wake pamoja na ule mkanda wa ngono ambao hakuwa amemshirikisha mtu yeyote. *** MAMA LAO ASAKWE AUWAWE! KOSA kubwa walilolifanya polisi waliowekwa kumlinda Mama lao akiwa hospitali ni ile hali ya kumchukulia kuwa yeye ni mwanamke. Na pia kwa ile hali ya kuchafuka na damu waliamini kuwa alikuwa amejeruhiwa na walikuwa wakitimiza wajibu tu huku wakiamini kuwa yule mwanamke hawezi kuupata uhai wake tena. Hawakujua kuwa hakuwa amejeruhiwa na ile risasi bali ililengwa katika kifua cha yule kijana na kukipasulia mbali. Kilichomzimisha mama lao ni ule uoga tu!! Polisi hawakumfunga pingu, walimwacha huru wakati dripu zikipishana katika mishipa yake ya damu. Majira ya saa nane usiku mama lao alirejewa na fahamu zake. Akatulia kwa muda bila kuweweseka, ikawa kama bahati kumbukumbu zake hazikuwa mbali sana. Akayafumba macho yake! Akabaki katika namna ileile ya kupoteza fahamu lakini akizivuta vyeama pumzi zake. Alifanya vile ili kupata uhakika wa usalama wa eneo lile. Ni bila kujua kuwa ile ilikuwa siku yake ya kuingia katika utata mkubwa zaidi maishani mwake. Baada ya takribani dakika thelathini tangu azinduke alisikia hatua za watu zikijongea katika chumba alichokuwa amelazwa. Aliisikia sauti ikiwaelekeza kwa mbali juu ya kitanda ambacho amelazwa. Walikuwa wanaume wane. Mama lao akafunua jicho lake kwa upenyo mdogo sana, akatazama kushoto kwa na hatimaye akaziona sura. Mkojo ukapenya katika nguo yake, tumbo likaanza kumkata. Alikuwa anaonana moja kwa moja na wanyakyusa ambao walimteka Sam na kisha kumrejesha akiwa amezimia, walikuwa ni walewale walio katika mtandao wa mawaziri kwa jinsi alivyowasikia siku walipoenda kula katika banda lake. Akiwa hajalifumba jicho lake bado, aliwaona wanyakyusa wale wawili wakisemezana kikabila. Walikuwa wakipanga mpango wa papo kwa hapo na mara kila mmoja akagawana mtu wake, wakawatia kabali wale askari wawili na kisha kuwadunga sindano. Waliendelea kuwadhibiti hadi walipolainika kabisa. Wakawachukua na kuwasukumia uvunguni mwa vitanda. Kisha wakasemezana kinyakyusa tena, wakakumbushana juu ya maelekezo ya mkuu wao wa kazi. Kuwa kama yule mama yupo hai aondolewe pale hospitali na kisha auwawe na kama amekufa tayari basi mzoga uachwe hospitali. Kijana mmoja akainama na kuyasikiliza mapigo ya moyo ya mama lao ambaye alikuwa akiendelea kujikojolea. “Mzima huyu… si tumdunge na yeye sindano afe hapahapa au?” alimwomba ushauri mwenzake…. Kusikia hivyo mama lao akahisia anazikosa pumzi zake, mapigo ya moyo yakazidi kwenda kasi lakini hakutaka ajulikane kuwa amezinduka, lakini akajiapia kuwa wakitaka kumdunga sindano lazima aanzishe timbwili. “Kaka eeh! Tufuate tulichoagizwa, hujui bosi ana maana gani aisee… je kama hizi sindano haziui mapema… hebu acha bwana mambo yako….” Mwenzake alimpinga. Mama lao akaipata nafuu kidogo…. Mara mirija ikatolewa na yeye akabebwa mzegamzega. Akaendelea kujikaza asionyeshe dalili zozote za kuzinduka. Kwa sababu alijua kosa lolote lile litayagharimu maisha yake kabla hajaonana na Sam. Ndani ya sekunde kadhaa akajikuta hewani kisha akatua katika kitu katika kochi, kwa ule mshtuko akajikuta amefumbua macho, bahati ilikuwa upande wake taa ilikuwa imezimwa katika ile gari ambayo ilionekana kama ya kubebea wagonjwa. Na mara milango ikafungwa na gari likatoweka kuelekea mahali ambapo mama lao hakujua ni wapi. Harufu ya kifo ikaziandama pua zake na waziwazi akatambua kuwa yupo katika dakika za mwisho za uhai wake. Alijaribu kufikiri ni kitu gani atafanya kujiepusha na kikombe hicho lakini akili haikufanya kazi kabisa…. Akaamua kufanya sala zake za mwisho huku akijilaumu kwa kujiingiza katika mchezo asioujua sheria zake!! **** MAJIRA ya saa mbili na dakika kadhaa Sam alikuwa akitembea kinyonge kuelekea katika nyumba ambayo alikuwa akiichukia. Ilikuwa ni nyumba ambayo aliishi kwa furaha sana wakati akiwa na Tina wake lakini ndani ya juma moja tu ilikuwa imegeuka chungu sana. Alifika na kufungua mlango, mara akashtuka kuwa mlango ule haukuwa umefungwa na funguo. Sam akajaribu kukumbuka iwapo wakati anaondoka alifunga mlango, hakulipata jibu, akili yake ilikuwa imechoka haswa na hakujali iwapo ni kweli hakuufunga mlango ama aliufunga kwa kutumia funguo. Akaingia kichwakichwa akiwa ametawaliwa na uchovu. Akajitupa katika kochi sebuleni, akatazama huku na kule kisha akaingia chumbani. Akaondoa nguo zake kisha akaingia bafuni, akaanza kujimwagia maji. Maji yale baridi kabisa yakampa uhai kidogo kiakili. Alipojipaka sabuni akayafumba macho yake, ghafla shingo yake akahisi mlango wa bafuni ukifunguliwa, akataka kufungua macho ilihali ana sabuni usoni sabuni ikapenya machoni, akalazimika kufumba macho. Na hapo ghafla shingo yake ikakabwa kabla hajapiga kelele za aina yoyote ile. Sam alitapatapa huku na kule lakini shingo yake haikuachiwa. “Sam….tulia….” sauti ilimnong’oneza kwa chini sana. Sam hakutulia badala yake alizidisha kutapatapa…. Ule mkono nao ukaendelea kumkamata. “Sam ni mimi…. Tulia…” ile sauti ikanong’ona tena. Sam akaigundua kuwa amewahi kuisikia mahali. Akatulia mara akainamishwa chini. “Nawa!” Sam akatii akanawa uso, sabuni ikamtoka. Na hapo akajikuta yu bafuni, ana kwa ana na mama lao. Sam akapigwa butwaa la mwaka kwa kimbwanga hicho. “Usiongee…” Mama lao akatoa sauti ya chini sana. Sam akaukumbuka umakini alioonywa na mdhamini mtata wa usiku wa manane. “Kwani..” akataka kuzungumza, mama lao akamziba mdomo. Sam akajipa utulivu zaidi! Mama lao akashusha macho yake chini, Sam naye akayashusha! Ama! Alikuwa yu uchi wa mnyama… upesi akalirukia taulo lake na kujifunga. Mama lao akatabasamu!! Kisha akamsogelea Sam na kumnong’oneza. “Maisha yangu yapo hatarini sana, nimewatoroka wauaji, na walikuja hapa kwako pia…” “Sielewi Mama lao…” alijibu kwa kunong’ona Sam. “Wametega vinasa sauti…. Usiruhusu kabisa kuongea sauti ya juu! Wamekuja mara mbili ndani ya chumba chako…” Mama lao akamsimulia Sam mkasa mzima juu ya tukio la hospitali, na namna ambavyo wauaji walijisahau baada ya kupata wanawake na kwenda kufanya nao uzinzi wakiamini mama lao amezimia. Mama lao akaitumia nafasi hiyo kukimbia mahali asipopajua, hadi alipopata pikipiki iliyomfikisha nyumbani kwa Sam. “Sam sijui kama nitadumu sana katika kujificha lakini sikiliza kitu kimoja cha msingi, kuna mtu anaitwa BVB huyu ndiye aliyewaagiza wale wanyakyusa kukukamata wewe, na pia ni huyo BVB aliyemwagiza yule mwendawazimu kuiunda ajali na kumuua baba wa Steven Marashi. Sam, amani na maisha yangu yapo mikononi mwako, mimi nitaenda Mbeya kwetu nitajificha huko lakini ni wewe wa kunifanya niwe huru tena. Tafadhali mtafute huyu BVB mfikishe mbele ya sheria. Simjui hata kwa sura lakini tafadhali kuwa makini kuanzia sasa… una jukumu zito sana nahisi hata Tina watakuwa wanamshikiria wao… halafu nimewasikia wakizungumza juu ya mkanda sijui ni mkanda upi” mama Lao aliongea katika sikio la Sam kwa hisia kali. Kisha akamkumbatia kwa nguvu. Sam akayasikia mapigo ya moyo ya yule mama jinsi yalivyokuwa juu!! Vita imeanza rasmi!! Sam akajisemea kisha akamwachia Mama lao na kupiga ngumi ukutani. Hasira ikachemka katika moyo wake, ule uoga akauweka kando na kuuvaa ujasiri. Mama lao akamtia moyo kuwa ni yeye aliyeushika uhai wa Tina na kubwa zaidi alikuwa mwenye uwezo wa kuifichua siri iliyofichika. Safari tatanishi ikaanzia pale!! ***** ALFAJIRI sana Sam akafanikisha kumfikisha mama lao kituo cha mabasi, akapanda na gari na kuliacha jiji la Dar es salaam. Sam alisubiri hadi alipohakikisha basi limeondoka ndipo na yeye taratibu alianza kujivutavuta ili aweze kurejea maskani yake ya Temeke. Kwa sababu ilikuwa ni asubuhi sana hapakuwa na foleni ambazo huleta kero ya kuishi katika jiji la Dar es salaam, hivyo ndani ya dakika zisizozidi arobaini tayari Sam alikuwa maeneo ya Tandika. Aliposhuka akavutiwa na muuza magazeti ambaye nd’o kwanza alikuwa anakifungua kibanda chake. Sam akazuga kuwa kuna kitu ama mtu anamngojea pale, lakini nia yake ilikuwa kusoma vichwa vya habari vya magazeti ya siku ile. Hatimaye yule bwana akaanza kuyatandaza magazeti katika meza yake. Jicho la Sam likakutana na kichwa cha habari kikubwa kikifuatiwa na vingine vidogovidogo. “Muuaji wa Steven Marashi aua askari wawili, amlevya daktari na kisha kutoroka mikononi mwa polisi” Sam hakuwa na subira tena, upesi akamwomba yule bwana ampatie lile gazeti, akafanya malipo na bila kusubiri akafunua na kuisoma ile habari ambayo iliandikwa na mwandishi ambaye jina lake halikuwekwa wazi. Habari ile ikawa inamzungumzia mama lao…. Kuwa ameua askari wawili na kisha kutoroka mikononi mwa polisi. Sam akashusha pumzi kubwa sana akalikunja lile gazeti, wakati anaondoka akaliona gazeti jingine na kichwa cha habari, “GAIDI LA KIKE LAUA POLISI NA KUTOROKA” Sam akafanya tabasamu la karaha na kisha akatoweka. Akiwa njiani alikumbuka kuwa tayari alikuwa ametangaza vita rasmi tangu alipoambiwa na mama lao juu ya BVB. Japo hakujua hata hilo jina ni la nani lakini aliamini kuwa iwe isiwe atashinda hiyo vita. Wazo la wapi pa kuanzia kumsaka huyo mtishia amani anayeitwa BVB lilikuja baada ya kutambua wazi kuwa kuna watu wenye nguvu serikali ama popote pale watakuwa nyuma ya kifo cha Steven Marashi, na kama wapo nyuma ya jambo hilo basi lazima kuna kitu watakuwa wanafahamu ama wanakihitaji. Mkanda wa ngono! Sam akajaribu kuweka hili kama jibu lake sahihi….. Mkanda huu unahusiana vipi sasa na Tina wangu, na kwanza yupo wapi? Maswali yaliendelea kumiminika katika kichwa chake. Na alipomkumbuka Tina akazikumbuka siku njema za mapenzi yao, akazikumbuka ahadi tele walizopeana za kulindana. Sam akasimama kando ya barabara na kuegemea mti akayafumba macho yake. Akaikumbuka ile siku walipokutana ndani ya daladala, Sam akiwa anaumwa kichwa na bahati mbaya akawa amekosa siti ndani ya gari, mara akahisi mguso katika bega lake, alipogeuka macho yake yakakutana na sura ya Tina. “Kaa hapa kaka yangu!” sauti ya Tina ikamweleza Sam wakati huo akimpisha kiti. Sam hakuamini kilichotokea, kupishwa siti na dada tena wa Dar es salaam? Mara wakajikuta wanashuka kituo kimoja, Tina hakuwa mwenyeji eneo lile hivyo akajikuta akimuuliza Sam. Ikawa zamu ya Sam kutenda wema, akampeleka hadi mahali alipokuwa anahitaji. Safari yao ikaanzia hapo, urafiki hatimaye mapenzi. Walipotangaziana ndoa, yakatokea hayo ambayo sasa yamewatenganisha!!! “Eeh! Mungu wangu mlinde Tina wangu huko alipo…” Sam akafanya dua fupi, kisha akaendelea kutembea huku akiwa amejipanga pa kuanzia. Naam! Ilikuwa kama alivyopanga na ilikuwa hivyo. Sam akiwa anatambua vyema kwa ushahidi wa Mama lao kuwa mle ndani kuna vinasa sauti vimetegwa, aliamua kuanza kucheza na akili ya adui yake. Alipofika akajibwaga kwenye kochi, na baada ya dakika kadhaa akasikika akizungumza kwenye simu. “Masu eeh! Usiuweke usiku, tukutane Sinza mida ya saa mbili nikupatie ule mzigo. Wao si wamemchukua Tina ngoja na mimi nilipue tu kila mmoja aumie kivyake, wajinga wananichukulia poa. Sasa wewe usipoteze muda tukutane Sinza Hotel, chumba namba kumi na nane….. jitahidi kujali muda, nazima simu.” Sam akayamaliza mazungumzo hewa huku akitambua wazi kuwa alikuwa ananaswa sauti na wabaya wake. Simu hii feki ikazua kizaazaa!! ****
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni