SEHEMU YA TISA Nimejifunza kitu chini ya jua kwamba si kila mvumilivu huishia kula mbivu, wapo waliovumilia sana na bado wakaishia kula maumivu. Na si kila subira huvuta heri, subira nyingi huishia kuizidisha shari.... Tena kubwa zaidi jingine wale waliosema mwenda pole hajikwai, hii si kwa wote kuna akina mimi tuliojaribu kwenda polepole lakini matokeo yake hatukuishia kujikwaa tu bali kupoteza kucha na vidole vya miguu. Na hapo nikajifunza kuwa maisha hayana kanuni!!! NA HII NI SEHEMU YA TISA. Tina aliishika ile karatasi na alipoifungua kidogo tu, akaiachia ghafla kisha akasimama wima na baada ya hapo akajishika eneo lake la moyo na mara akalainika na akawa anaelekea kuanguka chini. Nikawahi kumdaka tukaanguka naye.... Tina akapoteza fahamu huku akiwa anatokwa jasho jingi mno.. Hapo sasa nikalazimika kuiweka ripoti kamili kushoto na nikatilia maanani usalama wa Tina mke wangu...... NILIONGEZA mwendokasi wa lile pangaboi na kisha nikamsogeza Tina hadi akawa usawa wa pangaboi lile, nikainamakuhakikisha iwapo kwanmza anapumua vizuri, nilipohakikisha kuiwaanapumua vyema nikaona ni heri kumvutia subira nione nini kitajiri..... Zilipita kama dakika tano akiwa bado ametlia vilevile.... nikaingia bafuni na kuchota maji kidogo ili nije kumwagia nione kama patakuwa na mabadiliko ama la niombe msaada zaidi kutoka katika hoteli ile. Niliporejea na maji nilimkuta Tina akiwa ameketi kitako akiwa anashangaa huku akijibinyabinya kichwa chake. “Nimekuwaje Mjuni?” aliniuliza. Nikamueleza kuwa alipoteza fahamu, lakini nikamsihi awe mtulivu tu... nikamueleza kuwa mimi ni mume wake halali kabisa na asiwe na papara zozote kama nilivyomsihi kuanzia mwanzo. “Tafadhali Mjuni nakuomba uichome moto karatasi hii, nipo tayari kusikia maneno yote lakini si maandishi hayo nakuomba sana, mimi ni mkosefu lakini nisaidie katika hili...” alinisihi sana huku akijaribu kujiweka tena katika sehemu aliyokuwa ameketi awali. Nilimuelewa na kumweleza kuwa sitamsomea maandishi yale na baada ya mazungumzo hayo nitaichoma moto karatasi ile. Akanishukuru, nikamueleza kuwa muda wa chakula umefika maana oda tuliyoweka ilikuwa tayari na ilikuwa ni sisi tu kupiga simu waweze kutuletea. Tina alisema ni kweli anayo njaa lakini hajui kile chakula kitaingilia wapi. Nilizidi kumpa ujasiri na kumueleza kuwa ni vyema ajilazimishe kula kuliko kuacha kabisa kula kwa sababu atajizulia mambo mengine yanayoepukika, nikamkumbusha juu ya vidonda vyake vya tumbo. Akakubaliana na mimi kuwa atajilazimishakula hivyohivyo. Nikanyanyua mkonga wa simu nikabofya kuwaeleza kuwa watuletee chakula. Ndugu msikilizaji kwa Tina nilikubali kuacha kumsomea ujumbe ule katika maandishi yale kwa sababu mwandishi alikuwa ni yeye na hivyo alijua kila kitu alichokuwa amekiandika katika karatasi zile lakini siwezi kukuacha wewe na maswali, ni maandishi yaliyonipondaponda na kuondoka na uvumilivu wangu wa muda mrefu. Maandishi yale yaliyoandikwa na mwanamke ninayempenda kabisa yalisomeka hivi.. Wasalaam Eric, Ni matumaini yangu upo salama kabisa ukiendelea kufurahia maisha na mke wako kipenzi. Mimi pia ni mzima lakini sina furaha Eric wangu. Kama nilivyokueleza siku ile kuwa natamani mimi ningekuwa mke wako halafu mkeo awe mke wa huyu mume wangu.... Eric sijielewi kabisa juu yako, kuna wakati nakurupuka usiku naanza kuwaza eti muda huo wa usiku umemkumbatia huyo mke wako, najikuta napatwa hasira sana na roho yaniuma waziwazi. Eric, japokuwa haunipi nafasi kama mimi ninayokupa katika moyo wangu tambua kuwa sijiwezi kabisa bila wewe. Hakuna mwanaume anayeweza kuchukua nafasi yako. Sio kwamba mume wangu hanipendi, ananipenda sana lakini hisia zangu bado ni kwako tu..... ujue nilidhani kuwa nikiolewa nitakusahau, kumbe nd’o nimezidisha tatizo sasa nateseka zaidi. Kuna kama mara mbili hivi nimewahi kuchanganya jina la mume wangu badala ya kumuita Mjuni nikamuita Eric. Sema hakushtukia... Kiukweli ndani ya hii nyumba nipo kwa sababu natakiwa kuwepo tu.... ule upepowa mahaba unaovuma nikiwa nawe hapa hakuna kabisa na siwezi kujilazimisha.. Huwezi amini Eric, yaani wakati mwingine ili nipate walau hisia za kumkumbatia lazima nifumbe macho nione kama mbele upo wewe hapo ndo Napata unafuu.. halafu hali hii inazidi kuwa mbaya kadri ya siku na siku zinavyozidi kusonga mbele. Najua utajiuliza sana kwa nini nimeamua kukuandikia barua badala ya kukupigia simu, najua nikipiga simu utasikiliza kwa sikio hili na kisha yatatokea kule, lakini maandishi haya naomba la ukijisikia uyasome na utambue kuwa sina cha kujizuia kwako. Na kwa maandishi haya nakuapia Eric ili niwe na furaha lazima nikuzalie mtoto. Nikiwa namuona huyo mtoto nione kama nipo na wewe... Na siku tukikutana nitakueleza kitu kingine kizuri mpenzi wangu ambacho naamini utaniunga mkono tu. Tafadhali nimeiacha barua hii kwa kijana wako wa dukani na wewe naomba ukishanijibu uiache hapo dukani nitaikuta.. Tafadhali usiache kunijibu mpenzi wangu na mume halali wa Tina. Nakupenda!!! Ilimalizika barua hiyo iliyomalizia kuuponda moyo wangu, na tangu siku hiyo nikatambua kuwa ninampenda sana Tina. Kwa sababu badala ya kuwaza nini cha kumfanyia kama adhabu nikawa nawaza ni kitu gani nifanye ili Tina wangu aweze kutulia katika himaya yangu. Lakini baada ya kuwatembelea washauri kadhaa na kuwashirikisha juu ya hali kama hiyo bila kuwaeleza kama inanihusu mimi moja kwa moja na mke wangu walinipa ushauri ambao ulikuwa kama marudio tu, lakini kuna mmoja aliyetoa ushauri mfupi sana. Aliniambia “Mjuni kijana wangu, milele utabaki kuwea Mjuni na huyo Eric atabaki kuwa Eric hauwezi kuwa Eric kamwe!!” Ni kweli msikilizaji, Eric alibaki kuwa Eric ambaye ameuteka nyara moyo wa Tina na mimi Mjuni nilibaki kuwa mume jina tu kwa Tina. Kufikia hapa nikasalimu amri na kuamini kuwa si kila mvumilivu hula mbivu, Mjuni mimi nilikua nimeishia kula maumivu!! Chakula kililetwa nikala pamoja na Tina ambaye kiuwazi alikuwa anajilazimisha tu kula lakini ilibidi iwe hivyo kuliko kubaki na njaa. “Mjuni mume wangu naomba unipe nafasi nizungumze najisikia kifua changu kinaweza kupasuka, adhabu hii imenitosha Mjuni niruhusu niseme lolote mume wangu. Najua haupendi kusikia nikikuita mume wangu lakini tafadhali nakuomba....” Tina alinisihi huku akitokwa machozi, tatizo nililokuwanalo na hata wewe linaweza kukukumba ikiwa tu umewahi kupenda kwa dhati. Chozi la Tina bado lilikuwa linaupondaponda moyo wangu. Kuna watu wanaweza kunitafsiri kama mwanaume mjinga lakini ni heri nisikuongopee lolote katika ripoti hii, elewa kuwa Tina alikuwa chaguo langu. “Tina utazungumza sana nikimaliza mimi, na nitakusikiliza sana....” nilimjibu na kumsihi aendelee kula. “Hapana Mjuni... naomba walau dakika tano tu....” alizidi kunisihi.. “Tina hii ni ripoti kamili naomba uniachie nafasi niikamilishe kwanza zimebaki kurasa chache tu!!” niliusimamia msimamo wangu....... ##Ni ripoti kamili mdau, yenye mambo lukuki ndani yake...... bado muafaka haujapatikana wala ripoti haijamalizika.... Endelea kufuatana nasi!!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni