ESEHEMU YA KUMI NA SABA Nikaendelea kumsihi aongozane nami na hatimaye akakubali, nikachukua ruhusa kwa dada yake na kumuahidi kuwa siku inayofuata nitarejea nikiwa pamoja na Tina. Wakati huo swali kuu lililokuwa linanisumbua ni juu ya Sonia... yupo wapi mtoto yule niliyempenda na swali jingine lilikuwa juu ya sarafina nilitaka kujua ni lini alimzaa mtoto yule na ni nani baba yake!!! Sikuona kama ni jambo la busara sana kumpeleka Tina nyumbani kwangu, kwanza mchana ule sikuwa nimeenda makaburini kumsindikiza Freddy aliyekuwa ametutoka baada ya kujinyonga hivyo kuonekana na mwanamke pale ningeweza kuleta tafsiri nyingi sana mbayambaya machoni kwa wapangaji wenzake, na jambo la pili ambalo nililihofia lilikuwa juu ya kukosa uhuru sana. Kama marehemu Freddy na mkewe walipokuwa wanagombana kila mtu aliweza kusikia vipi kuhusu mimi kuzungumza na Tina. Sikutaka jambo hili liwe matangazo kwa kila mtu... Nikaamua kumchukua Tina hadi katika nyumba ya kulala wageni yenye hadhi ya wastani. Ndani ya kile chumba baada ya Tina kurejea katika hali yake ya kawaida alianza kuzungumza na kunisihi sana nisimuulize maswali na badala yake nimsikilize tu huenda mazungumzo yake yanaweza kutatua maswali yangu. Na kweli Tina alianzia pale palipokuwa pananitatiza... Akanikumbusha mara kadhaa alivyokuwa anaweweseka usiku enzi za raha katika ndo yetu, akanikumbusha pia jina alilokuwa akilitaja mara kwa mara hadi nikafikia hatua ya kumuuliza hilo jina ni la nani... Aliposema hivi nikakumbuka kuwa alikuwa akiota sana jina la Sarafina!! Hapa sasa nikaanza kuupata mwanga huku nikipata pia cha kuongeza katika Ripoti yangu. Kumbe nilimuoa Tina akiwa tayari yu na mtoto mkubwa tu. Na kuhusu huyo mtoto ambaye ni Sarafina alijazwa mimba na mwanaume tapeli wa mapenzi aliyemdanganya kuwa akimzalia atamuoa. Ile kubeba mimba na mambo yakabadilika, mwanaume akawa haeleweki mara leo aseme hivi na kesho anabadilika kama kinyonge. Hadi unafika wakati wa kwenda hospitali kujifungua bado alikuwa hana msimamo, baada ya kujifungua maisha yakawa magumu sana na mwanaume akiwa haonekani mara kwa mara. Tina akawahi sana kumwachisha titi sarafina ili aweze kuingia mtaani kupambana kumtafutia chakula, na hapo ndipo akaanza kumuacha mikononi mwa dada yake ambaye ni mlemavu. Tina alifuta machozi kidogo kisha akaendelea kusema kuwa kutendwa vile na yule mzazi mwenzake haikuwa sababu kubwa sana ya kuwachukia wanaume na hata hapo anapozungumza hajawahi kuwa na chuki na wanaume wote kwa sababu anaamini wazi kuwa wapo wanaume wanao upendo wa dhati kabisa. Maisha yalivyozidi kumpiga ndipo kama bahati akakutana na mwanaume wake wa kwanza kabisa aliyemtoa usichana wake. Alikuwa amechakaa vibaya sanaalipokutana na mwanaume huyu... na hapa akajikuta akiingia penzini angali mwanaye alikuwa mdogo sana. Tina anakiri wazi kuwa alifahamu kuwa anafanya makosa lakini tatizo ni kwamba alikuwa muhitaji zaidi. Hapo nikamuingilia kati na kumuuliza wazazi wake walilichukuliaje jambo hili na kwa nini hakuwaomba msaada. Tina akatabasamu na kisha akaanza kujitukana yeye kisha akawatukana na wasichana wote wanaofanana na yeye katika jambo hilo la kudanganyika. Akaelezea kuwa aliibeba ile mimba nje ya matakwa ya wazazi wake ambao walimuapia kuwa iwapo atabeba mimba nje ya ndoa basi watampa laana, hivyo alipoibeba mimba hii alijidanganya kuwa wataoana upesi na yule mwanaume hivyo hata wazazi hawatajua kama alikuwa na mimba kabla ya ndoa. Na hata wakijua atakuwa ameolewa tayari haitakuwa na uzito... Baada ya bwana yulekuikataa mimba ile basi ikabidi hata wazazi wasijue. Dada yake mlemavu wa miguu akamsaidia kuitunza siri.... Akashusha pumzi zake kishaakaendelea...... “Huyo mwanaume kweli alinifaa sana katika kipindi kile kigumu, na kwa sababu alikuwa mwanaume wangu wa kwanza sikuwa na mashaka naye na ninakiri kweli nilimpenda na nilitamani sana anioe.... hata yeye sikumueleza iwapo nibna mtoto tayari,nilikuwa najisikia vibaya sana kumkana Sarafina wangu kwa wanaume lakini nililazimika kufanya vile kwa sababu baadhi ya wanaume wakisikia una mtoto hata mpango waliopanga juu yako unaisha...” akasita Tina akanitazama na kuniita jina langu nikaitika. “Bila shaka umemjua tayari baba yake Sarafina... nikikueleza kuwa mimi ni mchafu sana kwa maneno matupu hauwezi kunielewa lakini jaribu kufikiri mtoto wa kwanza haya huyo sawa utasema nilimpata kabla sijaolewa na wewe haya na huyu wa pili naye nikampata kwa ujinga ujinga tu.....” alisonya kisha akavuta pumzi na kuzishusha kwa nguvu. Tina aliendelea kusimulia hadi akafikia kwenye lile tukio ambalo nilikuwa nalihitaji sana, nilitaka kufahamu baada ya kutoroka nyumbani akiwa pamoja na Sonia ni wapi alielekea na ni wapi yupo Sonia. “Niliyopitia ni mengi sana Mjuni nakusihi usiklize tu kwa sababu hata nisipoyasema ndo tayari yametokea na hayawezi kubadilishwa!!” alitoa kauli ile na kunifanya nibaki njia panda nikijiuliza ni kitu gani kilitokea huko nyuma. Wakati najiuliza haya nilikuwa pia najiuliza nitahimili vipi kupokea taarifa eti kuna namnanamna zilijitokeza Sonia akaaga dunia. Nilikuwa nampenda sana mtoto yule. “Sonia yupo wapi Tina?” uvumilivu ulinishinda nikajikuta nauliza.... Sonia badala ya kujibu alinitazama sana machoni moja kwa moja, kisha akainama na kuinuka tena...... “Mjuni Kalisti...” akaniita jina langu kikamilifu..... Nikajikakamua na kuitika.... “Wewe ni mwanaume wa kipekee...” alisema huku akilazimisha kutabasamu. “Tina tafadhali nieleze kuhusuSonia kwanza tafadhali nieleze.....” nilimsihi na hapo wasiwasi ukizidi kuchukua nafasi katika moyo wangu..... “Nitaeleza kila kitu bila kuacha neno lolote Mjuni ninachoomba ni usikivu wako tu......” Kauli hizi za Tina ziliendelea kunitafuta vibaya mno......... **ehee! Ni kitu gani kilimtokea Tina na Sonia kuanzia alipotoroka hadi alipo hivi sasa? Usiikose sehemu inayofuata... itakupa baadhi ya majibu...... MAISHA ni darasa lenye somo jipya kila siku. Wewe ni mwanafunzi katika darasa hili, ombea sana kila kukicha kuwa usije kuwa mfano kwa wanafunzi wenzako kujifunzia..... na inapotokea moja kati yenu anakuwa mfano jitahidi sana kuufanyia kazi mfano huo. Kuna mengi sana huwatokea wanadamu wenzetu ambayo ni sawasawa na darasa la bure kabisa kwetu lakini wanadamu hufunga macho yao ili wasione na masikio yao ili wasisikie kisha kesho yake wanafanya kosa alilofanya fulani na kuambulia majuto....
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni