Jumamosi, 26 Desemba 2015

HILA NO.6

SEHEMU YA SABA TATIZO moja kubwa ambalo huwagharimu wanawake pindi wawapo na ghadhabu ni kuamini kuwa kila kitu wanachofanya wanakuwa sahihi. Na wakiwa katika katika hali hii mara nyingi huwa wakubwa wa siri na wavivu wa kushirikisha mtu juu ya mambo yao. Labda mwanamke mwenzake tena walioshibana. Ni hiki mkilimsibu mama Tina, akiwa kama mwanamke mwingine tena mwenye mapenzi ya dhati kwa mtoto wake aliyekuwa hajulikani alipo baada ya kukamatwa na polisi. Alipokea simu ileile ambayo Sam alidai kuwa yawezekana ni Tina atakuwanayo, ajabu hakuzungumza Tina walizungumza wanaume na kumwelekeza mama Tina mahali ambapo Tina yupo, aende na pesa kwa ajili ya kumchukua. Pesa yenyewe ya kukodi teksi tu! Ajabu. Bila kuishirikisha akili yake vyema, mama Tina akamshirikisha mdogo wake wa kuishi naye, wakaondoka huku ndani ya teksi wakimnanga Sam kadri walivyoweza, wakafikia hatua ya kumwita mwanaume suruali asiyemjali mchumba wake. Walipokelewa eneo husika maeneo ya Koko, majira ya usiku.. bado watu walikuwepo katika hoteli wakipata vinywaji na chakula. Mama Tina akaombwa aingie peke yake ndani na yule mwanamke mwingine akabaki kumsubiri nje!! Akiahidiwa kuwa atarejea na Tina baada ya dakika chache, mama Tina akaingia kichwakichwa!! Muda mchache ukawa muda mwingi, saa zima likazaa saa la pili na la tatu. Baridi likamzidia yule mwanamke na kujikuta akizidiwa na uvumilivu, akaamua kupiga simu…. Simu ya mama Tina ilikuwa inaita tu bila kupokelewa. Aliendelea kupiga bila mafanikio. Hatimaye akaamua kuingia ndani ya hoteli kumtafuta.  Bado hakufanikiwa kumuona, hadi pale aliposikia kelele za kuhamasishana juu ya jambo Fulani la hatari. Akavutika kwenda kupoteza muda katika tukio hilo wakati huo akimsubiri mama Tina. Kama alidhani anaenda kupoteza muda haikuwa hivyo….. Alikuwa anaenda kushuhudia mwili wa mama Tina ukiwa hauna uhai wowote ule. Mwili ulikuwa sehemu ileile ambayo Sam aliagizwa kwenda kuchukua kadi ya simu na mtu ambaye aliamini kuwa alikuwa ni teja. Utata ukaendelea!!!      UKUNGU uliyatawala macho yake na kumfanya aone maumbo kadhaa yakiambaa katika ukungu ule katika namna ya kukera, alijaribu kuyapikicha macho yake na hapo akasikia miungurumo ya ajabu ajabu. Ule ukungu akajiaminisha kuwa ni mawingu na ile miungurumo basi akaona kuna kila dalili ya mvua. Mvua inataka kunyesha halafu nimekaa nje? Alijiuliza katika nafsi yake, kisha akaulazimisha mwili wake uweze kunyayuka aweze kuondoka eneo lile kujiepusha na mvua kubwa iliyokuwa inataka kumwagika. “Pumzika Sam, subiri usisimame!” sauti zilizokuwa za miungurumo zikazungumza na akasikia vyema. “Mungu wangu? Mawingu yameniita jina langu….au malaika?” alijiuliza lakini safari hii kwa sauti ya kukwaruza kidogo. Wakati huohuo akiendelea kunyanyuka…. Mara akaguswa begani, akashtushwa na kitendo kile akajipapasa begani mara akakutana na kiganja cha mkono. Sam akapagawa na kuanza kupiga kelele!! Ni katika patashika hiyo alijikuta akiona vyema mbele na wala hapakuwa na mawingu bali umati wa watu ulikuwa umemzunguka. Sura kadhaa alikuwa akizitambua lakini kuna sura moja aliitambua zaidi. “Sam mwanangu ulipoteza fahamu hukoo mjini, kuna wasamaria wema wamekuleta hapa….. pole sana” ilikuwa sauti ya Mama Lao!! “Nini? Nilianguka, hapana hakuna kitu kama hicho mama…hakuna kabisa nasema sijaanguka mimi…” alipinga Sam huku akijisikia fadhaa kuwa amekaa chini huku amezingirwa na umati. “Dah! Maskini wee! Sijui hata kama ataelewa huyu….” Kijana mwingine alilalamika pembeni huku akimwonea huruma Sam. Sam aliamua kuituliza akili yake bila kusema lolote, akayafumba macho yake na kujilazimisha kukumbuka mara ya mwisho alikuwa wapi kabla hajarejeshwa nyumbani kwake bila kujitambua. Akili ikafanya kazi yake ipasavyo, akakumbuka kila kitu. “Nooo! Noooo! Sikuzimia, walinichoma na kitu kama pini hivi eheee! Nimekumbuka ni kitu kama sindano, hapa begani, mh! Hivi ilikuwa begani ama shingoni….. ni..be….aah! ilikuwa shingoni….. wajinga sana wale jamaa wameniteka wale, hata siwajui maskini nimewakosea nini mimi eeh! Nimewakosea nini sasa….wamemchukua Tina wangu….na mama na mama wame…. Whaaaat! Mama amekufa?” Sam alihangaika huku na kule akitoa maelezo ambayo yaliwathibitishia watu kiuhakika kabisa kuwa mtu aliyepoteza fahamu, akirejea katika fikra zake za awali huwa anaweweseka. Wakadhani kuwa hata Sam alikuwa katika kuweweseka!! “Anko Sam, ingia ndani upumzike, haupo sawa?” “Nini? Sipo sawa, sipo sawa natambua kuwa huyu ni mama lao, mama anayelisha mtaa mzima kwa tusiokuwa na familia, huyu hapa mama Khadija na Khadija wake anasoma kidato cha kwanza hapo Makongo, huyu naye sio baba Hamadi, na huyo Hamadi wake si ndiyo yule anayetaka kuwa mtangazaji…. Mnataka nitaje mtaa mzima nd’o mfahamu kuwa nipo katika timamu zangu…..sijachanganyikiwa narudia kusema kuwa nilitekwa baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali katika bega langu la kuume, na wakati yanatokea haya nilikuwa nimepokea taarifa kuwa mama mkwe wangu amepoteza uhai. Naitwa Samwel Mbaule na nipo katika akili yangu….naomba niaminike!!” Sam aling’aka kwa ghadhabu na kwa kitendo chake cha kutambua watu waliokuwa mbele yake kiliwafanya wote waanze kuamini kile alichokuwa akikisema. “Simu yako hii hapa… hao wasamaria wema walisema tukupatie ukizinduka…” jirani mmoja alizungumza huku akimkabidhi Sam ile simu. Sam alicheka kwa kujilazimisha, cheko la karaha…. “Eti wasamaria wema, mabaradhuli wakubwa wale wananionea bure tu…wananionea tu…” alilalama huku akiichukua ile simu, akasimama na kuwashukuru wote waliompokea akiwa amepoteza fahamu, kisha akafungua mlango wake na kuingia ndani ya chumba asichokuwa na imani nacho. “Mmeweka tena madawa ya kulevya nyie paka shume waonevu wa kukwapua samaki mdogo wa mama mjane maskini…wekeni tena nitavuta na kuzimia tena. Naona mna lengo la kunisababishia niwe na kifafa…endeleeni lakini Mungu aliye hai ananipigania…. Na wakati unakuja hamtaweza kunizimisha tena bastard!!” alikaripia Sam huku akiamini kuwa ujumbe ulikuwa unafika. ***** Baada ya kujimwagia maji na kuuweka mwili wake katika uchangamfu tena, Sam aliitwaa simu aliyokuwanayo, lengo lake likiwa moja tu. Wazo ambalo alilipata akiwa bafuni, kuwa ukitambua kundi fulani linakushinda basi ungana nao ili wote muwe washindi! Sam alijiuliza maswali mengi na kuamini kuwa lile kundi linalomwandama lilikuwa likishabihiana na kifo cha Steve Marashi. Hivyo wakimtambua muuaji wa Steve iwe isiwe wataachana naye na hata Tina atarejeshwa mikononi mwake. “Nyie majamaa…..” alianza kuzungumza kwa sauti akiamini kuwa mle ndani kuna vinasa sauti na lazima watamsikia tu…. “Nyie majamaa mnadhani namjua muuaji ama mimi naweza kumuua rafiki yangu Steve….mnanikosea sana heshima kwa hilo….mnanitesea bure Tina wangu na mama mkwe wangu mmemuua amakweli mmeamua kunionea….sasa sikilizeni humu katika simu kuna mtu alijitambulisha kama muuaji wa Steve na hadi sasa sijajua ni nani…jina lake lilihifadhiwa kwa herufi tatu ‘SLM’….Sikieni sasa hii ni simu ya mchumba wangu….mimi nampigia huyu SLM ili mmsikie wenyewe ni kwanini anasema kuwa anasingiziwa kumuua Steve. Msikie kama atanitaja mimi sasa….” Sam alisita. Akaichukua simu na kuanza kupekua jina lililohifadhiwa kwa herufi zile ambazo zilikuwa zimenasa katika kichwa chake kutokana na zile meseji kadhaa alizotumiwa na kuzifuta. Sam hakuamini macho yake alipotafuta namba zile pasi na kufanikiwa…alitafuta kwa jitihada zote lakini bado hakufanikiwa! Jina SLM halikuwepo tena katika simu ile! Sam akayahisi macho yake yakichonyota, akaamini kuwa wale watekaji walikuwa wanazidi kumwona muongo. Hatimaye akaanza kulia kama mtoto mdogo!! “Mmelifuta jina…ni nyie mmelifuta washenzi wakubwa nyie.. mnamjua aliyemuua rafiki yangu…mnamjua na bado mnaniandama…ok! Njooni mniue na mimi..mumuue na Tina..mkamuue kila mtu, wanadhambi wakubwa nyie…” Sam akaporomosha maneno makali makali, kisha akajirusha kitandani kwake. Hakika alikuwa amepagawa! Alitamani kulala lakini usingizi ukagoma….  Ili kujinusuru katika utata huu, Sam akaamua kutafuta chcohote cha kuweza kumfariji na kumsahaulisha. Alikuwa amepanga kuwa jioni aelekee katika msiba wa mama mkwe wake huku akijiahidi pia kwenda polisi kupata taarifa juu ya kifo hicho. Katika kupepesa macho akakutana na kikaratasi cha kuhifadhia santuri ‘CD’… akakitazama kile kikaratasi na hapo akakumbuka kuwa aliyempatia alikuwa ni marehemu Steven Marashi. Alimpatia santuri ile siku moja walipokutana akamweleza kuwa ilikuwa ni filamu yake mpya ambayo anatarajia kuitoa. Sam akawasha runinga yake, akatia ile santuri ili aweze kujiliwaza na kumuenzi rafiki yake kipenzi. Kama kawaida alitegemea kukutana na matangazo kadhaa ya filamu kabla ya filamu yenyewe kuanza. Lakini ajabu haya yote yalikuja lakini sio katika mfumo na nembo iliyozoeleka kuwa inasambaza kazi zake Marashi. “Ah! Alihamia kampuni mpya ama…. Mbona hata siijui hii… Black Entartainment… ya wapi hii….” Alijiuliza Sam…. Mara akatokea Lili. “Wacha wee alicheza na Lili, si alikuwa anazuga kuwa hataki kucheza naye filamu yoyote….nd’o maana akanipa kama Sapraizi eeh” akakaa vyema aweze kuitazama vyema ile filamu. Mara ghafla mshangao ukahamia katika mshtuko, Lili alikuwa amevaa katika namna ambayo ni sawasawa na kuwa uchi tu. “Nd’o maana haya ma Bongo muvi yao siyapendi….sasa nd’o kuvaa gani huku si uchi kabisa yupo?” alihamanika Sam… Lakini hamaniko hilo halikudumu sana , zaidi likahamia katika kustaajabu. Lili akayageuza makalio yake kuelekea katika kamera na mara likatokea jambo ambalo lilimfanya sam ajikute anaziba macho yake. Lili alibetua kitufe fulani katika nguo yake ambayo ilikuwa ni sawa tu na mkaa uchi. Lakini baada ya kubetua akawa uchi wa mnyama. “Mama yangu weee!!....huyu si Lili huyu jamani….” Alijiuliza mwenyewe kisha kaangalia kushoto na kulia kama kuna mtu ambaye anaweza kumjibu. Hakuwepo!! Na alipoyarudisha macho yake kwenye runinga akamwona mwanaume akiwa uchi. Hapa ukawa mwisho wa labda labda sasa ukawa ni uhakika. Ile ilikuwa ni video ya ngono, muigizaji akiwa ni Lili wa Tanzania, lakini ile sura ya mwanaume haikuwa maarufu na Sam hakumtambua mara moja. “Ni kitu gani hiki ulinipa Steve Marashi…ulimaanisha nini wewe eeh! Steve ulimaanisha nini, hebu kama haujafa kweli njoo uniambie nini ilikuwa maana yako we rafiki!! Njoo Steve…. Au…aaah! Hapana…” Sam alighafirika kweli. Lakini hapohapo akasikia sauti ikiwaamuru Lili na mwenzake kulianza tendo. “Stand by……..ACTION!!!” iliamrisha sauti ile ya kiume. Kijasho kikaanza kumtoka Sam, masikio yake yalikuwa yameiskia sauti ya STEVEM MARASHI ikitoa amri!! Amri ya Lili kuanza kucheza ile filamu ya ngono. Kilichotokea baada ya hapo… Sam alilazimika kuzima runinga yake mara moja!! Alikuwa amepagawa. Nafsi moja ilimtuma kuufikisha mkanda ule polisi ikiwa ni kigezo namba moja cha wao kuanza upelelezi juu ya kifo cha Steve Marashi, lakini nafsi nyingine ikamsihi kuwa mkanda ule awapatie wale watu wabaya wanaomsumbua kila kukicha huku wakimmiliki Tina wake. Hakujua ni wapi angewapata lakini aliamini kuwa wapo karibu naye na wanamsikia!! Kabla hajapitisha maamuzi yoyote yale, mlango wa sebuleni uligongwa…. Upesi akakimbilia deki na kuitoa mahali ilipokuwa, akaificha chini ya uvungu wa kitanda. Alipoufungua mlango alikutana ana kwa ana na mwanamke wa kazi, mcheshi na anayemzoea mtu kwa sekunde kadhaa tu. Alikuwa ni MAMA LAO!! Hakuwa na tabasamu usoni na ni kama kuna mambo mazito alikuwa ameyabeba na ilikuwa ni lazima ayatue. “Karibu…” Sam alimkaribisha huku akiachia nafasi mlangoni mama yule akapenya. Sam akaufunga mlango na kisha kumkaribisha mama lao katika mojawapo ya sofa pale sebuleni. Baada ya salamu na pole za hapa na pale. Mama lao akamueleza Sam jambo lililobadili kila kitu katika kichwa chake huku likimwacha katika namna ya kukosa maamuzi kabisa!! Huo ukawa mwendelezo wa utata!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni