Jumatano, 30 Desemba 2015

HILA NO.10

SEHEMU YA KUMI  Taarifa za vifo vya mapacha wawili tegemeo kabisa katika ngome ya mzee Matata ilipokelewa katika namna ngeni kabisa na mzee yule, alikuwa amepagawa na hakutarajia hata kidogo jambo kama lile lingeweza kutokea. Hakuamini hata kidogo kama Sam angeweza kukabilia na vijana wale machachari na kisha yeye akaibuka bingwa. Tena sio bingwa wa kawaida tu, bingwa aliyeua. Upesi akachukua simu yake na kumpigia mzee Robert, mrakibu mkuu wa polisi. Simu ilipokelewa kwa utulivu! Harakaraka na kwa papara kubwa Matata alianza kumuhoji Robert juu ya tukio lililojitokeza Sinza hotelini. “Kwani kuna tatizo gani mzee Matata ya nini kuuliza kila kitu kinachohusu usalama wa raia na hasahasa siri za jeshi la polisi. Samahani lakini kwa namna moja ama nyingine nashindwa kukuelewa mkuu….” Bila kujibu chochote mzee Matata akakata simu. Robert akabaki kutetemeka asijue mzee yule alichukulia vipi maelezo yale aliyompa. Lakini alifanya vile kwa sababu alilazimika kufanya, kwanza alikuwa amevurugwa sana. Matukio yalikuwa yanapangana, kabla hili halijaisha anasikia jingine likipanda juu yake.  Ilikuwa lazima achanganyikiwe na matukio yale yaliyozungukwa na utata. Akiwa anaanza kusahau juu ya simu aliyozungumza na mzee Matata, mara simu yake ya mkononi ikaita. Alikuwa ni IGP…..     Robert akaomba dua zote kabla ya kuipokea simu ile kwa sababu alimjua vilivyo mkuu wake wa kazi. “Robby, hivi ungemjibu mzee Matata vizuri ni kitu gani kingekupungukia labda…… Robby, mzee Matata akiongea na mkuu wan chi ujue utaingia matatani. Nisikilize Robby, wewe na mimi tunafahamu ni pesa kiasi gani mzee Matata ametoa ili kufadhili kampeni za chama. Unajua ni jinsi gani mzee Matata na raisi ni marafiki, chunga sana mdomo wako Robby, chunga sana inaweza kukugharimu, nimekusihi haya kwa sababu wewe ni mzazi na una familia kubwa… sitaki familia yako iteseke. Nadhani unanielewa, sasa mpigie simu mzee Matata tena ni muda huu na umwombe msamaha….” Alihitimisha IGP. “What? Ni nini hiki IGP… Msamaha kwa kuficha siri za jeshi letu mkuu…” “Nimesema mwombe msamaha. Nimemaliza…” akakata simu IGP. Robert Massawe akabaki kuitazama simu ile kana kwamba ina lolote la kumshauri ama inaweza kushiriki naye katika mshangao mkubwa aliokuwanao… lakini haikuwa hivyo. Simu nayo iliendelea kumtazama. “Si bure…..” Robert alijisemea huku akiichukua simu yake na kubofya jina la mzee Matata. Funika kombe mwanaharamu apite!! Alijisemea huku akiungoja upande wa pili uweze kupokea simu. Simu iliendelea kuita bila kupokelewa!! ***** WAKATI simu ya mzee Matata ikiita, mzee huyu alikuwa ameenda mahali kujipooza hasira zake. Kitendo cha kukatiwa simu ya Robert alichukulia kama dharau kubwa sana kwake na tena ikiwa imefanywa na mtoto mdogo asiyekuwa na uwezo wa kutoa kauli yoyote mbele yake. Mzee Matata alikifikia chumba alichokusudia akakifungua na kukabilia na sura iliyokuwa ikisihi huruma. Sura ya kike iliyopauka haswa na kuchubuka kutokana na kipigo. Macho yake makubwa yalikuwa yamedumbukia ndani na midomo yake ilikuwa mikavu. “Bitch! Huyo hawara wako anashirikia na watu gani?” Matata alitupa swali. Yule binti aliyezidi kusihi huruma kwa yale macho yake tu alijitahidi aseme lolote lakini akashindwa. Akabaki kulishika koo lake na hapo sauti ya kukoroma ikamtoka. “Nina kiuuu…” Hakika alikuwa ana kiu, kiu kikalikausha koo na kuondoka na ile sauti yake nzuri. Sauti iliyompagawisha Sam na kujikuta akiamua kutangaza ndoa kabisa. Alikuwa ni Christina Elisha Prosper ama alivyozoeleka kwa wengi kama Tina! Ile hali ya Tina kulalamika kiu badala ya kujibu swali aliloulizwa ilimghafirisha tena mzee Matata, akahisi anazidi kudharauliwa na watu wasiostahili hata kupita njia anayokanyaga yeye. Mzee Matata akaondoka, sura yake ikiwa nyekundu akaingia bafuni na kutoka na ndoo iliyojaa maji. Akaifikisha katika chumba alichokuwa amehifadhiwa Tina. “Inama unywe maji kisha unijibu…” mzee Matata akamweleza Tina kwa sauti iliyojaa upole. Tina akajisogeza kwenye ndoo na kuinama kama mbuzi. Akaanza kunywa maji. Mzee Matata akamvamia pale pale kwenye ndoo na kukishika kisogo chake na kumzamisha kichwa kizima katika ile ndoo. Tina alitapatapa akirusha miguu huku na kule, alivuta maji kwa pua na midomo. Akazikosa pumzi zake.  Baada ya dakika mbili mzee Matata akamwachia. Tina akabaki kutapika huku na kule, akizisaka pumzi kwa jitihada kubwa, katika kuruka huku na kule mara akamtapikia mzee Matata katika mguu wake. Yule mzee asiyekuwa na huruma akamnasa kibao kisha akamfyatua teke kali tumboni huku akimsindikiza na matusi. Tina akatua katika kingo ya ukuta, uso ukabaki kutambaa sakafuni na maneno yasiyoelewekaeleweka yakimtoka. “Sam anashirikiana na nani katika kikundi chake cha kijasusi??” alihoji mzee Matata. “Sijui lolote…. Najua ni mwandishi tu…..” alilalamika Tina. Mzee Matata akataka kumrushia adhabu nyingine ya teke lakini safari hii akaisikia simu yake ikiita. Akaufunga mlango na kutoweka. Akaipokea simu na kuupokea msamaha kutoka kwa Robert. Mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi!! Ile hali ya kuombwa msamaha ikampunguzia ghadhabu kidogo na kujiona mtukufu sana mbele ya watu wenye madaraka. “Haya kijana…. Ni nani wale waliopambana na kuuana katika hoteli ya Sinza…” akamuhoji Robert kifedhuli. “Wawili hawajajulikana majina lakini mmoja ni kijana wetu…” alijibu Robert huku akiuma meno yake kwa hasira. “Na kijana wenu naye amekufa?” aliuliza. “Haijathibitishwa bado lakini yupo mahututi hospitali ya jeshi Lugalo…” “Ok! Vizuri ntakupigia baadaye nikihitaji kujua juu ya hali yake. Poleni na muwe na siku njema…” akaaga na kukata simu. “Fuck!” alifoka Robert huku akiibamiza meza iliyokuwa pale ofisini, akaituliza akili yake na kujiuliza juu ya yule mzee ambaye anatambulika nchini kwa biashara zake kubwa anazomiliki. Sasa kulikoni mambo hayo ya jeshi awe anayafuatilia kwa ukaribu kiasi hicho. Lazima kuna kitu hapa!! Alijishauri, na kisha akajiapiza kutothubutu kufuatilia nyendo za mzee Matata. Hakutaka kuyapata matata!! Akakumbuka maneno kadhaa ya IGP alipokumbushwa juu ya familia yake, hapo uoga ukamwingia. Lakini hakuwa amejitoa katika vita na mzee Matata kama alivyodhania!!  Nd’o kwanza alikuwa anaikaribia. *** SIMU yake iliyokuwa katika mfumo wa mtetemo iliunguruma mara tatu kabla mkewe hajamgutusha kutoka usingizini. Robert Masawe alijinyoosha kidogo kabla ya kutazama kwenye kioo na kukutana na namba mpya. Hilo halikumshtua ilikuwa kawaida kupewa taarifa kadha wa kadha kutoka kwa wakuu wake ama wadogo zake kikazi kwa kutumia namba mpya. “Jambo afande, CW00JT Lugalo hospitali..” alijitambulisha kwa namba yake na Robert akatambua kuwa kuna ujumbe anatakiwa kupokea. “Endelea afande.” “Kuna vijana watatu wanahitaji kumwona Inspekta Yakubu Gama….” “Vijana? Vijana kutoka wapi?” “Madaktari wameagizwa na mzee Matata!” “Whaat? Madaktari, madaktari kivipi?” “Sina nijualo zaidi ya kukupa hii taarifa afande..” “Usiwaruhusu kwanza!” akaagiza na kukata simu. Akatulia kitandani kwa sekunde kadhaa, mkewe naye akaketi kitako kuungana na mumewe. Hakutaka kumuuliza lolote, zaidi alibaki kumminyaminya begani kama namna ya kumfariji. Robert Masawe, mrakibu msaidizi wa polisi aliitwaa tena simu yake wakati anataka kupiga mara ikaingia simu kutoka kwa mzee Matata. Robert akaruka sentimita chache kutoka katika kitanda, ni kama alikuwa ameona mdudu wa hatari. Hakuipokea simu ile akaiacha iite hadi pale ilipokatika. Na hapo Robert akampigia IGP. “Jambo afande!” akasalimia. IGP hakujibu akaendelea kumsikiliza. “Mkuu, Mzee Matata ameagiza madaktari kwa ajili ya Inspekta Yakubu Gama! Unayo taarifa hiyo?” “Unawezaje kupata taarifa nzito kama hiyo kabla mimi sijaipata?” IGP akajibu katika mfumo wa swali kwa swali. Jibu ambalo lilimkera Robert lakini hakuwa na la kufanya. “Lakini mkuu ulipaswa kunieleza kwa sababu vijana walio katika lindo wanatoa taarifa kwangu kama ulivyoagiza mkuu…”  “Kwa hiyo unamaanisha waanze kuripoti kwangu moja kwa moja?” “Hapana afande!!” “Waruhusu waingie nimezungumza naye, ametusaidia madaktari kutoka India wanusuru uhai wa Gama…. Wakati mwingine tabia yako ya kupenda kuuliza kila kitu siku ya siku utasababisha tukose misaada….” Akamaliza na kukata simu. Super retendant Robert Masawe akapagawa!  Na hapo mkewe akaamua kuhoji kulikoni, Robert Masawe alijaribu kumkwepa mkewe lakini mwanamke yule hakukubali kabisa. Akakazia hadi Robert akasalimu amri akaketi kitako na kuanzia kumsimulia mkewe juu ya mkasa mzima unaoendelea. Mkewe alikuwa makini sana kumsikiliza na baada ya maelezo yale, mkewe akatokwa na kauli ambayo bwana Robert hakuitegemea. “Ukilala usingizi basi Gama atalala usingizi wa milele leo, pindi utakapoamka utakutana na lile neno kwamba jitihada za madaktari zilishindikana…. Hakuna madaktari hapo mume wangu, hao ni watu wabaya na hapo wanataka kumzimisha Gama ili asiseme ambacho amekigundua huko alipotoka…” “Heh! Mke wangu umeyajuaje haya yote?” “Nasoma sana riwaya mume wangu hasahasa za kipelelezi, wewe hupendi riwaya lakini zile za wakongwe zina mambo mengi ya kujifunza, mfano Mhanga wa ikulu ya Beka Mfaume, Mkimbizi ya Hussein Tuwa na Msako wa Hayawani ya Eddie Ganzel…. Naona wanayoyaandika nd’o kisa kama hiki, ukitaka kuamini we lala halafu asubuhi tutasimuliana…. Lakini uhai hautakuwepo tena. Gama atakuwa mfu!!” Maneno ya mkewe yakamsisimua Robert licha ya kutokuwa na undugu wowote na Gama lakini alitambua kuwa nchi ilikuwa ikimuhitaji sana kijana shupavu kama yeye ili amani iendelee kuwepo huku waovu wakifikishwa mbele ya sheria. Uzalendo ukajikita katika moyo wake, ujasiri ukajiunga naye upya. Akaona si sawa kumpoteza Gama katika namna nyepesi hivyo. Alitambua kuwa vijana waliokuwa wameweka ulinzi kwa Gama wasingeweza kuwaruhusu wale madaktari kuingia katika chumba cha mgonjwa bila idhini yake yeye.  Pale pale akachukua simu ya mkewe akabofya namba za mmojawapo wa askari katika lindo la hospitali ya Lugalo ambayo alikuwa amehifadhiwa Gama. Akamwambia asogee kando kabisa waweze kuzungumza. “Naomba uende katika chumba alicholazwa Gama, kamtazame hali yake na ukiwa humo chumbani nipigie simu.” Akamaliza na kukata!! Yule kijana kama alivyoamrishwa akawapita wale madaktari ambao walikuwa wakingoja ruhusa, akaingia katika chumba alichokuwa amelazwa Gama. “Hali yake bado si salama amepoteza fahamu bado..” “Afande! Sina imani hata kidogo na hao madaktari, ni mimi nakueleza wewe tu na ujue wewe tu kwa sababu kanuni za jeshi kumtilia mtu mashaka ni nguzo kuu katika upelelezi. Hivyo nakuomba ufanye kitu kimoja…… ni cha hatari lakini nd’o inaweza kuwa salama yetu…. Wasiliana na daktari mmoja anaitwa Haji. Ni rafiki yangu sana kisha nipe nizungumze naye. Mengineyo nitakujuza. “Sawa afande!” alijibu yule kijana kisha akatoweka. Akafanya kama alivyoamriwa! ****  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni