Jumanne, 15 Desemba 2015

RIPOTI KAMILI SEHEMU YA 21

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA MAPENZI upofu wahenga walisema..... Unaweza penda usipopendwa , ama unaweza kuangukia sehemu ambayo unahisi kwako ni sahihi lakini mwishowe inakuwa kinyume na hapo....... NA Hii ni sehemu ya ishirini na moja. Washauri wa kisaikolojia wanayo nafasi kubwa katika maisha yetu. Watu wengi hujikuta wakifanya maamuzi mabovu kwa sababu ya kuathirika kisaikolojia na kuikosa tiba walau ya kiushauri tu. Hata kwa Tina ingeweza kuwa hivi iwapo tusingekutana lakini ya Mungu mengi... Tina alipata washauri wazuri waliomjengea kujiamini na kisha kumpa tumaini jipya la kuishi!! Tina aliendelea na biashara zake huku mimi peke yangu nikiwa na utambuzi kuwa yu muathirika wa virusi vya Ukimwi!! Alichoniomba sana ni kwamba nisimvujishie sirio yake kwa watu wengine.... Wakati huo hata mapenzi kwa Sarafina yule mtoto wake aliyekuwa amebakia yalikuwa yamerejea kwa hali ya juu... Kiafya Tina alibadilika na taratibu ule mvuto wake wa zama zile ukarejea. Hakuwa akifanania na changudoa ama aina yoyote ya msichana ambaye ananunulika kwa bei nyepesi...  Na kama ilivyo kawaida ya wanaume bila kujua mwili wa mwanamke umependezeshwa na nani huishia kuziruhusu tamaa zao ziwatawale na kisha kurusha ndoano. Wengine waliopewa jibu la hapana walijiondokea zao, lakini tatizo lilikuja kwa kijana mtanashati aliyeitwa Abduli. Huyu alienda kwa gia ya kumuoa Tina kabisa...... Tina akajitetea kuwa dini ni kikwazo yule bwana akatangaza ndoa ya bomani, lakini Tina akazidi kuweka ngumu.  Huyu hakwenda kama wenzake wa awali walivyojaribu kumshawishi Tina huyu alitumia njia ndefu sana...... Kwanza alijiingiza kama mteja wa Tina, baadaye akaketi naye na kumuomba wafanye biashara ile pamoja, Tina akakubaliana naye kwa sababu alionyesha nia.. kweli wakafanya biashara ile kwa mafanikio, hatua kwa hatua ukaribu ukazidi kuongezeka na hatimaye yakafikia hapo yalipokuwa yamefikia. Nakiri kuwa kuna muda Tina alipokuwa akinieleza juu ya Abduli nilikuwa naguswa na pepo la wivu lakini kwa usalama wa afya yangu  nilikuwa napuuzia wivu ule...... Nilimsihi sana Tina afuate kile alichotueleza daktari kuwa ajitahidi sana kuwa na imani na asivisambaze virusi maksudi kwa kushiriki ngono zembe. Sasa Tina alikuwa anakabiliana na kijana Abduli ambaye alikiri kuwa alikuwa mmoja kati ya watu waliomfanya akue kibiashara na pia alikuwa rafiki yake wa karibu sana ukiniondoa mimi. Maisha yakaendelea kwenda mbele na ukaribu kati ya Tina na Abduli ukaendelea kuongezeka, Tina hakuacha kunishirikisha kuwa mara kwa mara Abduli ameendelea kumsihi juu ya kuwa naye katika mahusiano. Siku hii alikuja na wazo moja ambalo liliyazua mengine mengi...... Tina akashauri kuwa niigize kana kwamba mimi ni mpenzi wake ilimradi tu Abduli aache kumsumbua. Sikuona kama ni wazo bay asana kwa hapo awali kwa sababu yule tayari aliwahi kuwa mke wangu na hatukuwahi kutalikiana...... Kweli ikawa siku ambayo Abduli alikumbushia juu ya jibu lake kwa Tina, akaelezwa kuwa mimi ndiye mpenzi wake. Kitu ambacho tulikosea ni kwamba hatukujua kuwa moyo wa mwanadamu ni kichaka hujui ameficha nini humo. Abduli alikuwa anamaanisha aliposema anampenda Tina hivyo kitendo cha Tina kumueleza kuwa anaye mpenzi tayari lazima tu kingemvuruga kwa kiasi kikubwa sana. Kweli alivurugika!! Japokuwa hakuonyesha mbele ya Tina wakati uleule lakini ni dhahiri shahiri kuwa alichanganyikiwa...... Na maamuzi ya mtu aliyechanganyikiwa mara nyingi huwa ni maamuzi mabaya. Hata alichoamua Abduli hakikuwa kitu kizuri kabisa. Kwanza alivunja mawasilino na Tina kwa muda na kisha akajenga chuki ya waziwazi kwangu. Awali kila alipokuwa akienda nyumbani kwa Tina walipita nyumbani kwangu kunisalimia.... hili likaishia pale. Hata tulipokuwa tunakutana barabarani  hakuwa tayari kusalimiana na mimi. Mapenzi jama mapenzi! Yanaweza kukufanya ukafanya mambo ya kipuuzi bila kujua kama ni wewe unayafanya. Nilikuwa namsikitikia sana Abduli...... Kitu kimoja ambacho mimi na Tina tulikisahau ni kujiuliza je nini kinafuata baada ya kumfanyia vile Abduli? Tuliposahau kuwaza hilo yeye Abduli aliwaza nini kinafuata baada ya kumkosa Tina? Alichokiwaza nd’o kilichokuja kuleta mshtuko!! ***** Siku hiyo ilikuwa ni jumamosi tulivu kabisa jijini Mwanza, siku hii jioni baada ya shughuli zangu za hapa na pale nilijisogeza katika mgahawa mmoja wenye hadhi ya kati kwa ajili ya kupata kinywaji huku nikitazama mechi ya soka nakumbuka ilikuwa ni Manchester united na Liverpool zote za uingereza, mimi ni shabiki wa klabu ya Arsenal lakini mtanange huu kamwe huwa sipo tayari kuukosa. Nilikuta shamra shamra katika mgahawa ule, mashabiki wakipeana vijembe hapa na pale, nikafika na kuchukua nafasi nikaagiza kinywaji... Baada ya dakika tano mechi ikaanza. Ilikuwa mechi kali sana kiasi kwamba ilizichota akili zangu kwa dakika zotwe arobaini na tano hadi ukafika ule muda wa mapumziko ndipo nikakumbuka kuitazama simu yangu. Nilikuta kuna jumbe nne mpya.. nilipozifungua zote zilikuwa zinatoka kwa Tina. Nadhani sikuzisikia kutokana na yale makelele ya mashabiki lukuki Ujumbe wa kwanza uliuliza nipo wapi, ujumbe wa pili ulisema njoo, ujumbe wa tatu ulisema tafadhali njoo kwangu nimelewa, ujumbe wan ne ukasema tafadhali Mjuni nakuomba. Nilibanduka upesi kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekaa na kutoka nje. Nikazisoma tena zile meseji na kugundua kuwa zilikuwa zimetumwa dakika thelathini zilizopita..... Swali nililojiuliza ni kwamba imekuwaje Tina akaanza tena kunywa pombe wakati alikuwa ameacha kabisa hata ile ya kuonja.... Pili nikaikumbuka vyema ile tarehe huku nikijisemea isijekuwa ni sikukuu ya wajinga tarehe mosi Aprili!! Hapana haikuwa! Hapo nikajionya kuwa chelewa chelewa utakuta mwana si wako, nikachukua pikipiki upesi na kumpa maelekezo ya wapi anatakiwa kunipeleka. Akaondoa chombo chake kwa kasi ya kawaida ambayo niliridhika nayo,moja kwa moja hadi nyumbani kwa Tina. Alinifika nikashuka upesi maana pesa yake nilimlipa mapema kabisa. Nikaufikia mlango wa chumba cha Tina na kuugonga mara moja ile naugonga nikaona unafunguka kumaanisha kuwa haukuwa umefungwa kwa ndani. Kwa sababu nilikuwa mwenyeji sana pale niliingia tu bila kusita. Kweli harufu ya pombe ikanipokea..... Na Tina alikuwa amelala kitandani dhahiri akionyesha kutotambua lolote linaloendelea duniani. Nilimtikisa kama mara mbili na hapo nikatambua jambo jingine, alikuwa amejifunika ama amefunikwa shuka tu na ndani hakuwa amevaa kitu chochote...... Haikuwa kawaida ya Tina kulala kizembe namna hii..... labda baada ya kukaa mbali nami ndo alianza tabia hii..... Nilimtikisa sana lakini bado hakuonyesha kurejewa na fahamu zake vyema, uzuri ni kwamba mapigo yake ya moyo yalikuwa yapo sawa na alikuwa anapumua vyema. Kwa sababu alikuwa amelala bila kushusha chandarua chake niliamua kukishusha chandarua asiendelee kuwapa mbu faida. Wakati nashsha chandarua nikakutana na pochi ya kiume pale kitandani..... mshtuko ukanikumba. Ni nani alikuwa yu pamoja na Tina pale kitandani....

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni