Jumapili, 3 Januari 2016
HILA NO.12
SEHEMU YA KUMI NA TATU
YAKUBU Gama alijisikia kuwa yupo fiti kiasi cha kuanza rasmi harakati zake za kuusaka ukweli. Lakini mwili haukuwa imara, miguu bado ilikuwa dhaifu na alitakiwa kutembea hatua chache na kisha kupumzika. Sumu iliyokuwa katika bomu lililolipuka ilikuwa imemuathiri.
Gama hakutaka kupumzika zaidi, hivyo akaamua harakati hizi azifanye huku akiwa na wasaidizi. Alihitaji watu wa kufanya kazi kwa niaba yake. Alihitaji watu wachache na ikiwezekana hata mmoja tu mwenye roho ya paka isiyoogopa kifo na kifua cha chuma cha kutunza siri.
Ni wapi atawapata? Hili nd’o lilikuwa swali alilojiuliza kabla hajaamua kuwasiliana na mrakibu msaidizi Robert Masawe ambaye nd’o alifanikisha mipango ya kuokoa uhai wake. Huku akitilia mkazo suala la mwili feki wa Gama kuzikwa bila kuagwa kwa sababu ulikuwa umeharibika.
Mpango huo ukahitimishwa na ripoti ya daktari Macho ambaye lake lilikuwa moja na bwana Robert Masawe.
Robert Masawe, akitumia gari ya mkewe aliendesha usiku mnene, hadi Morogoro ambapo alikutana na Gama.
Baada ya salamu Gama alimweleza mambo kadhaa na kisha kumwomba amtafutie mwanamke mwaminifu mwenye kifua cha chuma na roho ya paka ambaye anaweza kushirikiana naye kwa ukaribu zaidi.
“Gama… huhofii kwamba mwanamke anaweza kutuharibia”
“Mwanamke mwenye kifua cha chuma ni zaidi ya mwanaume jasiri….” Alijibu Gama huku akiwa amemkazia macho Robert.
“Basi nipe siku ya leo nifikirie kwa kina maana hili jambo tunaloshiriki lina matokeo mawili…”
“Ni ama kufa kwa mateso ama kupona na majina yetu kudumu katika vitabu milele na milele” Gama alimalizia ile sentensi kabla hata Robert hajamalizia.
Robert akatabasamu na kujisikia fahari kuzungumza na kuwa katika mpango ule madhubuti na kijana machachari kama Gama.
“Laiti kama usingekuwa umejeruhiwa naamini hili jambo ungelimaliza mwenyewe tena upesi sana.” Robert alisema huku akisikitika.
Maongezi yao yakamalizika kwa ahadi ya kupata muafaka ndani ya masaa machache yajayo.
Njia nzima akiwa anaendesha gari bwana Masawe alijiuliza ni kwanini Gama alikuwa akihitaji mwanamke katika shughuli ile.. lakini hakutaka kuumiza kichwa sana kwani alikuwa na mtihani wa kumtafuta huyo mwanamke anayeweza kushirikiana na Gama.
Alifikiria sana juu ya watumishi wa jeshi la polisi ambao anaweza kuwaamini lakini nafsi haikutulia kwa yeyote. Akafikiria kwa kina sana hata watu kadhaa aliowahi kukutana nao maishani. Akafikiria na kukosa jibu.
Hapakuwa na yeyote wa kuweza kuaminika katika hili!
Hofu ya kuyakoroga mambo na mwisho kuishia kitanzini ilikuwa imemtawala Robert. Lakini maji alikuwa ameyavulia nguo, hivyo iwe isiwe sharti lilikuwa lazima ayaoge tu.
Alipofika mzani wa Mikese kuondoka kutoka Morogoro, mara kama radi vile akili yake ikawaka na kukumbuka kitu. Akamkumbuka dada yake lakini kutoka tumbo la mama mwingine.
Ilikuwa ni miaka mingi imepita bila kuonana naye. Lakini moyo ukajiachia kabisa kuwa iwapo hakubadili tabia zake basi ni yule alikuwa akimfaa kwa kazi iliyokuwa mbele yake.
Alikuwa na kifua cha chuma, jasiri asiyeyaogopa maisha.
Alikuwa na uwezo wa kuitunza siri kadri awezavyo, alikuwa muongeaji sana lakini bahati mbaya alikuwa hayasemi yaliyo siri kwake.
Hili jambo lilimfanya Robert amshauri dada yake aende jeshini. Lakini hilo likagonga mwamba, dada alikuwa na siri zake lukuki. Hatimaye akaondoka nyumbani pasi na kuaga.
Robert akaingia jeshini na ikapita miaka mingi sana bila kuonana.
Ssa alikuwa akiuhitaji msaada wake ndugu huyo!
Wapi pa kumpata? Alijiuliza.
Jibu lilikuwa jepesi tu, ni mtu mmoja tu ambaye angeweza kujua.
Huyu alikuwa ni mdogo wao wa mwisho ambaye alitokea kuivana sana na dada yao. Lakini na yeye alikuwa na tabia zilezile.
Roho ya paka na kifua cha chuma! Huenda nd’o maana wakapendana.
Akaitazama saa yake, ilikuwa ni saa nane usiku. Hakutaka kusubiri zaidi akaegesha gari pembeni, akaichukua simu yake na kubofya namba za mama yake mzazi.
Bahati nzuri mama hakuwa amelala, alikuwa kwenye sherehe fulani na nd’o ilikuwa inaisha.
“Haujambo…” aliuliza.
Mama tayari amelewa looh! Robert alijisemea baada ya kumsikia mama yake. Alimjua vyema alivyo rafiki wa pombe. Lakini uzuri ni kwamba hakuwa mtu wa kupoteza kumbukumbu hata akilewa.
“Mama unayo namba ya Subira… ninahitaji sana namba yake sasa hivi.”
“Amefanyaje mwanangu tena mnataka kumfunga”
“Aaah! Mama hapana….”
“Hana simu… nikifika nyumbani nipigie nitampa simu yangu mzungumze.”
Kweli baada ya nusu saa Robert akapiga simu, mama alikuwa nyumbani tayari na simu ikapokelewa na Subira. Mdogo wao wa mwisho.
“Shkamoo kaka.”
“Marahaba, Subira hivi mmefunga shule ama?”
“Ndio tumefunga.”
“Nahitaji kesho uje Dar…”
“Mbona ghafla kaka, mi nataka kusoma twisheni…”
“Ndio ni ghafla lakini nahitaji uje, unakuja na kuondoka baada ya siku chache tu…”
“Aaah! Mi na wifi hazipandi kaka, sitaki tugombane.”
“Hautafikia nyumbani kwangu, nitakupokea tutazungumza na utalala mahali na kisha kuondoka. Nakutumia pesa kwenye simu ya mama, usije ukamwacha akatoa yeye ataenda kunywa pombe pesa yote. Nenda ukatoe mwenyewe halafu asijue kama unakuja huku, si unamjua mama tena.?”
“Sawa kaka! Kama usemavyo itakuwa hivyo” alijibu kwa ufupi. Robert akakiri kuwa hakika alikuwa anazungumza na roho ya paka.
****
DAR-ES-SALAAM, Tanzania saa tano usiku!
Katika mgahawa mdogo ambapo chipsi huuzwa hadi majira ya saa tisa usiku. Robert alikuwa ameketi na mdogo wake wa mwisho, Subira ambaye alikuwa ametokea jijini Mbeya siku hiyohiyo. Na kuingia jijini Dar majira ya saa kumi na mbili jioni. Lakini waliamua kukutana majira hayo ya saa tano usiku kwa sababu za kiusalama zaidi. Alikuwa ni Robert aliyetoa ushauri ule.
Mgahawa ulikuwa na watu wachache sana, licha ya hayo walijitenga mbali kabisa na mwanga.
Kwa kuwatazama upesi ungeweza kudhania kuwa yule likuwa ni mtu mzima amechepuka katika ndoa yake na hapo yupo na mwanafunzi wanayeishi naye katika mapenzi ya siri. Na kule kukaa kwao gizani ni kuendelea kuipalilia siri yao kwa maua ya miiba.
Robert alikuwa mtulivu, lakini Subira alikuwa mtulivu na makini sana. Alipiga funda moja la soda yake kisha akamtazama kaka yake machoni, ikiwa ni ishara ya kumtaka aanze kuzungumza.
“Subira mdogo wangu, nia yangu ya kuonana na wewe ni kwa ajili moja tu. Kwa ajili ya kukomboa mamia ya watanzania kutoka katika maisha magumu wanayoishi.”
“Lakini mimi bado mwanafunzi! Unataka nijiunge na siasa ama” alijibu huku akimkazia macho.
“Natambua na nd’o maana nikaamua kuonana na wewe. Wanafunzi nd’o mzizi wa ukombozi” Akasita kisha akaendelea, “Hivi shuleni kwenu kuna waalimu wangapi?”
“Sidhani kama umeniita Dar ili kujua maendeleo yangu shuleni…” Subira alimkatiza.
“No! anyway, tuachane na hayo lakini nimekuita hapa nahitaji msaada wako mkubwa kupita yote.”
“Upi kaka..”
“Nahitaji kuonana na Sekela.”
“Dada Sekela?” Subira akahoji. Robert akatikisa kichwa kukubaliana na mdogo wake.
“Unafahamu alipo ama, maana ni miaka sasa hajarudi nyumbani. Naamini yupo Dar!” Subira alitoa jibu ambalo Robert alilitarajia.
Hivyo ikamlazimu kusimulia kila kitu kilivyo na ni kwa jinsi gani msaada wa Subira ulikuwa unahitajika ili Sekela aweze kupatikana. Alitambua wazi kuwa licha ya umri mdogo wa binti yule hakuwa akitekwa kirahisi kwa maswali ya mitego.
Robert akasimulia mkasa juu ya serikali inavyoendeshwa kihuni huku wenye haki wengi wakiishi kama digidigi katika nchi yao ambayo inajitamba kuwa ni nchi huru kwa watu huru.
Alipomaliza kusimulia juu ya ugumu anaokutana nao hasahasa imani ya IGP na raisi juu ya mtu mbaya mzee Matata machozi yalikuwa yanamlenga Subira.
“Mzee Matata.. sura yake siku ambayo ameleta msaada wa vitabu shuleni kwetu haikunivutia kabisa kuamini kuwa eti amefanya vile kwa sababu ya huruma kwa watanzania. Walinibishia sana wenzangu lakini sasa naanza kupata imani na kila nilichokuwa nawaza siku ile…” Subira alizungumza kwa sauti ya chini huku akitikisa kichwa juu na chini.
Maelezo ya kaka yake yalikuwa yamemgusa haswa na kuamua kumuamini na kumfungukia kile akijuacho.
“Kaka, kumbuka yule ni dada yako, hata kama baba zenu ni tofauti anabaki kuwa dada yako tu. Nakumbuka uliwahi kusema kuwa polisi hana ndugu, kama umeamua usemi huo uzidi ule wa damu nzito kuliko maji basi amini kuwa mateso atakayopata dada yatakuwa juu yako na laana ya mama itakuangukia kwa sababu nitamweleza iwapo mambo yataenda kinyume. Mimi nitakukutanisha na Sekela, ila uyashike hayo niliyokueleza….”
“Subira, niamini mimi siwezi kufanya ujinga kama huo hata siku moja….”
“Sekela yupo Morogoro, nitawasiliana naye na kukutanisha naye. Kesho usiku… naomba unipeleke nikalale sasa…” alimaliza Subira na kusimama, Robert naye akasimama.
Wakaondoka hadi nyumba ya kulala wageni ambayo Robert alikuwa amemuandalia mdogo wake.
Usiku ule ukapita!!
****
MOROGORO, Saa mbili usiku.
Subira alikuwa katika nyumba ya wageni tayari alikuwa amewasiliana na dada yake juu ya kuonana kwao.
Hakumweleza kabisa juu ya ujio wa bwana Robert. Hivyo Sekela hakutilia mashaka yoyote na majira hayo alikuwa amekaribia katika chumba kile.
Walipeana mambo kedekede ya hapa na pale huku mdogo mtu akiwa mwingi wa maswali ya hapa na pale huku akihitaji kujua nini hatma ya dada yake katika kuusaka uhuru wake tena.
Kabla hii mada haijafika mbali mlango wa chumba kile ukagongwa. Subira alijua nini kinaendelea, mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana lakini alijikaza asionekane mwoga. Akauendea mlango na kuufungua. Na hapo akaingia Robert Masawe.
Ana kwa ana na Sekela ama maarufu kwa jina la mama lao. Dada yake kutoka kwa baba mwingine lakini mama yao akiwa ni mmoja.
Mama lao hakuonyesha mshtuko wa aina yoyote lakini jicho lake liliwaka haswa kumaanisha kuwa yu katika hasira kali mno.
Moyoni alijua tayari amekamatika, alitaka kumvamia Robert ili akabiliane naye lakini akashangazwa na upole wa yule bwana.
“Dada nisamehe bure, lakini amini kuwa hautajutia litakalozungumzwa maana hata wewe linakuhusu… kaka kama ulikuwa hujafahamu huyu hapa anaitwa mama lao, sahau kuhusu Atuganile au sekela. Bila shaka kila mmoja anamuhitaji mwenzake iwapo uliyonieleza ni ya ukweli”
“Sijabadili chochote katika maelezo yangu ya awali…”
“Basi mimi nawapisha!” Subira akasimama na kutoweka.
Mama lao akazungumza kwa kina na Robert, hatimaye akaondoka naye wakati huohuo wa usiku.
Akaenda kukabidhiwa kwa Yakubu Gama!
Naam! Kikosi kazi kikaanza kujengeka!
Baada ya kumwona mama lao na umbile lake, Yakubu alitaka kumpuuzia lakini walipoanza kuzungumza tu. Ile hali ya kujiamini ya mama lao ikamfanya aanze kuamini anazungumza na mwanamke wea shoka.
Mama lao akamueleza Gama juu ya kutekwa kwake na kuponea chupuchupu kufa mbele ya mikono ya wanaume wa kinyakyusa, Gama naye akamweleza mkasa wake uliotaka kuondoka na uhai wake.
Katika maelezo yao, kila mmoja akajikuta katika fumbo la nani ni BVB.
Yakubu Gama akawa kiongozi wa huu mchezo, mama lao akawa mtekelezaji. Kikosi kazi kikawa kinamkosa jemedari mmoja tu, huyu alikuwa ni Sam. Alikuwa akihitajika sana ili kuweza kukamilisha huu mchezo. Mchezo ambao Yakubu Gama aliubatiza jina la Kombolera
Mama lao alihoji nini maana ya Kombolera katika jambo hili zito. Lakini Gama akamwambia aelewe kuwa hiyo ni kombolera tu na mwishowe hatauliza tena kwa nini yaitwa kombolera. Bali atajiona mwenyewe akicheza kombolera
“Haya kombolera yetu inaanzia jijini Dar es salaam.” Gama akaagiza kisha usiku ukawa mwingi wote wakalala.
Hello, nimependa na wewe mwenzangu usome hadithi hii nzuri. Utafurahi naamini. Ili usipitwe na hadithi tamu na nzuri nyingi kama hizi, unaweda download Hadithi App kutoka PlayStore kwa kubonyeza hapa: https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni