SEHEMU YA NNE Kile kitendo cha kutambua kuwa simu iliyokuwa kiganjani mwake haikuwa ya kwake bali ya mchumba wake kilimfadhaisha sana Sam na hapo kengele ya hatari ikalia katika kichwa chake. Ni kitu gani kinatokea hapa?? Akajiuliza bila kuyapata majibu sahihi. Akili yake ikaiunda picha iliyotokea kituo cha polisi pindi alipokuwa anahojiwa, alikumbuka namna mpelelezi wa kesi yake alivyomuuliza juu ya uhalali wake katika kuimiliki simu ile, akakumbuka namna alivyojibu bila wasiwasi na hata alipoambiwa apige namba yake akajaribu lakini kinyume na matarajio ikaita upande wa pili. Inamaana niliingia mahabusu na simu ya mke wangu ama? Alijiuliza tena lakini safari hii akiishika tena ile simu na kisha kujaribu kupiga namba yake afahamu ni nanji huyo aliyekuwa na simu yake… japo kwa makisio alitambua kuwa Tina ndiye anayeweza kuwa na simu ile na si mwingine. Alipopiga simu haikuwa ikipatikana! Sam akaishiwa nguvu na ubaridi ukajipenyeza katika ngozi yake. Akaitambua kuwa ile ni dalili ya uoga jambo ambalo hata yeye mwenyewe alishangaa ni kwa nini anaogopa. Kutopatikana kwa simu yake hewani kukamkumbusha namna yule mpelelezi wa kesi yake ambaye hakupata hata kumjua jina lake alivyoshtuka baada ya simu ile kuita upande wa pili. Kuna nini? Alijiuliza. Na wakati huohuo akatoka na mwayo mrefu na tumbo likaunguruma. Akakumbuka kuwa hakuwa ametia chochote mdomoni tangu aingizwe mahabusu na hata alipoachiwa bado hakukumbuka kutii haja za tumbo lake. Sam akaituliza akili yake na kujaribu kupuuzia kila kitu kilichokuwa kimetokea huku akijiaminisha kuwa Tina wake yupo salama na kila kitu kilichotokea yawezekana ni makosa tu yaliyofanywa na jeshi la polisi. Aliamua kujifariji hivyo ilimradi tu aweze kuiruhusu akili yake kuuongoza mwili wake kufanya mambo mengineyo. Mojawapo likiwa ni kula!! Alikuwa na njaa!! Njaa ikamfanya amkumbuke Mama Lao…. Na hapo akafanya tabasamu la matumaini…… hakujua kama alikuwa akikifuata kizaazaa!!...... ***** MAMA LAO MGAHAWA, ulikuwa mgahawa maarufu sana wilayani Temeke. Hata kwa ambao hawajawahi kufika waliutambua kwa jina. Na hii ni kwa sababu ya huyo Mama lao mwenyewe… mmiliki wa mgahawa ule. Kwa jinsi jina lilivyokuwa kubwa usingeamini macho yako pale ambapo ungefika eneo la tukio na kukutana na majamvi yasiyozidi sita yaliyozungushiwa katika miti kadhaa, turubai chakavu liliunda kivuli katika namna ya mapengo mapengo. Maneno mengi ya mama lao, ucheshi na ukarimu kwa wateja wake ilikuwa ngao kuu ya kuwavutia watu wengi. Hata Sam na Tina licha ya kuwa na kipato kikubwa kiasi bado waliweza kujumuika mara kadhaa katika mgahawa ule kujipatia vitafunwa, supu na mara moja waliwahi kukaa kwa ajili ya chakula cha mchana katika banda lile maarufu. Lakini umaarufu wake haukulipuka ghafla tu!! Umaarufu wa banda lile ulikuzwa zaidi na kitendo cha Sam na Tina wake kujumuika na muigizaji maarufu Steven Marashi katika banda lile kwa ajili ya kula supu ya makongoro. Si mama lao pekee aliyetokwa macho kumshangaa marashi bali kila mteja aliduwaa na asiamini kile alichokuwa akikiona. Steve naye hakuuacha ucheshi wake uishie runingani tu… aliuendeleza hadi pale. Waandishi wa habari hawakuwa nyuma… baada ya kusikia habari za Steve Marashi kukutwa katika banda bovu la mama lishe walifanikiwa kunasa picha kadhaa, nyingi na maarufu zikiwa zile ambazo steve alikuwa ameshika kongoro akilipeleka mdomoni. “AMINI USIAMINI STEVE MARASHI AMEFULIA AKUTWA KWA MAMA LISHE AKILA KWA MKOPO!!” “STEVE MARASHI AISHIWA!” Hivi vilikuwa vichwa vya habari katika magazeti mbalimbali ya udaku. Steve alipohojiwa katika vipindi mbalimbali alilipaisha kadri awezavyo banda la mama lao. Kama hiyo haitoshi Steven Marashi akarekodi filamu yake moja huku akilitumia banda lilelile la mama lao…. Na hapo sura ya mama lao ikatambulika kwa wengi. Na hapo kila mtu akalitambua banda lile hata ambaye hajawahi kuliona. KITENDO cha kuambatana na Steve Marashi kilimfanya Sam awe anatazamwa kwa jicho la tatu na watu mbalimbali huku wengi wao wakimuonea gele. Tofauti na siku nyingine ambazo Sam huwa anafika kwa mama lao na utani wa hapa na pale huku mama lao akiulizia wapi alipo Steve Marashi…..siku hii ilikuwa tofauti. Sam alikuwa mkimya na mama lao naye alikuwa mkimya zaidi. Kila mteja aliyeutambua urafiki wa Sam na Steve alikuwa akimtazama kwa jicho la huruma bila kusema neno lolote. Alikuwa ni mama lao aliyezua kizaazaa!!....... Ilianza kwa sauti ya chini!! Mama lao akawa anasemasema peke yake huku akifunyanga vidole vyake, maneno haya hakuna aliyeyaelewa!! Sauti ilipopanda juu kiasi ikaonekana alikuwa akizungumza kikabila ambacho pia hakuonekana aliyekuwa akikifahamu. Na hatimaye kikafuata Kiswahili…. Mama lao akawa anaomboleza kifo cha Steven Marashi katika namna ya kulaumu. Mara amlaumu Mungu, mara amlaumu marehemu mwenyewe na hatimaye akapaza sauti akamlaumu Lilian. Na hapo akaanza kujigalagaza chini, ikawa ni shughuli ya wateja kuhangaika naye. “Uuuuuuuwi!! Lili weeeee, umeniulia mwanangu Lili weeeeee…… uuuwi Sam weeee wamekuuulia rafiki yako Sam weeeee….” Mama lao aliendelea kupiga mayowe bila kukoma. Banda la jirani wakakisikia kilio cha mama lao, walikuwa akina mama… walipofika wakaungana katika kilio wakijua tayari mama lao amefiwa! Walianza kulia wasijue amefiwa na nani… walilia tu! Wanawake!! Penye wengi hapakosi mengi, wakati wengine wakihangaika na mama lao, vijana wengine waliitumia fursa hiyo kutoroka bila kufanya malipo na wengine wakiiba vitu vichache vilivyokuwa katika banda lile. Bila hawa vijana kutambua ni kitu gani wameiba…. Waliiba kitu kimoja cha muhimu sana!! Hata mama lao alipotulia hapakuwa na uwezekano wa kuendelea tena na biashara kwa siku ile. Sam alirejea nyumbani kwake huku picha ya Steve akiwa marehemu ikianza kumwingia vyema kichwani na kuamini kuwa ni kweli swahiba wengi alikuywa amekufa. Alitamani kuwapigia simu waandishi wenzake ili aweze kujua ni nini kimemuua Steve lakinio alihofia kupata majibu kadha wa kadha yasiyoshabihiana na mwishowe yamchanganye kabisa. lakini akapiga moyo konde na kuamua kumpigia mmoja wapo wa waandishi na pia rafiki yake wa karibu. Alipoishika simu aweze kumpigia akakumbuka kuwa ile haikuwa simu yake, hivyo hata namba asingeweza kuipata. Wakati akiitazama simu ile akakutana na ujumbe ambao hajui uliingia muda gani. Akaufungua bila kusita. “Shoga eti wanasema mimi nimemuua Steve jamani…. Shoga naenda kufia jela mimi.. najua ni wewe unayeweza kuniamini. Hata nikiwa jela tambua kuwa nisingeweza kumuua Steve hata kwa kulazimishwa….. I will miss u.” Sam alirudia kuusoma ujumbe ule mara mbilimbili, mikono yake ikaanza kuvujwa jasho. Huyu ni nani anayesadeikika kumuua Steve? Na anafahamiana vipio na Tina? Alijiuliza huku akizitazama namba zile zilizohifadhiwa kwa jina la SLM. Namaba zilezile zilizotuma ujumbe wakati akiingia mahabusu!! Akili yake ikafyetuka ghafla, zile lawama kuwa polisi wanaweza kuwa walimbadilishia simu wakati yupo mahabusu zikateketea na kuamini kuwa alibadilishiwa simu mapema kabisa hata kabla hajaingia mahabusu. Nani mwingine kama sio Tina…. Wivu wa kipuuzi kabisa!! alighafirika Sam. Na kwa jinsi tukio lilivyokuwa zito akaona ni heri afike nyumbani kwa mama Tina aweze kumweleza anayoyafahamu juu ya tukio hilo ili wajue ni wapi wanaweza kuanzia kuutafuta utatuzi wa Tina kukamatwa na polisi. Njaa ilikwishatokomea zake, akajiandaa upesi na kuchukua pikipiki maarufu kama bodaboda… ikamfikisha nyumbani kwa mama Tina. Salamu yake ilijibiwa kinyonge sana, tena bila kutazamwa usoni kama alivyozoea mama yule kumtania kwa kumuita majina yanayowakilisha mapenzi mazito. Sam akatambua kuwa mama mkwe wake alikuwa amenuna!! Kukaa kimya kusingesaidia Sam akalazimika kuuliza maswali mawili matatu. “Hao polisi walimkamatia wapi Tina…” “Hapo nje!” “Walikuwa wamevaa sare za kipolisi..” “Sikumbuki!!” alikuwa akijibu kwa kiburi fulani…. Sam akaamua kuwa mkali kiasi … “Mama, nina uchungu mkubwa sana kusikia kuwa….” “Weee komea hapo..uwe na uchunmgu hadi dakika hii hujui mchumba wako alipo. Uchungu gani we mwana nauliza…eeh! Uchungu upi hujui kama mwenzako yupo anapigwa huko na hao maaskari we umelala tu…” mama mkwe aling’aka. “Mama nimelala mahabusu jana. Nilikamatwa kama alivyokamatwa Tina bila kuijua sababu yangu…nimeachiwa usiku wa manane.. nikadhani kuwa Tina yupo hotelini. Nikapiga simu yake naambiwa inatumika. Lakini baadaye sana nikagundua kuwa Tina anayo simu yangu na mimi ninmayo yake, sijui kama alinibadilishia ama nilichanganya wakati naondoka. Si unafahamu kuwa zinafanana kila kitu simu zetu. Hadi hapa ninapozungumza na wewe sijui kinachoendelea…. Nd’o nimekuja hapa tujue nini kinatokea. Lakini kwa ufupi na ufinyu sana kuna mmoja wetu ama wote kwa pamoja tunahusishwa juu ya kifo cha Steven ‘Ven’ Marashi..” alizungumza kwa sauti ya kunong’ona lakini inayoonyesha msisitizo. Macho yakamtoka mama Tina aliposikia mstari wa mwisho. Mwanaye kuhusishwa na kifo cha msanii yule maarufu. Akanyanyua mikono yake na kuiweka kichwani kisha akafumba macho kama anayekabiliana na hali fulani ya kuzuia kumbukumbu fulani isimpotee. “Nilimkataza lakini Tina…” “Ulimkataza nini mama….eeh!” Sam alihoji kwa shauku. Lakini mama hakujibu zaidi ya kuendelea kulalamika peke yake. “Hawa watu maarufu kujifanya anawajuajua….ona sana..” alijisemea mwenyewe. Sam akamtuliza na kumweleza kuwa kila jambo litaenda sawa. Na hapo akaaga kuwa anaelekea vituo kadhaa vya polisi kumtafuta Tina. Alizurura siku nzima vituo vyote vikubwa akimuulizia Tina, lakini hakupata walau fununu juu ya wapi alipokuwa mpenzi wake huyo. Kila kituo hawakutambua jina la Christina wala kutambua msichana yeyote aliyekamatwa katika mazingira ambayo Sam alijaribu kuyaeleza. Hali hii ilimtia katika utata. Alitarajia kuwa litakuwa jambo jepesi tu kufanikiwa kumpata Tina lakini haikuwa hivyo. Namba za makachero kadhaa alizokuwa anazifahamu zilikuwa katika simu yake ambayo hakuwa nayo tena. Jambo hili likamtesa sana. Wakati akiendelea kuhangaika, majira ya saa mbili usiku simu ya Tina aliyokuwanayo ikaita. Haikuwa mara ya kwanza kuita, na mara zote hakuwa akipokea. Akaitazama macho yakamtoka pima. Ilikuwa ni namba yake ikiwa inampigia. Akatambua kuwa iwe isiwe lazima atakuwa ni Tina anayepiga maana ndiye ambaye alikuwa na simu ile. “Sisi ni vibaka wastaarabu.. tumeokota simu hapa Koko Beach. Sisi hata shida ya hii laini hatuna, shida yetu ni simu tu. Kwa hiyo tunakuachieni laini yenu hapa katika mwamba huu uliopo ndani ya maji. Tunaiwekea kijiwe juu yake, ukiwahi asubuhi utaikuta lazima… hata ukirudi sasa hivi. Asante kwa simu bosi..” ilikuwa ni sauti ya kijana muathirika wa madawa ya kulevya (teja) ikikoroma upande wa pili. Na kabla hajajibu chochote simu ikakatika. Alipojaribu kupiga haikuwa ikipatikana na kamwe hakuipata tena!! Kengele za hatari zikaanza kupiga katika kichwa chake, kupatikana kwa simu yake maeneo ya fukwe za Koko kulimaanisha kuwa Tina hakuwa kituo cha polisi tena ama la kuna hila zinafanyika ambazo yeye binafsi hajui nini yaweza kuwa sababu. Taarifa ya kupigiwa simu kwa namba yake hakuifikisha kwa mama mkwe wake mapema usiku ule. Alihofia kuwa mama yule anaweza kupagawa na labda shinikizo la damu linaweza kumhangaisha. Akajiahidi kuwa siku inayofuata asubuhi ataenda kumweleza kila kitu alichofanikiwa kufanya kwa siku nzima. Ni vile tu wanadamu hatujui lijalo… lakini laiti kama tungejua lijalo. Sam angemweleza tu mama mkwe wake…. Huenda angemwepusha na mengi!! Ila hakujua….. ***** Taarifa ya kupigiwa simu kwa namba yake hakuifikisha kwa mama mkwe wake mapema usiku ule. Alihofia kuwa mama yule anaweza kupagawa na labda shinikizo la damu linaweza kumhangaisha. Akajiahidi kuwa siku inayofuata asubuhi ataenda kumweleza kila kitu alichofanikiwa kufanya kwa siku nzima. Ni vile tu wanadamu hatujui lijalo… lakini laiti kama tungejua lijalo. Sam angemweleza tu mama mkwe wake…. Huenda angemwepusha na mengi!! Ila hakujua….. *****
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni