Jumamosi, 12 Desemba 2015

HADITHI RIPOTI KAMILI SEHEMU YA TATU

SEHEMU YA TATU
Iliwahi kuwa mijadala ya kawaida tu wakati wa maisha yangu kijiweni, tulikuwa tunajiuliza ni umri gani sahihi kabisa kwa mwanaume kuoa ama mwanamke kuolewa? 
Kuna waliosema miaka 30, wengine wakasema ndoa haijalishi umri cha msingi umpate wa kukupenda na wewe umpende.....
Lakini kuna mmoja alisema kuwa kumpata anayekupenda na wewe ukampenda ni ngumu sana kutokea katika maisha halisi, akasema kuwa ukishampata ambaye wewe unampenda basi mfundishe na yeye kukupenda na hapo mtaenda sawa!!!

HII NI SEHEMU YA TATU.

Baada ya yale maneno ya rafiki yangu kuwa kuna mgeni asiyekuwa wa kawaida aliwahi kufika pale nyumbani kwangu, na ile kumbukumbu ya uwanja kufagiliwa jioni katika hali isiyokuwa ya kawaisda nilipanga kufanya uchunguzi mdogo kabla sijamuuliza jambo lolote mke wangu.
Lakini baada ya kufika nyumbani na kuoga niligundua kuwa fikra zangu zilikuwa za kipuuzi sana, yaani nianze kufanya uchunguzi juu ya mwanamke aliyekuja kuzungumza na mwabnamke.
Hapana!!
Halikuwa jambo sahihi kwangu hata kidogo, niliona ni heri ya wanawake nikawaachia wanawake. Angekuwa mwanaume hapo sawa ningetakiwa kupata mashaka.
Nikaamua kuachana na mashaka haya, na yale maneno ya marafiki nikayasahau nikaendelea kumtumikia mke wangu yule aliyekuwa mjamzito.
Miezi ya ujauzito ule ilipofika minne, mke wangu akiwa na kisilani chake kilekile aliniletea hoja kuwa anahitaji kwenda kumsalimia bibi yake ambaye naye anaitwa Christina na huku ndipo alipolipata hilo jina la Tina.
Nilipojaribu kumueleza kuwa atateseka akienda huko kwa sababu ni mimi pekee ambaye naweza kumuelewa katika hali ile aliyonayo, hapo sasa ikawa kesi akanuna akagoma kula na kisha akanifukuza chumbani eti niwe nalala sebuleni.
Nilibaki kucheka tu huku nikiamini kuwa ni ile mimba yake imekuja na mauzauza yale ya kunichukia. Na hii ipo hivyo kuna wakati mwanamke akibeba mimba anakupenda sana lakini mara nyingi hujenga chuki na kisilani kisichokuwa na maana, hata atakapojifungua na ujaribu kumueleza ataruka maili mia akikataa kabisa kuwa si yeye aliyekuwa anafanya hayo!!
Kuliko kukubaliana na mambo ya kulala sebuleni huku mke wangu amenuna kitandani nikaamua kumruhusu kwenda kwa bibi yake huenda ni huyu ambaye ujauzito ule ulikuwa umempenda.
Akaniaga akaondoka baada ya siku mbili!!
Alipokuwa huko mambo yakabadilika, kila mara ananipigia simu, na alikuwa mwenye furaha sana. Hali hii ilinifanya niwe nacheka mwenyewe tu kwa sababu ilikuwa ni kama kituko.
Tulipanga majina ya kumuita mtoto akiwa wa kiume ama akiwa wa kike....

Niliendelea kuishi peke yangu, kuna marafiki walinishangaa sana kumruhusu mke wangu kuwa mbali na mimi huku akiwa na hali ile, niliwapuuza kwa sababu niliamini kabisa kuwa yanayotokea ndani wao hawajui. Hata mama yangu mzazi alisema kuwa si jambo la heri, ilikuwa mapema sana kumwacha mke wangu kuwa mbali na mimi, nilijaribu kumgusia mama juu ya hali ilipokuwa imefikia.
Akaguna na kisha akasema ya kwetu anatuachia sisi, lakini niwe makini sana na mke wangu maana wao wanawake wanajijua wenyewe.
“Yaani hata sisi kwa sisi hatujuani vizuri, sembuse nyie wanaume kutujua sasa..... ila sina maana mbaya mwanangu, nakusihi tu!!” mama alinieleza tulipokuwa tunazungumzia lile jambo.
Maneno haya ya mama yaliyokuwa katika mfumo wa fumbo ndiyo yaliiamsha akili yangu na kuamua kufikiria mara mbilimbili.
“Mama yangu ananipenda sana hawezi kuniambia jambo lisilokuwa na mantiki...” nilijionya na hapo nikachukua hatua thabiti.
Nilijionya sana nikiwa peke yangu ndani kuwa kwa lolote lile nitakalokuta kuwa haliendi sawa basi moyo wangu na uwe na subira kuu.
Nadhani ni onyo hilo ambalo liliniwezesha kuwa imara sana.
Nauli ya kwenda nyumbani kwa bibi yake Tina kwa daladala ilikuwa shilingi mia tano na kwa pikipiki ilikuwa shilingi elfu sita.
Nilitenga bajeti kwa ajili ya ripoti hii!!
Kwa sababu ilikuwa ni ripoti kamili... ripoti niliyoifuatilia kwa muda wa mwaka mmoja na nusu bila kuchoka, wakati huo moyo wangu ulikuwa wa baridi sana.......
Naam! Hatimaye ikawa ripoti kamili!!!
Ni ripoti ambayo ningekuletea wewe pekee isingekuwa na maana, badala yake ripoti hii nilimsomea muhusika mkuu.

ILIKUWA Imepita miezi mitano tangu Tina mtulivu kabisa awe amejifungua mtoto wa kike, mrembo ambaye alidai kuwa amefanana kila kitu na bibi yake.
Ndugu msomaji na msikilizaji, kumbe ukiamua kuuamrisha moyo upoe unapoa tu..... Watu wengi huwa wanaumizwa na hisia za mapenzi kwa sababu hawana amri kuu katika mioyo yao, unamkuta mwanamke anagundua kabisa mpenzi aliyenaye anamsaliti mara kwa mara. Kila akigundua hili anaishia kulia na kukonda kwa mawazo, uamrishe moyo wako sasa uambie imetosha sitaki uwe mjinga mjinga ewe moyo wangu!! Moyo utatii amri yako....

Wakati huu moyo wangu ulikuwa umepoa sana na nilikuwa tayari kuisoma ripoti kamili.
Siku hii nilimchukua mke wangu pamoja na mtoto wangu kwa ajili ya mtoko wa kawaida tu ambao ungeweza kufanyika siku ya mapumziko aidha jumamosi ama jumapili lakini mimi nilifanya hivi siku ya jumatano. Ikiwa ni miezi kumi na nane kamili tangu nianze utafiti wangu.
Niliondoka na mke wangu mbali kabisa na wilaya niliyokuwa naishi, kuna mahali nyumba ya kulala wageni nilikuwa nimechukua chumba kikubwa kabisa kilichotutosheleza.
“Umepajuaje huku?” aliniuliza mke wangu akiwa amembeba mtoto..... nilimtazama na kumweleza kuwa kuna rafiki yangu alinielekeza na aliwahi kuja naye hapo siku ya fungate lake. 
Tina akatikisa kichwa kukubali....
Tuliingia na kutulia, tukaagiza chakula cha mchana kwani chai tulikuwa tumekunywa nyumbani tayari.
Nilizungumza na Tina na kupanga mipango yetu mingi tu ya siku za usoni. Pia tukapanga mambo lukuki ili mwanetu aweze kuishi katiika mazingira mazuri siku zijazo.
Baada ya kuweka oda yetu ya chakula na kuwa tumepanga mambo yote hayo, niliuendea mlango na kutoa funguo bila yeye Tina kuwa na ufahamu iwapo nimefanya jambo lile.
Nilikuwa na sababu maalumu za kufanya vile.
Nikarejea kuketi kitandani wakati huo mtoto alikuwa amelala.....
Nikatoa kitabu changu kidogo cha kumbukumbu na kumueleza Tina kuwa kuna jambo dogo sana nahitaji kumueleza na anatakiwa kuwa msikivu na mwisho kabisa kama likiwepo la kuongezea anaweza kuongezea.
“Mh! Vipi ramani ya nyumba au?” alidakia huku akiwa na mshawasha wa kujua ni kitu gani nilichotaka kumweleza.
“Hapana sio ramani ya nyumba hii mke wangu, hii ni ripoti kamili.” Nilimjibu huku nikilazimisha tabasamu.
Sasa moyo wangu uliokuwa umepoa ulianza kuchafukwa na kitu nisichokijua.......
“Hee! Ripoti kamili? Zipi hizo?” aliniuliza akiwa mwenye furaha.
“Naomba uvumilivu wako sana, usiingilie nikiwa natoa ripoti hizi... nakusihi sana mke wangu...” nilimwomba huku nikipambana kuidhibiti hali ile ya kuchafukwa iliyokuwa ikinilazimisha kufanya jambo ambalo sikutaka kabisa.

“Tina kipenzi changu, mwanamke pekee ambaye nakutambua kama mke wangu na dunia nzima inajua hivyo..... mwanamke uliyenifanya hadi leo hii sijui ladha ya sigara, nimesahau mambo ya kijiweni, ni msafi kupindukia. Napenda kukueleza kuwa kabla sijaisoma ripoti hii tambua kuwa nakupenda sana.... maneno haya yamenyooka na sijalazimishwa na mtu. Nakupenda Tina.” Nilisita na kumtazama akiwa anayepoteza amani yake usoni, mikono yake nayo ikimtetemeka.

***Naam Tina anangoja kuisikiliza ripoti kamili...... usikose kusikiliza pamoja naye ripoti hii........ ni kesho tena hapahapa katika ukurasa huu...

ITAENDELEA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni