Jumamosi, 12 Desemba 2015

HADITHI RIPOTI KAMILI SEHEMU YA TANO

SEHEMU YA TANO “Tina hivi unajua nampenda mtoto huyu kwa kiasi gani? Hivi unajua mama yangu anampenda kiasi gani mjukuu wake na vipi kuhusu babu yake.. unawaona wanavyompenda na kumjali mtoto huyu!!!?” akatikisa kichwa kukiri kuwa ni kweli ninayosema. “Sasa jiulize ni wanaume wangapi hapa duniani wanaweza kupenda watoto wasiokuwa damu yao huku wake zao wakiwa wamewaaminisha kuwa ni damu zao, jiulize kina babu na akina bibi wangapi wanaweza kupenda wajukuu wasiokuwa wao katika maana halisi.” Nikasita na kumtazama Tina akiwa anahaha huku na huku. Mara akashika glasi ya maji ili anywe. “Kunywa maji Tina kisha nikueleze nilijuaje kuwa huyu si mtoto wangu....” Hata yale maji hakunywa aliishia kuinua glasi na kuitua tena mezani, alitaka kuzungumza nikawahi kumziba mdomo wake asiseme neno lolote, na sikuruhusu tabasamu litoweke katika uso wangu niliendelea kutabasamu ili Tina aidha awe na amani ama ashindwe kabisa kunisoma iwapo nipo katika hasira ama hali tu ya kawaida. Baada ya kuwa ametulia niliendelea kusimulia. “Tina...  shem Stela hivi yupo wapi siku hizi?”  Nilimuuliza lakini sikuwa namaanisha kuwa nahitaji jibu lake. Niliendelea kusimulia,  “Tina utake usitake na hata kama machoni utakataa lakini nafsi yako lazima inakusuta tu kuwa dada yako yule ni mtu mbaya sana, yaani kati ya wanawake wenye roho chafu niliowahi kukutana nao basis hem Stela yupo katika orodha tena huenda hata kumi bora yumo. Yaani kweli Tina na akili zako ukitambua wazi kuwa ninakupenda na ninakuthamini lakini bado ukawekwa kikao na kujazwa ujinga wa kitoto namna ile......” nikasita nikacheka kidogo, Tina akashtuka sana. Nikacheka tena kisha nikaendelea. “Tina, yaani na umri wako ule ukashawishiwa na dada yako jambo la ajabu kama lile. Yaani kisa pesa kisa pesa Tina..... eti hapa nikikuuliza sababu utasema sababu ni bikra.... sawa ni yeye aliyekutoa usichana wako na kukuingiza katika ulimwengu wa mapenzi lakini hii si tija Tina. Sawa alikuwa mwanaume wako wa kwanza, kwani mimi katika kumbukumbu zangu simtambui msichana wangu wa kwanza au? Namkumbuka vizuri sana japokuwa mimi sikuwa wa kwanza kwake... lakini nilipoamua kuingia katika maisha ya ndoa nikaamua kusahau kila kitu. Ndugu msikilizaji napenda kukusihi jambo moja la muhimu. Kamwe usilete mambo ya kabla ya ndoa katika ndoa yako, ama hata kama sio ndoa basi kwa kijana, usikubali kuleta mambo ya kabla ya mahusiano kwenye mahusiano yako ya sasa. Eti umeoana na mtu hapo kabla hamjaoana mlipenda sana kufanya starehe, leo hii mmeoana mnataka kuendelea kufanya starehe badala ya kufanya maendeleo. Ama eti unakuwa kama Tina, kisa kabla sijamuoa kuna mwanaume wake wa kwanza aliyemtoa usichana wake na kumuingiza katika ulimwengu mpya, hadi nakuja kumuoa anaendelea mahusiano na mwanaume yule. Hili ni daraja la juu la upuuzi tafadhali liepuke..... Tina! Ulikosa kitu gani kwangu hadi ukaamua kujiingiza katika mahusiano na bwana yule, tena mke wa mtu daah! Inauma sana Tina, hebu simama Tina wangu.. simama ujitazame jinsi ulivyokuwa msichana mwenye mvuto, jitazame ulivyokuwa msichana jasiri. Lakini ajabu eti ujasiri wako ukaishia katika dhambi hiyo, jiulize mkewe akisikia ripoti hii atajisikiaje, kwamba wewe Tina ambaye ni mke wa mtu umeenda kumbebea mimba mume wa mtu tena kwa makubaliano kabisa. Tina ukanifanya mi mpuuzi kweli, yaani ukashirikiana na dada yako mkapanga kuwa mimi na wewe tusipate mtoto kwanza ili umzalie huyo Malaya mwenzako. Sikia Tina, kama ulikuwa haujajua jambo moja ni kwamba katika pita pita zangu kuikamilisha ripoti hii nimegundua mambo mengi sana, dada yako alikufanya wewe daraja tu.. unatumika atakavyo lakini kuna jambo alikuwa ananufaika nalo. Yule mzazi mwenzako alikuwa akimlipia ada ya chuo. Alikuwa pia anamnunulia simu mpya kila zilivyokuwa zinatoka. Wewe ukawa unaamini kuwa eti mapenzi ndo yalikuwa yanakuendesha, pole Tina ulikuwa mtumwa wa mapenzi.” Nilipotaka kuendelea mara kitoto kiliamka na kuanza kulia japokuwa si kwa sauti ya juu.. nikamchukua pale kitandani na kugundua kuwa alikuwa amejikojolea. Tina akataka kumbadilisha nguo nikamsihi awe mtulivu nitafanya mimi kila kitu. Nikambadilisha nguo zake vizuri... Na hapohapo sikutaka kupoteza wakati nikaendelea kuzungumza kilichokuwa kinafuatia. “Sonia mtoto wangu, mama yako ni mwanamke imara sana, nakuombea sana mwanangu hata nikifa leo basi uurithi ujasiri na uimara wa mama yako katika kupigania maisha lakini kamwe usirithi upumbavu wake hata chembe nakuombea sana mwanangu Sonia.....” nilikitazamakile kitoto kikiwa kimetulia kabisa kikiwa kinanitazama. “Najua wewe ni malaika na haya ninayoyasema unanisikia na kuyatunza katika kichwa chako..... Sonia, mama yako ni wa ajabu sana.. alikuwa akiniongopea kuwa anaendfa kwenye mikesha kanisani huko mara kwa mara nikawa nabaki mimi na wewe nyumbani nilikuwa nakubadilisha nguo, nakubembeleza hadi unalala. Akirejea haniulizi nimeweza vipi kukubadilisha nguo, leo hii anataka anisaidie kukubadilisha nguo.. eeh afanye hivyo ili iweje sasa kwa siku ya leo??” nilikiuliza kitoto kile huku nikikitekenya mashavuni, kikacheka kidogo huku kikitupa miguu yake huku na kule. Sasa Tina alikuwa anabubujikwa na machozi na huku kilio cha kwikwi kikimwandama. Sikujihangaisha katika kumbembeleza niliendelea kusema na Sonia. “Mwanangu Sonia, ninakukumbusgha usijekuwa kama mama yako. Yaani kweli unatumia kivuli cha kanisa kunilaghai mimi huku unaenda kwa bwana yako, tena bwana mwenyewe ndo baba yako Sonia. Baba gani sasa huyo? Kama angekuwa baba kweli angekubali vipi kila siku aende kuonana na mama tu halafu wewe anakuacha, eeh! Sonia mimi nd’o baba yako mwanangu...... achana kabisa na huyo tapeli wa mapenzi aliyefanikiwa kumlaghai mama yako hadi akawa mjinga!!!”  Kitoto kilikuwa kimenikazia macho huku kikiendelea kutoa tabasamu lililonipendeza kulitazama na hili lilinipa faraja sana japokuwa hakuwa damu yangu nilimpenda sana Sonia. “Sikia Sonia, eti mama yako akaenda kubeba mimba halafu akajifanya ni ya kwangu, kumbe kuna mjinga mmoja hivi anataka wazae naye eti kisa tu alikuwa mwanaume wake wa kwanza..... samahani sana Sonia nasema maneno mazito sana mbele yako, lakini nafanya hivi kwa sababu naweza nisiipate tena nafasi kama hii ya kusema nawe tena kwqa kirefu kama leo. Halafu nimekutazama Sonia nimekumbuka jambo jingine la muhimu sana lakini hili halikuhusu wewe mwanangu, wewe lala ngoja niseme na mama yako.” Nikamtua Sonia kitandani akabaki kuchezea vidole vya mikono yake, nikamgeukia Tina ambaye aibu kubwa sana zilikuwa zikijionyesha katika uso wake. Ni mtu aliyetamani kukimbia lakini angeenda wapi wakati nimeufunga mlango, huenda alitamani pia dunia ipasuke lakini muujiza huo hauji hovyohovyo... kwa sababu iliishaandikwa kuwa mwisho wa ubaya wowote ule ni aibu!!! ***Ni kipi kingine katika ripoti ya Mujuni Kalisti. Na nini hatma ya ripoti hii na maisha yake ya baadaye yeye na familia yake.. vipi kuhusu Sonia mtoto wa kusingiziwa lakini ambaye anapendwa kwa dhati na baba yake!!!! Usikose kufuatilia sehemu ya sita......    Hello, nimependa na wewe mwenzangu usome hadithi hii nzuri. Utafurahi naamini. Ili usipitwe na hadithi tamu na nzuri nyingi kama hizi, unaweda download Hadithi App kutoka PlayStore kwa kubonyeza hapa: https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni