Jumamosi, 12 Desemba 2015

HADITHI RIPOTI KAMILI SEHEMU YA NNE

SEHEMU YA NNE
Mwanamke anaweza kuwa mama yako, anaweza kuwa mke wako, dada na hata rafiki yako. Lakini ukimpata mwanamke mmoja anayeweza kuwa kama mama yako, mke na pia awe rafiki yako basi usimuache kamwe mwanamke huyu kwa sababu wewe utakuwa ni mmoja kati ya watu wachache waliobahatika kupata bahati katika maana halisi ya bahati!!!
NA HII NI SEHEMU YA NNE...

“Tina kipenzi changu, mwanamke pekee ambaye nakutambua kama mke wangu na dunia nzima inajua hivyo..... mwanamke uliyenifanya hadi leo hii sijui ladha ya sigara, nimesahau mambo ya kijiweni, ni msafi kupindukia. Napenda kukueleza kuwa kabla sijaisoma ripoti hii tambua kuwa nakupenda sana.... maneno haya yamenyooka na sijalazimishwa na mtu. Nakupenda Tina.” Nilisita na kumtazama akiwa anayepoteza amani yake usoni, mikono yake nayo ikimtetemeka.
Nilivuta pumzi huku nikijizuia hali iliyokuwa inamkuta Tina isiweze kunikuta na mimi. Nilizibana pumzi zangu kwa sekunde kadhaa na kisha nikazishusha.......
Naam nikajisikia ahueni, lakini hii haikuwa tiba tossha.
Mpenzi msikilizaji, wataalamu wa mambo wanasema hivi, ikiwa una kitu kinakuumiza moyoni na ukajibana muda mrefu bila kukitoa wajiundia sumu kali mwilini inayokuua polepole.
Kusema kinachokusibu ni mojawapo ya tiba!!
Na huu ulikuwa wakati wa mimi kujitibu!!
Nilimtazama tena Tina wangu usoni na kisha nikakitazama kijitabu changu kidogo.. nikapaona pa kuanzia.
“Tina mke wangu....” nilimuita kwa sauti ya kawaida kabisa.
“Bee!” aliitika huku akijibinyabinya mikono yake.
“Unamkumbuka Yasinta.....” nilimuuliza, akatikisa kichwa kujibu kuwa anamkumbuka.
“Unamkumbuka kwa lipi?” nikajazia swali jingine....
“Mjuni!! Kwanini wanikumbusha juu ya Yasinta angali tumemzika miezi mingi sasa imepita, lakini sijamsahau binamu yangu hadi sasa... kwanini wanifanyia hivi...” alikuwa mkali kiasi fulani wakati ananipa jibu hili.
Sikujali juu ya ukali wake, badala yake niliendelea.
“Ni kweli Yasinta alikufa, sikoseli ilimuua yasinta. Lakini hakufa na kitu kingine ambacho unadhani alikufa nacho Tina, Yasinta hakufa na kipengele kimojawapo katika ripoti hii.....” nilisita nikamtazama usoni tena kisha nikaendelea.
“Nilipata fursa ya kuzungumza na Yasinta kabla hajafariki, lakini hata kabla sijazungumza naye kuna vitu kadhaa niliwahi kuvinukuu enzi za uzima wake... Tina Binamu yako alikuja kuishi nasi akiwa bado binti asiyeujua mji vizuri... ulimfanya ayaone mambo mazito kuliko umri wake... nachelea kusema sio sikoseli tu iliyomlaza Yasinta kaburini hata mambo makubwa aliyohifadhi katika moyo wake yalimfanya azidiwe zaidi. Na laiti kama angepata nafasi ya kunieleza mapema huenda hadi sasa angekuwa hai..... Tina waweza kunilazimisha eti nilifukue kaburi la Yasinta ili aweze kutoa ushahidi lakini haitawezekana kwa sasa wewe tambua kuwa Yasinta hakuweza kuvuta pumzi za mwisho kabla hajanieleza kuwa kuna kipindi ulidanganya kuwa unampeleka hospitali, ukadanganya kuwa amelazwa amezidiwa na wewe utalala huko lakini haikuwa hivyo, punde baada ya Yasinta kupewa madawa uliongozana naye hadi hospitali nyingine isiyokuwa rasmi ambapo sasa mgonjwa ulikuwqa ni wewe ulienda kutibiwa maradhi yako ya mahaba katika chumba kingine. Tina, sina hasira sasa na ninakusihi sana unisikilize tu muda wako wa kusema ukifika utasema.
Hii ya kwenda na Yasinta ukaona haijatosha kunifanya mimi mpumbavu, maskini mtoto wa watu Mungu amrehemu, ukaenda kumlaza sebuleni huko akang’atwa mbu huku akikusikia ukiugulia mahaba katika chumba cha mwanaume mwingine. Naona ulitumia faida ya kuona Yasinta hajazoeana sana na mimi hivyo ukaamua kufanya haya ukiamini kuwa hatakuja kunieleza.
Na si kwa Sinta tu, natambua wazi huyu mtoto aliyelala hapo... sio mara zote eti ulikuwa unampeleka hospitali ama kliniki kama ulivyopenda kusema najua hata yeye ulimtumia kama daraja la kwenda kupata huduma kwa bwana ama mabwana wengine.....” nilisita nikatabasamu na kumuita jina lake ili aendelee kuwa makini.
“Tina!! Unapoamua rasmi kujiunga na timu ya waongo jitahidi kuwaambia hao waongo wakufundishe kuwa na kumbukumbu thabiti... naona walisahau jambo hili kukufundisha.... kliniki uliyokuwa unaenda hukusita kuitaja kila siku ukaniona mimi bwege eti sitajihangaisha kufuatilia... sasa sikia kipande hiki.... kuanzia mwezi wa kwanza wa kwenda kliniki hadi leo hii ninapokusomea hii ripoti kamili uliwahi kuniaga mara kumi na mbili kuwa unaenda hospitali, lakini kiuhalisia baada ya utafiti wangu wa muda mrefu nimegundua kuwa umewahi kwenda mara tano tu Tina!! Hivi hizo mara saba ulikuwa unaenda wapi??? Sihitaji unijibu kwa sasa, ukipenda utanijibu baada ya taarifa hii ikiwa kamilifu.....
Tina! Ujue sigara ilikuwa rafiki wa kweli kwangu, sigara haikuwahi kunisaliti, nikiiwasha inawaka nikiivuta inavutika na nikizima nitaikuta kesho ikiwa palepale nilipoiweka baada ya kuizima. Ukaja Tina ukanilaghai nikaamua kuachana na rafiki huyu wa kweli..... kama hili halitoshi ukanibebesha na mzigo wa usafi. Ndio ni mzigo tu huu kwa sababu sasa nimekuwa mtumwa, nikiona doa kwenye shati nafua, nikiona vumbi nafua!! 
Tina kwa sauti laini ukasema utakuwa sigara kwangu, sigara gani ya kinafiki namna hii... laiti kama sigara zingekuwa kama wewe nadhani wavutaji wote wangeacha kuvuta  mara moja bidhaa hii.
Ewe Tina nikakuamini na kukupatia moyo wangu uufanye unavyotaka leo hii unanipa mtihani huu mgumu kabisa wa kukusomea ripoti hii.
Ujue nimejifikiria siku nyingi sana, sikuwa na ujasiri wa kukusomea ripoti hii lakini leo imebidi tu. Japokuwa naona ni kama ndoto.
Mke wangu Tina, unakumbuka vyema baada ya kujifungua ukanisihi sana nikufungulie biashara kwa sababu ukikaa sana nyumbani unahofia kuvimba miguu.. nikajisemea huyu sasa ndo mwanmamke wa shoka, sikia Tina simaanishi kuwa wewe si mwanamke wa shoka la! Wewe ni mwanamke shupavu haswa na ninakiri mbele yak oleo kuwa mafanikio haya niliyonayo leo ni kwa sababu nipo na wewe, umenipigania sana hakika.
Na hata uliponisihi nikusaidie ufungue biashara zako niliobna ni jambo la heri mno, tazama nikachota akiba yote na kukuanzishia biashara ya nguo, ukasema utakuwa unakopesha watu mtaa kwa mtaa. Na kweli ikawa ukaanza kuwakopesha, awali ilikuwa nguo za wanawake pekee mrtaji ukakua ukaongezea na nguo za wqkibaba.
Hapa ndipo ulipoona kukopesha nguo pekee haitoshi ukalazimika kuanza kuukopesha nma mwili wako, kwangu mimi ukifika unasema umechoka sana lakini kwa wanaokopesheka unawakopesha bila kuchoka.
Najua unashangaa sana kuwa haya yote nimeyajua vipi na kweanini sikukueleza mapema haya ili tuachane, ningeweza kufanya hivyo Tina wangu lakini nilijipa muda wa kuligundua shaka, kulitafutia jibu lake na kisha kukitafuta chanzo.
Shaka nililipata na jibu pia lakini kuna baadhi ya vyanzo sina hadi sasa. Natarajia leo hii utanieleza nini chanzo.......

“Tina hivi unajua nampenda mtoto huyu kwa kiasi gani? Hivi unajua mama yangu anampenda kiasi gani mjukuu wake na vipi kuhusu babu yake.. unawaona wanavyompenda na kumjali mtoto huyu!!!?” akatikisa kichwa kukiri kuwa ni kweli ninayosema.
“Sasa jiulize ni wanaume wangapi hapa duniani wanaweza kupenda watoto wasiokuwa damu yao huku wake zao wakiwa wamewaaminisha kuwa ni damu zao, jiulize kina babu na akina bibi wangapi wanaweza kupenda wajukuu wasiokuwa wao katika maana halisi.” Nikasita na kumtazama Tina akiwa anahaha huku na huku. Mara akashika glasi ya maji ili anywe.
“Kunywa maji Tina kisha nikueleze nilijuaje kuwa huyu si mtoto wangu....”

Naam! Ripoti ndio kwanza ukurasa wa kwanza, anasomewa Tina. Isikilize kwa makini imeambatana na mengi sana ambayo ni somo na funzo kubwa kwako........

Asante!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni