SEHEMU YA KUMI NA SITA WATU hujiaminisha kuwa siku hizi hakuna mapenzi ya kweli na hata ukiwauliza mapenzi ya kweli yalikuwepo lini hawana jibu!! Zaidi watasema enzi za wazee wetu... kana kwamba waliishi enzi hizo na kushuhudia haya!! Tafadhali usiwasikilize hawa, kwa sababu maneno yao ni yale maneno ya wakosaji... penzi la kweli chanzo chake ni wewe.. amua sasa kuzalisha penzi la kweli... usiishi kwa kufuata maneno ya watu. NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA SITA. Looh! Macho yakanitoka gizani, licha ya mabadiliko yote makubwa katika mwili wa mtukanaji yule bado sura yake haikuweza kuyapotea macho yangu. Alikuwa ni Tina! Tina mke wangu, aliyepotea katika uso wangu miezi mingi sana iliyopita tena katika mazingira ya kutatanisha....... Midomo ilijifumba kila nilipojaribu kuifunua, miguu iligoma kupiga hatua yoyote ile mbele. Nilikuwa nimepagawa!!! Nilidhani akifika na kunibaini sura yangu labda naye atapagawa na kuzizima kama mimi lakini ajabu aliniona na ni kama ambaye hakukumbuka lolote, hapo kweli nikakiri kuwa pombe si rafiki mzuri sana hasahasa kama utamuendekeza, Tina niliyekuwa namjua mimi ni yule Tina aliyenikanya juu ya matumizi ya vitu visivyokuwa vya msingi... akaniachisha sigara niliyoizoea, akaniweka katika mstari ulionyooka. Akaapa kuwa kamwe hatakuja kuwa na urafiki na pombe kwa sababu ilimsababishia umaskini mkubwa ulioambatana na fedheha baba yake!! Nami akanisihi nisije nikaingia katika mkumbo huo. Leo hii namshuhudia Tina yuleyule akiwa amelewa chakari, afya yake imezorota sana. “Tina!” nilijaribu kumuita. “Nd’o jina langu unasemaje na wewe hanisi!!” alinibwatukia huku akikishika kiuno chake kana kwamba hapo awali tulikuwa tumegombana. Alipomaliza kunibwatukia akamgeukia dada yake. “sasa wewe nawe ushapewa huo ulemavu bado tu unataka wanaume.. hivi ungekuwa mzima si ungetembea na kila rika wewe..... dada uwe unaona aibu wakati mwingine” Zawadi aliinama chini kwa aibu huku akitikisa kichwa, bila shaka aliamini kuwa Tina anazungumza jambo asilolijua hata kidogo. Baada ya hapo akanyanyua kichwa. “Kaka Mjuni, mzoee tu huyu mdogo wangu.... hajui alitendalo.” Alinieleza kwa sauti ya kinyonge kabisa. Tina akaingilia kati akawa kama mbogo mwenye ghadhabu anatokwa na matusi makali ya nguoni ajabu hakuna aliyejali, bila shaka walikuwa wamemzoea tayari. Majirani walipita na kuendelea na shughuli zao bila kushangaa. Nilimsogelea Tina huku nikishindwa kuamini eti kwa miezi hiyo michache alikuwa amenisahau... au ni mimi nilikuwa nimemfananisha!! Nilijiuliza huku nikizidi kumkaribia. “Vipi kaka, unahamia kwangu ushamalizana na huyo mwenzako au? Naona unataka kula kuku na mayai yake!!” alinihoji. “Tina mimi ni Mujuni... Mujuni Kalisti.....” nilijitambulisha huku nikimkazia macho yangu. “Namfahamu Mjuni mmoja tu.... kuna Mjuni mmoja katika duniani nzima.. wewe labda fotokopi... ehee sawa Mjuni fotokopi nieleze unataka nini?” alinihoji kilevilevi..... “Ni mimi huyo Mjuni unayemfahamu........” nilimsihi na sasa nilimfikia na kumshika mkono wake. Nikautazama ule mkono huku akijaribu kuutoa kwa nguvu, hapo sasa akaanza kulalamika kuwa mimi ni polisi nimekuja kumpeleleza..... sikumuachia badala yake nilikifikia kile kidole ambacho nilimvisha pete siku ya harusi yetu ya kimila. La!haula... ile pete ilikuwa palepale katika kidole kile. Ile kuigusa ile pete nikapatwa na mguso wa aina yake katika moyo wangu!! “Ni mimi niliyekuvalisha pete hii... hakuna mwingine zaidi yangu...” nilimsihi... sasa Zawadi dadake alikuwa amepigwa na butwaa hakudhani hata kidogo kuwa tunaweza kuwa tunafahamiana. “Niache wewe mwanaume, niache wewe ni mzimu.... mzimu jamanii mzimuuu nisaidieni..” alipiga mayowe huku akilazimisha nimuachie. Sasa majirani walianza kututazama kwa makini wakijongea eneo lile. Hapo nikakumbuka jambo moja la mwisho ambalo nilihisi linaweza kusaidia kwa kiasi fulani. Niliukumbuka wimbo fulani wa kizazi kipya ulioimbwa na msanii aitwaye Dito unaoitwa Tushukuru kwa yote. Wimbo huu Tina aliyekuwa kama mimi tu ambao hatukuwa wapenzi wa nyimbo hizo lakini huu alikuwa akiupenda sana na ni yeye pia alinishawishi mimi kuupenda wimbo ule. Niliupenda sio tu kwa sababu Tina aliupenda bali niliupenda kwa sababu kila mstari ulikuwa na maana kubwa katika penzi letu... ni wimbo uliokuwa unatia moyo, unaimarisha penzi na pia kuamsha hisia thabiti...... Nilijikohoza kidogo na kisha nikayafumba macho yangu na kuhamia duniani yangu pekee dunia ambayo nilijiona ninaishi mimi na Tina tu hakuna aliyekuwa anatutazama. Na hapo nikaanza kuimba kama nilivyozoea kumuimbia. “Kwa pamoja tutazame hapa tulipo Anatuonyesha picha ya mbali huko tuendapo Mengi utasikia yakisemwa usiweke moyoni Kuteleza inatokea mambo ya ndani usiyalete hadharani Kama ndege njoo turuke angani woote Nikushike unishike ili tuwe woote! Mvua ikinyesha iwe Baraka ya penzi letu LOLOTE LIKITOKEA BASI TUANGUKE NA TUFE WOTE” Nilimuimbia kipande hicho ambacho na yeye alikuwa akiniimbia mara kwa mara hasahasa nikiwa nimekwazika..... Naam! Hakuna kitu kinaleta kumbukumbu na hisia kali kama nyimbo, msisimko uliompata Tina ulionekana dhahiri baada ya kuwa nimefumbua macho. Tina sasa hakuwa na papara tena bali alilegea na kisha akaangukia magoti, na hapo alianza kuangua kilio kikubwa, sio kilio kwa sababu ya kuongozwa na pombe bali alikuwa akiumizwa na uwepo wangu pale. Alikuwa amekumbuka mbali Tina wangu!! Alinisihi sana niondoke na akiamka pale aichukulie kama ndoto tu, alizungumza mengi sana ya kujutia hakika alisikitisha sana, hata kama una moyo mgumu lazima huruma ingechukua nafasi. Nilibaki kimya nikimsikiliza tu.... huu ulikuwa usiku wa aina yake... sasa watu walianza kujaa na hakuona aibu yoyote ile kuendelea kuzungumza...... Alinieleza kuwa Mungu aliye hai anamuadhibu, sasa hana mbele wala nyuma yupoyupo tu... na alikiri kuwa anaamini kwa zaidi ya asilimia sabini atakuwa ameathirika. “Ni heri nife kwa UKIMWI ili adhabu ikamilike, mimi si mwenye haki hata kidogo Mjuni, mimi ni wa kufa tu na ninastahili yote haya ninayopitia...” alizungumza Tina kwa uchungu mkubwa. Na hapo dada mtu hakuwa na swali, alikuwa ameanza kuupata mwanga. Nilimsihi Tina asiendelee kuzungumza mbele ya watu na nikamuomba niondoke naye. “Hapana Mjuni... hapana utaniua mjuni.....” alikataa. Nikamsihi kuwa mimi ni yuleyule na kamwe sijawahi kubadilika hivyo aniamini. “Maneno yako yataniua mjuni..... yataniua.... niache tu nife kwa UKIMWI!!” alizidi kusihi. Niliona nizungumze naye tena kidogo huenda atanielewa. “Tina, hata mimi nimewahi kufanya makosa mengi sana na nikasamehewa.. hakuna mwanadamu ambaye hajawahi kufanya kosa... wewe ni nani hadi ujipe adhabu kubwa hivi....” nilimuhoji. “Mjuni.... mimi ni mchafu, changudoa, mlevi, sina utu hata kidogo... yule Tina uliyemuoa akakuonyesha mapenzi si huyu wa sasa huyu ni shetani. Niache Mjuni na uende zako.... niliyokufanyia yanatosha....” alinijibu huku akilia...... Kilio cha Tina kiliniumiza sana kwa sababu alikuwa analia akimaanisha na ni kama alikuwa anayeombea nyakati zirejee nyuma. Na haikuwezekana...... Ndugu msikilizaji, ni kweli sikuwa na hisia za kimapenzi na Tina lakini kwa mwanamke niliyeanza naye maisha kuanzia chini, tukapanda hadi juu upendo ule wa kawaida tu usingeweza kufutika. Na hasahasa nilivyomtazama katika hali aliyokuwanayo basi ulikuwa wakati ambao alikuwa ananihitaji zaidi. Nikaendelea kumsihi aongozane nami na hatimaye akakubali, nikachukua ruhusa kwa dada yake na kumuahidi kuwa siku inayofuata nitarejea nikiwa pamoja na Tina. Wakati huo swali kuu lililokuwa linanisumbua ni juu ya Sonia... yupo wapi mtoto yule niliyempenda na swali jingine lilikuwa juu ya sarafina nilitaka kujua ni lini alimzaa mtoto yule na ni nani baba yake!!! ***Naam! Ndugu msikilizaji je? Ndo Ripoti inafikia ukingoni au ndo kwanza inanoga...ni nini hatma ya wawili hawa...... UKWELI HUMWEKA MTU HURU WAHENGA WALISEMA, lakini yapo mazingira ambayo ukiutanguliza ukweli basi unakuwa mwanzo wa kuwa mtumwa...... na ukiuficha huo ukweli unakuangamiza kabisa. Je kipi bora kuwa mtumwa ama kuangamia......
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni