SEHEMU YA NANE Wanawake hulalamika sana karibia katika kila kitu kuwa wanaonewa ama kunyanyaswa. Na wanawake hudai kuwa adui yao wa kwanza kabisa ni mwanaume... lakini hii haipo sawa, adui wa kwanza kabisa anayewanyanyasa wanawake na kuwanyima haki zao ni KUTOJIAMINI. NA HII NI SEHEMU YA NANE. “TINA hadi sasa wewe ni mke wangu kabla ripoti hii haijamalizika lakini sijui itakuwaje baada ya ripoti hii lakini nitapenda kama utakuwa balozi muhimu kwa wanawake wenzako, nenda ukawaeleze kuwa nguvu ya uhakika ya mwanamke ni kujiamini na kosa kubwa kabisa wanalofanya wanawake ni kujifanya wanajiamini wakati hawajiamini. Naamini unaelewa maana ya kujiamini na kujifanya wanajiamini. Na kama haujaelewa nitatumia mfano huu. Mwanamke akiitwa na mwanaume faragha na hana mahusiano yoyote na mwanaume yule na moyo wake ukajipa tahadhari kuwa huenda wito ule si salama. Mwanamke akasema sihitaji tukutane huko nahitaji tukutane sehemu ya wazi huko ni KUJIAMINI. Mwanamke huyohuyo akipata wito kama huohuo, na moyo ukapatwa na mashaka, akaamua kuvaa suruali inayobana akiamini kuwa ndiyo kinga thabiti ya kuepuka lolote litakalotokea huko, huyu anajiafanya anajiamini lakini hajiamini. Na wengi kati yenu mnaangukia daraja la pili, kujifanya mnajiamini huku hamjiamini na huyu ndiye adui yenu mkubwa. Tina nahitaji uwe mtulivu na uamini kuwa haya yametokea kwa sababu maalumu huenda umechaguliwa kuwakomboa wenzako kifikra. Tabia ya wasichana kujifanya wanajiamini ndo ilikukuta Tina mpenzi wangu, halafu kama ilivyo akili ya wenzako wengi wanajifanya kujiamini. Ukaona suluhisho pekee ni kumvulia mwanaume nguo akufanye anavyotaka, sikia Tina kizazi hiki kinateketea kwa kukosa maarifa, ukimkubalia mwanaume kuwa unamvulia nguo ili akutunzie siri basi umeamua mwenyewe kwa hiari yako mwenyewe kurejea zama za utumwa, leo ataonja na kusema hataonja tena lakini kumbuka ile siri haifutiki katika kichwa chake milele. Siku akijisikia tena anakwambia uende, mazoea yanageuka kuwa tabia.. hutaki anavujisha siri zako. Kipi bora, kupatwa na ajali moja kisha ukaamua kuzungumza na mumeo huku ukijutia kilichotokea?? Ama kumficha mumeo na kuendelea kuhudumia wanaume watatu kwa wakati mmoja. Nilikuwa nakuonea huruma sana Tina wangu nilipogundua kuwa sasa unanihudumia mimi, unamuhudumia Steven kijana wetu wa kufuga kuku, pia unamuhudumia yule bwana aliyekupa lifti na kama hiyo haitoshi mume mwenzangu aliyekutoa usichana na yeye alikuwa pale katika foleni akihitaji huduma yako. Tazama jinsi ulivyokuwa umeubeba mzigo mzito..... faida moja mliyonayo wanawake ni kwamba mnaweza kuhudumia sehemu tofautitofauti na uchungu mkaendelea kuutunza nyie pekee bila hawa wahudumiwa kushtuka kama wapo wengi. Maana nyie hamuishiwi vijisababu, na sauti zenu za kubembeleza ni kisu chenye makali ya kutisha. Tina hakuna kiumbe aiyeridhika linapokuja suala la mahusiano kama mwanaume, mwanamke anaweza kuridhika na hata kama hajaridhika kuna ugumu sana wa kutafuta pengine pa kujiridhisha. Tazama mwanaume ni rahisi kupata msichana wa nje kuliko mwanamke kupata bwana mwingine...... Namaanisha kwamba ukimvulia nguo leo kesho atawavua wengine. Ukitoka hapa naomba uyawasilishe haya vyema, waambie wasichana kuwa dawa ya kupendwa sio kujilahisisha!!! Waambie kuwa wewe Tina ulikuwa mke wa mtu na ukajirahisisha kwa bwana wa zamani na mwisho wa siku umekutana na siku mbaya kama hii ya kusomewa ukweli wa mabaya yako yote kipande kwa kipande!!” Nilisita nikavuta pumzi na sasa nikarejea tena katika kijitabu changu kile, lakini jicho langu likimshuhudia Tina akiwa anahema juu juu, sasa machozi yalishakauka na sidhani kama yangeweza kutoka tena. Ndugu msikilizaji usiombe yakakukuta!! Yasikie kwa marafiki ama uyaone katika filamu lakini yasikukute, awali nilisema mke anauma sana, narudia tena na tena mke anauma hasahasa mke wako halali..... “Tina mpenzi wangu unaponyanyua kinywa chako na kumueleza mtu kuwa unampenda kwa moyo wako wote, ni heri uulize kwanza moyo wako sio tu mdomo unajiropokea kwa sababu mwili umepandwa na hulka. Ninajiuliza mpaka leo hivi ni kweli ulivyosema unanipenda ilikuwa kutoka moyoni mwako?” nilimkazima macho na kumruhusu kunijibu. “Na..nilimaanisha kutoka moyoni lakini.....”.... sikutaka kumruhusu aendelee kusimulia, nilimziba mdomo wake na kumweleza kuwa jibu lile lilikuwa limenitosha kabisa. Akatii, nikaendelea kuzungumza. “Asante sana kwa sababu ulinipenda pasipo kulazimishwa na mtu yeyote yule, hili ni jambo la heri sana. Nakumbuka hata siku za awali wakati nazozana nawe kuhusu kunikubalia nilikueleza kuwa sina chochote cha ajabu cha kukufanya wewe uwe nami, nilikuelexza kuwa sina elimu kubwa bali najua kusoma na kuandika, nilikueleza sina mali nyingi lakini kamwe sitaki kubaki katika umasikini kwa sababu nilibarikiwa kuwa na viungo vyote kamilifu, nilikueleza kuwa sishindani na mwanaume yoyote kuhusu kuwa na mvuto bali namshukuru Mungu kwa uumbaji wake aliokusudia kwangu, na mwisho nilikueleza kuwa nina mapenzi yamejaa tele na yapo maalumu kwa ajili yako..... awali ilikuwa ngumu lakini hatimaye ukanikubali huku nikiwa nimekueleza yote kuhusu mimi. Sikuwahi kuongopa kuwa nina milioni kumi benki, sikuwahi hata kukueleza kuwa wazazi wangu ni matajiri niliusema ukweli wote kwa sababu nilihitaji kuishi katika uhalisia mkubwa sana na wewe. Naam! Ukanipokea bila kuwa nimetumia nimetumia uongo wowote. Nikakukabidhi moyo wangu ukanihakikishia kuwa moyo wangu upo sehemu salama kabisa....... lakini Tina. Hii inamaana gani labda, mtu aliyejivua nguo zote mbele zako na kuusma ukweli wote hatimaye unamlipa hivi......tazama sasa hadi leo hii nazungumza nawe ndipo nagundua kuwa mpaka sasa bado unaniongopea.....” nikasita nikafungua pochi yangu na kutoka na karatasi ambayo tangu niitunze katika pochi hiyo sikuwahi kuitoa kamwe hii ilikuwa siku ya kuitoa. Nikaitoa na kuikunjua kidogo kisha nikamrushia Tina katika mapaja yake. “Kama kweli ulinipenda na unadai kuwa unanipenda hadi sasa ni nini hicho Tina.....” Tina aliishika ile karatasi na alipoifungua kidogo tu, akaiachia ghafla kisha akasimama wima na baada ya hapo akajishika eneo lake la moyo na mara akalainika na akawa anaelekea kuanguka chini. Nikawahi kumdaka tukaanguka naye.... Tina akapoteza fahamu huku akiwa anatokwa jasho jingi mno.. Hapo sasa nikalazimika kuiweka ripoti kamili kushoto na nikatilia maanani usalama wa Tina mke wangu...... *Ripoti inazua balaa, Tina kimemsibu nini tena baada ya kuiona karatasi ile..... ni kipi kimeandikwa humo hadi ameshindwa kuhimili na kupoteza fahamu...... Usikose sehemu inayofuata...... Duniani kuna mambo jama!!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni