Jumamosi, 12 Desemba 2015

HADITHI RIPOTI KAMILI SEHEMU YA PILI

SEHEMU YA PILI
Huwa inakera sana pale mtu ambaye anakuita wewe ni rafiki kwake, hakutafuti hadi siku anapopatwa na shida tu nd’o anakumbuka uwepo wako.
Hakika hii inawakera wengi...
Lakini je? Umewahi kujiuliza juu ya mshumaa, umeme unapokatika na hauna mshumaa ndani.. unatembea mita nyingi kwenda kuutafuta ili tu ukusaidie kuleta mwanga??
Je! Unaona ni kiasi gani mshumaa ulivyo kitu cha muhimu katika shida ya mwanga??
Naam! Hivyo hivyo kwako, usijisikie vibaya mtu akija kwako wakati wa shida... wewe ni mtu muhimu sana katika kutatua shida... na usijisikie fadhaa kwa marafiki wa namna hii....

HII NI SEHEMU YA PILI.....

Niliuona usiku mrefu sana, lakini hatimaye palikucha na shemeji akaniaga akaondoka ila alinitia kichefuchefu alipokumbushia lile jambo la kumtumia taarifa tukishajadiliana.
Nilimsindikiza kwa macho, luile umbo ambalo zamani nililiona likiwa zuri kuwa kwake sasa niliona ni mfano wa dudu washa kubwa linalotembea kwa kujikunjakunja likiwa halina umbo linaloeleweka, na kichwa chake kile chenye nywele nzuri za kisasa nilikiona mfano wa mzimu. Kwa kifupi alikera kumtazama...
Tina akanivuta mkono tukaingia ndani.....
Sikutaka tufike chumbani alkini alinisihi, tulipofika akanieleza kuwa anajua wazi kuwa nimechukia mno kwa yote yaliyotokea lakini akaniomba radhi kuwa ni yeye mwenye makosa kwa kumshirikisha dada yake.
“Lakini mume wangu, sikumfikishia taarifa nilimwambia tu... jiandae kuitwa mama mkubwa!! Hivyo tu, sijui yeye hayo aliyoyaleta kayatoa wapi!!” alizungumza nami Tina huku akizikunja na kuzikunjua ndevu zangu, jamani! Tina alikuwa mwabnamke mwenye ushawishi.... na kama wewe hujawahi kupendwa ama kupenda nashindwa hata kukusimulia ni hisia gani huja pale unapojua kuwa unapendwa halafu anayekupenda anakubembembeleza hivi.
Na kama wewe unayeisoma ripoti hii upo katika ndoa, tafadhali shika usemi huu... kama macho yako yanamuona mke ama mumeo anavutia basi piga goti na umshukuru Mungu kwa sababu kuna watu wengi sana wanamuona huyo uliyenaye anavutia na wanatamani kuwa naye lakini tazama unaye wewe na anakupenda!!!
Hii ilikuwa kwangu pia, tulijadiliana na Tina na kwa pamoja tukaamua kumpuuzia dada yake na kile ambacho alikuja kutushauri. Na kisha tukakubaliana kuwa hatutaacha kumjibu kwa sababu hii itamfanya aje kutuuliza bali tutamjibu kuwa tuliamua wawili kuoana na tumeamua wawili kuwa tunataka mtoto na si wakati mwingine bali ni sasa, nia ndo hiyo tunayo na uwezo wa kumlea mtoto tunao tunachoomba ni kudra tu za mwenyezi Mungu tuwe na uwezo pia wa kumpata mtoto.
Nikamuagiza Tina alifikishe jibu lile.
Mimi nikaondoka na kwenda kazini.

Nilirejea saa mbili usiku, nikapokelewa na harufu ya maakuli, mate yakaniruka kooni kwa sababu fujo za Tina nilikuwa nazijua. Na njaa nayo ikaamka....
Nikaingia nikawakuta wakiwa wawili, dada mtu na Tina. Njaa ikakimbia...
Jamani nilikuwa simpendi yule dada yake Tina.....
Stela akasimamana kunisalimia kwa furaha akanipa pole ya kutwa nzima na kisha Tina akanipokea kifurushi changu na kukipeleka chumbani.
Jikoni akamuacha dada yake akiendeleza mapishi, akaniandalia maji ya kuoga, akanipatia na taulo halafu kama ilivyokawaida yake akanisindikiza hadi bafuni.
Mapenzi haya, acha yaitwe mapenzi na ndo maana hata hakuna anayeweza kuelezea nini maana ya mapenzi.
Huduma na ukaribu wake ukaniliwaza, akanisubiri mlangoni hadi nikamaliza kuoga tukaondoka wote akinibebea ndoo.
“Mnapendeza wenyewe looh! Wivu wanishika mie...” stella alitutania tulipompita, nikatioa tabasamu nikapita.

SAA tatu kasoro dakika kadhaa tukiwa tunakula, Stela alituomba radhi kisha akatueleza kuiwa siku ile alikuwa kidogo amelewa na kuvurugwa na mambo yake, akatuomba radhi kwa kuingilia mambo yetu ya ndani sana yasiyokuwa yanamuhusu.
Nikamweleza asijali yeye ni dada kwetu na pia kukosea tumeumbiwa wanadamu.
Akashukuru sana na kisha akaingiza utani wa hapa na pale mwishowe akasema yeye anataka mtoto wa kike, Tina akasema anataka wa kiume mimi nikasema nataka mapacha kabisa.
Tukacheka cheko moja kubwa halafu maakuli yakaendelea kushambuliwa.

Baada ya mwezi mmoja, Tina alikuwa amekamata mimba!!
Ilikuwa furaha tele sana kwetu na hata wazazi wa pande zote mbili walifurahia, walitamani kumbeba mjukuu wao.
Mimba ya Tina ikaja na madeko, nakiri kuwa kuna muda ilikuwa inakera lakini sikuwahi kumwonyesha Tina kuwa nakerwa na hali ile.
Kuna siku anagoma kulala na mimi kitandani, anataka tulale chini, siku nyingine anataka nimpikie ugali na mlenda, nikishaivisha anagoma kul;a anataka nimkaanfgie mayai na niweke chumvi nyingi.
Nikiivisha anakula kidogo anasema ameshiba!!
Ninachoshukuru ni kwamba mwajiri wangu katiika kampuni ile ya pamba alikuwa ni swahiba wangu hivyo hata siku nikichelewa kazini alikuwa ananielewa.
Tina akaendelea na visa vyake na hapa nikaanza kukutana na taarifa mbaya kutoka kwa marafiki na sasa naziunganisha katika ripoti yangu kamili.
Rafiki yangu mmoja aliwahi kunivuta kando na kunieleza kuwa eti aliwahi kumuona dada yake Tina akiingia pale nyumbani kwangu na mama mmoja aliyekuwa na gari kisha yeye akabaki ndani ya nyumba yule mama akatoka na Tina hadi garini.
Akaniuliza iwapo namjua mama huyo, nikamweleza hapana simfahamu mtu yeyote ambaye anamiliki gari na ni rafiki yangu ama ndugu wa Tina.
Yule bwana akaniambia kuwa basi huenda ni rafiki tu!! Akaniacha hivyo..
Lakini hapohapo nikakumbuka kuwa kuna siku ambayo niliwahi kukuta uwanja umefagiliwa jioni katika halui isiyokuwa ya kawaida.
Nikajiuliza inamaana sasa walifagia ili kufuta alama za matairi ya gari?? Na kama ni kweli walifuta ni kitu gani cha siri wanaficha?? 
Nilikosa majibu na kamwe sikumuuliza mke wangu, bali nikaandika katika kitabu changu cha siri, na leo hii nanukuu kutoka katika kitabu changu cha siri na ninakuletea wewe msikilizaji ripoti hii kamili usikilize kisha ujifunze!!!
Mimi yalinitokea lakini kwako iwe darasa huru.

ITAENDELEA!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni