Jumatano, 30 Desemba 2015

HILA NO.9

SEHEMU YA 9 WAKATI Sam anapiga simu ile hewa kuna makundi mawili sehemu mbili tofauti yalikuwa yametulia tuli kusikiliza anachokizungumza Sam, kila kundi lilipagawa katika namna ya kipekee. Kundi moja lilikuwa katika ofisi isiyokuwa rasmi iliyokuwa imejazwa na wanausalama wa taifa wanne. Simu ile iliwapa tumaini na kisha kuwapa swali tena juu ya huyo Tina. Tina ni nani na amechukuliwa na nani, mwanausalama mmoja akamtambua Tina kama mchumba wa Sam. Na pia akazitambua taarifa za kupotea kwake ambazo zilikuwa vituo kadhaa vya polisi. Hilo wakalipuuzia na kutilia maanani juu ya mzigo ambao Sam alikuwa akitarajia kumpa mtu wa kuitwa Masu, kwa jinsi walivyolinasa jina lake katika vinasa sauti. Mkuu wa usalama wa taifa akampendekeza kijana wake mahiri kabisa katika kufuatilia kimyakimya, asiyeogopa kufa na asiyetambua nini maana ya kusamehe!  Yakubu Gama akapewa jukumu hili . Na ni huyu ambaye aliagizwa kutega vinasa sauti katika nyumba ya Sam awali. Gama alifikishiwa taarifa hii akiwa anajiandaa kuandika barua ya kuomba likizo, hivyo wazo la likizo likaishia palepale. KUNDI la pili lilikuwa kundi la Mzee Matata, hawa waliipokea taarifa ile kwa shangwe hasahasa baada ya kusikia juu ya mzigo ambao Sam alikuwa akiumiliki. Ni hili walikuwa wakilitafuta siku zote, na hata uamuzi wa kurudisha vinasa sauti katika nyumba ya Sam ulikuja baada ya kukosekana mtu mwingine wa kumhisi juu ya umiliki wa mzigo ambao walikuwa na mashaka nao tangu awali.  Mzee Matata akafanya tabasamu la ushindi baada ya kupokea taarifa zile, safari hii alikuwa na vijana wapya baada ya wale waliotorokwa na mama lao kuambulia kupigwa risasi na kupoteza maisha. Akawapendekeza vijana wake wawili aliokuwa akiwaamini sana katika suala zima la kupeleleza. John na Johnson ama walivyozoea kuitana ‘PACHA’.  Na hakika walikuwa pacha, wote walikuwa na roho mbaya, wote walikuwa wartefu waliojaa miili yao kimazoezi na kubwa zaidi wote walikuwa hawachoki kuua, inapobidi na wakati mwingine hata isipobidi. Kwao kuua ilikuwa mojawapo ya burudani!! Na ni hawa waliofyatua risasi kuwasambaratisha wale wanyakyusa wawili baada ya kutorokwa na mwanamke wa shoka MAMA LAO. **** HAIKUWA saa mbili usiku kama Sam alivyoongea katika simu hewa. Badala yake ilikuwa saa tano asubuhi, akalipia chumba namba kumi na nane, akaingia katika kile chumba kisha akatoka baada ya kufanya alilopanga kufanya kwa umakini.  Alirejea majira ya saa kumi jioni akiwa amevaa miwani na kofia ya pama huku miguuni akiwa amevaa viatu maarufu kwa jina yeboyebo. Ilikuwa ngumu sana kutambua kuwa yule alikuwa ni Samwel Mbaule.  Akajiweka mahali ambapo angeweza kumwona kila mtu aliyekuwa akiingia na kutoka ndani ya hoteli ile ambayo ilikuwa imejitenga mita kadhaa kutoka barabarani. Nia yake ikiwa kumtambua adui yake ni nani aweze kuanza vita ya kimyakimya. Vita ya kumwokoa Tina iwapo yu hai, na pia kumweka huru mama lao dhidi ya hila aliyofanyiwa na kisha kutangazwa kuwa ni muuaji. Akiwa anakunywa soda yake taratibu, jicho lake liliendelea kuwa makini kabisa kutazama yeyote ambaye ataingia pale na kutoka walau atazame iwapo kuna sura anaweza kuifananisha.  Muda ulizidi kusogea lakini hakuambulia sura yoyote. Akaanza kukata tama huku akihisi mama lao hakuwa na uhakika wowote juu ya watu kuingia katika awamu mbili na kuweka vinasa sauti katika nyumba yake. “Huenda mama lao alikuwa ameghafirika tu!!” Sam alijisemea huku akiimalizia soda yake ili aweze kuondoka na kuingia katika chumba kile alichokilipia. Sam alisimama kinyonge kabisa huku kichwa kikimuuma, alijiona kuwa hana mbinu mbadala za kumjua adui yake kama ambavyo mama lao alimpamba kuwa anaweza kuwa.  Taratibu kabisa akafika mapokezi na kuchukua funguo za chumba chake. Akajiondokea huku akili ikimchemka vibaya mno. Alipoifikia lifti alibaki akijiuliza ni kipi sahihi, kupanda ngazi ili apoteze muda ama apande lifti awahi chumbani bila kuwa na sababu yoyote ya kuwahi? Wakati anajiuliza mara lifti ikafunguka na mtu mmoja akatoka, Sam akafikia maamuzi ya kuingia ndani ya lifti. Akaiamuru imfikishe ghorofa iliyokuwa na chumba chake. Ndani ya sekunde kadhaa mlango ukafunguka kumaanisha kuwa alikuwa amefika eneo stahiki. Taratibu Sam akaanza kuambaa katika korido ili aweze kukifikia chumba chake. Na mara akapatwa mshtuko mkubwa sana baada ya kusikia mlipuko mkubwa, si yeye tu bali wateja takribani wote waliokuwa vyumbani walikurupuka, wengine wakiwa uchi na wengine wakiwa na mavazi ya kulalia. Wanawake kama kawaida yao walikuwa wanalia kwa sauti za bila kujua ni kitu gani kimejiri….. **** Alikuwa ni Yakubu Gama ambaye alikuwa wa kwanza kuingia katika chumba ambacho Sam alikuwa amekilipia kwa ajili ya kukutana na mtu hewa waliyezungumza naye kwenye simu. aliingia katika chumba kile hata kabla Sam hajaingia na kutoka baada ya kukilipia. Hivyo wakati Sam anaingia hakuwa peke yake, Gama alikuwa yu ndani tayari. Waliofuata kuingia katika kile chumba walikuwa ni PACHA kutoka kwa mzee Matata. Alitangulia John kisha Johnson, wakati huo Gama akiwa uvunguni. Nia yake ikiwa ni kutoka katika ficho lile punde baada ya wawili hao walioingia kukabidhiana huo mzigo, aliiweka sawa bastola yake vyema katika kiwambo cha kuzuia sauti. Kisha akaendelea kutulia. Wawili wale ambao aliamini kuwa ni Sam na mwenzake (Masu) hawakuzungumza lolote badala yake walianza kupekua huku na kule kisha mmoja akaingia bafuni na hakutoka huko. Gama akiwa uvunguni akabaki katika mshangao lakini hakupoteza umakini wake, akayakaza macho yake vyema bila kuruhusu mtikisiko wa aina yoyote. Mara yule bwana mmoja aliyebakia akaingiza mikono yake uvunguni na kuanza kupapasa. Gama akawahi kuuondoa mguu wake ambao ungeweza kuguswa na yule bwana….. Baada ya kupapasa mara yule bwana akainama uvunguni. Ebwana! Macho kwa macho na Gama. Gama hakumwachia upenyo maana alijua tayari mambo yameharibika. Gama akafyatua teke, lakini kama ilivyo maaajabu… yule bwana akauondoa uso wake ndani ya nukta chache, Gama akajikuta amebutua teke kitanda. Na palepale akawahi kujitoa uvunguni, lakini kabla hajasimama imara akajikuta akipokea teke kali sana usoni, akayumba lakini hakuanguka akajiweka imara akasimama wima. Ana kwa ana na kipande cha mtu!!! Gama hakuonekana kuwa na mwili wa kimazoezi, alikuwa mnene kiasi na anayeonyesha kuwa legelege, jambo hili lilimzubaisha Johnson. Akamchukulia Gama kuwa ni dhaifu, akamsogelea ili amkwide, lakini akakutana na pigo kali la karate katika shingo yake na kisha ngumi kali katika korodani zake. Yule bwana mkakamavu akajikuta amelainika, hakika alikuwa amekutana na mtu kati ya watu! “Pachaaa…” akapiga kelele za hofu baada ya kuona amezidiwa, na hizi zilikuwa kelele zake za mwisho kabla Gama hajafyatua ngumi kali iliyojikita katika shingo yake na kumtupa chini ambapo hakuwahi kuamka tena milele. Wakati akipambana kuvuta pumzi za mwisho mara chumba kikavamiwa na Johnson, yule pacha ambaye alikuwa bafuni, hakuuliza swali akamvamia Gama kwa papara akamnyuka ngumi mbili tatu za harakaharaka. Gama akajituliza kwa umakini zaidi akamuhesabia hatua Johnson alipojisogeza tena Gama naye akafyatuka na kuanguka naye chini mzimamzima. Akamkaba shingo kwa uimara kisha akamuuliza juu ya wapi ulipo mkanda. Johnson hakujibu chochote kwa sababu alikuwa amepigwa kabali, Gama akalitambua hilo, upesi akamwachia na katika nukta iliyofuata akampiga ngumi nzito kwenye taya. Johnson akajiharishia!! Na hapo akakiri kuwa alikuwa anapambana na kiumbe wa ajabu kupita wote aliowahi kukutana nao katika maisha yake. “Ni nani alimuua Steven?, Tina ni nani?, na mkanda upo wapi… “ “Sijui lolote mkuu, nimeagizwa tu…” alijibu huku akigumia kwa maumivu makali. “Jina la aliyekuagiza.. upesi kabla sijainyonga shingo yako bwana mdogo…..” akatoa karipio kali Gama. Macho yake yakiwa mekundu na mikono ikiwa na tamaa kali ya kuua!! “BVB”  “BVB ni nini maana yake.. upesi….” Alihoji huku akiikaza shingo ya yule bwana.  Hilo likawa swali la mwisho kabisa kuuliza kabla yule bwana hajafanya kitendo cha ajabu, akaanza kujinyonga nyonga kama anayeugulia tumbo. Na mara mlipuko mkubwa ukasikika. Hapo ndipo kilipozuka kizaazaa!! Gama akarushwa mbali kabisa na mlipuko ule. Mlipuko ambao hakuutegemea katika mazingira yale! Mlipuko ule ukawavuta watu waliokuwa nje na ndani ya hoteli ile akiwamo Sam.  Na hakuwa Sam pekee bali askari kanzu wapatao kumi waliomsindikiza Yakubu Gama wakaingia kazini. Kwa papara kama kawaida yao!!  Utawajua tu kwa amri zao. Wakatapakaa huku na kule, raia nao wakakimbilia eneo la tukio, Sam akaongoza mbio hizo akawa mmoja kati ya watu waliowahi kuwasili eneo la tukio. Macho yake yakakutana na mwili wa Yakubu Gama katika chumba chake. Sura na umbo havikuwa vigeni kabisa katika macho yake. Sam alijiuliza ni wapi aliwahi kumwona kiumbe yule, akaituliza akili na kujikuta akimkumbuka. Alikuwa ni yule mwanaume aliyekuja kumwekea dhamana na kisha kumsihi awe makini. Dhamana ya maajabu ya usiku mnene sana. Inakuwaje bwana huyo katika chumba chake? Ilistaajabisha. Na hapo akajipongeza kwa kujisajili kwa jina lisilokuwa lake wakati anaingia hotelini hapo. Kwani kwa tukio lile tayari ni kizaazaa kipya. Sam akazidi kutambua kuwa lipo jambo ambalo limetanda katika mkasa wa kifo cha Steven Marashi na hata baba yake mzazi. Kichwani akajiwekea picha kuwa kuna pande zaidi ya moja zinawania mkanda ambao alikuwa anaumiliki! Pande hizo ni zipi? Alijiuliza bila kupata jawabu!! Katika purukushani za hapa na pale kabla polisi hawajaweka utando wao wa kuzuia raia kuingia ndani ya kile chumba, Sam alifanikiwa kukitoa kinasa sauti chake ambacho alikiweka baada ya kuingia katika chumba kile na kutoka majira ya saa tano. Kilikuwa kimewekwa katika godoro ambalo alikuwa amelichana na kisha kukitandika kitanda vyema. Sam alizuga kuwa amesukumwa, akaangukia pale na kwa sekunde chache akaondoka na kile kifaa. Wakati anaondoka alipishana na yule mwanadada aliyemwandikisha kuingia katika chumba kile. Yule dada bado hakuwa na uhakika kama yu sahihi ama la. Sam mwenye hofu akajikaza akaongeza mwendo. “We kaka…” yule dada akajaribu kuita. Sam hakugeuka. “Ni yeye jamani…”  sauti ikasikika kama akiwaambia watu fulani. Sam akawa ameifikia kona, akaanza kukimbia, akakata mitaa hapa na pale hadi akatokea Ubungo. Jasho lilikuwa linamtoka haswa. ***  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni