Alhamisi, 24 Desemba 2015

HILA NO.5

SEHEMU YA TANO BODABODA ilisimama jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Sam. Malipo aliyafanya awali kabisa walipokuwa kituo cha mafuta. Hivyo Sam hakuwa na la kupoteza zaidi ya kuagana na yule dereva bila kutilia maanani lile agano la usiku mwema alilopewa na yule bwana ambaye tayari alikuwa ameitia moto pikipiki yake. Kichwa cha Sam kilikuwa katika maumivu makali sana kutokana na mawazo mengi na pia mizunguko mingi aliyokumbana nayo siku hiyo na mbaya zaidi hakuwa amepata mafanikio yoyote. Tina wake hakujulikana alipo hadi wakati huo na simu yake iliyopigwa kutoka fukwe za koko hakujua ni nani aliifikisha huko na kwa sababu zipi. Mwendo wa mita mia mbili aliouzoea kutoka barabarani hadi nyumbani kwake aliuona mrefu sana siku ile tofauti na siku nyingine. Alijivuta hivyohivyo akiambaa katika njia ndogo ambayo alizoea kupita kila siku……. Hatimaye akaufikia mlango wake, akauchukua funguo mahali pake ambapo huwa anauhifadhi kila siku. Akafungua mlango na kuingia ndani. Akakiendea kitufe cha kuwashia taa.. akajaribu kuwasha lakini haikuwaka. “Aaargh! Luku imeisha tena?” alisononeka Sam huku akitupa kibegi chake kidogo bila kujali ni wapi kitatua. Akajipekua na kuitoa simu aliyokuwa nayo akaiwasha na kuanza kuangaza huku na kule. Chumba kilikuwa shaghalabaghala katika namna ambayo hakukiacha asubuhi alipoondoka kwenda kwa mama mkwe wake. Alipoangaza dirishani akashangaa na akili yake ikafunguka kuwa nyumba ya jirani ambayo walikuwa wanatumia LUKU moja umeme ulikuwa unawaka. “Hah! Mbona……. Mbona kwa mama Sarah unawake sasa….” Alijiuliza kwa sauti ya juu iliyoonyesha kukereka waziwazi. “Au kuna shoti?.... lakini mbona nyumba nayo ipo hovyo…nani ameingia humu ndani……” alijiuliza tena lakini safari alikuwa anahisi kama anaishiwa nguvu katika mwili wake, akaisikia ile simu ikiwa nzito, ikaanguka chini kisha na yeye mwenyewe akalegea na kuanguka chini.  Sam akatambua kuwa alikuwa alikuwa amenusa madawa makali ya kuleta usingizi ndani ya kile chumba. Akajikaza asiweze kusinzia akapapasa na kuikamata simu yake, akabofya kitufe cha kupigia akakutana na namba ya mama mkwe wake. Akajaribu kubofya lakini mkono ukawa mzito akaishia tu kuitazama simu yake. Mwisho akasinzia…… Fahamu zikamtoka!!! *** Katika mitaa flani nchini Tanzania, jopo la watu wanne lilikuwa katika chumba cha siri kwa siku nzima wakifuatilia kwa ukaribu kabisa kila neno ambalo vinasa sauti vilivyotegwa katika chumba cha Sam maeneo ya Yombo wilayani Temeke.  Usiku huu umakini uliongezeka zaidi baada ya kuanza kusikia purukushani za mlango kufunguliwa. Walitambua kuwa ulikuwa ni muda wa Sam kurejea nyumbani. Na huo nd’o huo wakati waliokuwa wakiusubiri kwa hamu kubwa ili watambue iwapo machale yao yamewacheza kwa mtu sahihi ama la! Nyaya za umeme zilikuwa zimetibuliwa maksudi ili Sam akigundua kuwa nyumba yake imeingiliwa na watu basi aanze kuhaha kutafuta kitu ambacho hata wao walikuwa hawajawahi kukiona lakini waliamini kuwa anaweza kuwa anahusika ama anaweza kuwa nacho. Ajabu Sam hakuonekana kushtushwa sana na wala hakutafuta chochote walichodhani kuwa anaweza kukitafuta. Madawa ya kulevya yalikuwa yanaanza kufanya kazi dakika kumi na tano baada ya kuvutwa na muhusika. Muda huu kwa upande wao ulikuwa sahihi kabisa iwapo hatajihangaisha kukitafuta basi huenda atakuwanacho mfukoni ama popote ambapo anaweza kuwa alikihifadhi na kutembea nacho. Hivyo atakapopoteza fahamu zake basi wataingia na kumpekua huku na kule ili kujihakikishia. Naam! Kama walivyokuwa wamepanga….. Sam akapoteza fahamu, vijana wawili wakakamavu wakaingia upesi ndani ya kile chumba na kumgeuza Sam wakiwa wamevaa mipira maalumu mikononi ili wasiweze kuacha alama zozote ndani ya chumba kile.  Tochi zao zikaangaza vyema wakati Sam asiyejitambua akiwa anapekuliwa kila kona. Kibegi chake nacho kikapekuliwa kwa umakini bila kufanikiwa kupata chochote ambacho kingeweza kuwasaidia katika upelelezi wao wa kitu wasichokuwa na uhakika nacho. Hatimaye wakaambulia sifuri!! Wakamuacha Sam pale chini wakaangaza chumba kwa makini tena. Kisha wakatoweka baada ya kurekebisha kile walichotengua!! **** Baridi kali ya sakafu majira ya saa kumi na moja alfajiri ilimzindua Sam kutoka alipokuwa amelala. Taa zote zilikuwa zinawaka kuanzia sebuleni hadi chumbani. Sam akainuka na kuketi kitako, akili yake ikaanza kufanya kazi akakumbuka mambo kadhaa yaliyotokea na kumfanya alale pale chini. Sam akageuka na kuitazama simu yake, ilikuwa palepale pembeni yake, na jina lililokuwa katika kioo lilikuwa la mama mkwe wake. Akakumbuka kuwa kabla hajakumbwa na usingizi mzito alitaka kumpigia mama mkwe wake lakini hakufanikiwa. Ni akina nani hawa na wanataka nini? Sam alijiuliza huku akisimama wima. Wakaukata umeme na sasa wameurejesha!! Wapuuzi kweli na pia ni waoga wa kutupwa! Alijisemea Sam huku akifanya tabasamu hafifu la kejeli. Ule ubaradhuli na ubabe aliouvuna wakati anapitia mafunzo ya JKT ulijijenga katika mwili wake na akili yake. Akawapuuzia maadui zake na kuwaona kuwa walikuwa na mioyo ya kike. “Kama kweli wanaume waje tena bila mbinu za kishamba kama hizi…” alimalizia kwa kutoa tusi zito la nguoni asijue amemtusi nani. Kisha akaliendea jokofu na kunywa maji glasi mbili….. Hakutaka kukaa akabaki amesimama vilevile akifikiria matukio hayo na kukosa maana yake. “Halafu mama alimzuia Tina kufanya nini?... haiwezekani iwe kirahisi rahisi tu eti alimzuia kujhichanganya na watu maarufu ama vionginevyo… lazima kuja jambo la ziada ambalo amelificha….. asubuhi na mapema naamkia nyumbani kwake haya mambo ya wanawake kufichiana siri yanaweza kugharimu maisha ya Tina…..” alisita kidogo baada ya kutambua kuwa Tina anaweza kupoteza uhai kizembe, uzembe wa mama mkwe wake kuficha siri. Hali ya kutambua kuwa Tina anaweza kupoteza uhai kizembe ilimtia katika uoga. Lakini mara akatishika zaidi baada ya kutanabai kwamba sio Tina pekee ambaye anaweza kupoteza uhai, bali hata yeye mwenyewe angeweza kuwa amekufa tayari kwa sababu walifanikiwa kumzimisha kwa masaa kadhaa akiwa hajitambui kabisa na hajui ni kitu gani wamefanya akiwa hajitambui. Jamaa ni hatari hawa aisee!! Alijisemea Sam huku uoga ukimwingia na ule ukakamavu na kiburi cha awali kikipotelea mbali. Hali ya hatari ikatawala, mbaya zaidi wanaomletea hatari hakuwa akiwafahamu na hakuijua sababu ya wao kumletea kashkashi hiyo. Uwepo wake katika hali ya uhuru alitambua wazi ni kwa sababu wawindaji walikuwa wakitaka kuendelea kumtumia. Sam akajiapiza kuwa makini katika kila hatua ambayo atakuwa anapitia. Zilipita dakika zaidi ya arobaini Sam akiwa amesimama wima mbele ya jokofu lake akifikiri hili na lile. Hatimaye akafikia hatua ya kuondoka wakati uleule kuelekea kwa mama mkwe wake, hakuiona haja ya kuendelea kupoteza muda. Akafanya maandalizi mepesi na kutwaa kibegi chake. Akaufunga mlango na kutoweka kuelekea barabarani ambapo angeweza kupata pikipiki ya kumfikisha nyumbani kwa mama mkwe wake. Hakupoteza muda sana barabarani kabla pikipiki haijapita, akapunga mkono nayo ikasimama. Akakwea huku akitoa maelekezo ya wapi alipokuwa anaelekea… akafanya malipo kabisa. Baada ya dakika arobaini na tano alikuwa Kinondoni jirani kabisa na nyumba aliyokuwa akiishi mama mkwe wake. Utulivu uliokuwa eneo lile ulimshangaza na kumfanya afikirie kuwa yawezekana kuwa hapakuwa na umeme ama la kuna tatizo jingine jipya. Haikuwa kawaida hata kidogo katika eneo lile kuwa na utulivu mkubwa kiasi kile. Hakutaka kujishughulisha na hisia zake binafsi bali aliamua kuufuata ukweli, na hapakuwa na namna nyingine zaidi ya kuonana na mama mkwe wake. Aligonga mlango mara mbili, ukafunguliwa na mtoto mdogo ambaye alizoea kuitana naye kwa jina la ‘anko’. “Bibi yupo?” alimuuliza moja kwa moja akimaanisha mama mkwe wake. “Aliondoka na shangazi tangu jana….. na hawajarudi. Ila shangazi amerudi halafu ameondoka amesema anaenda polisi…” alijibu yule mtoto huku akijifinyanga macho yake kupambana na usingizi. “Polisi? Kuna nini kwani anko….au…au ngoja….” Alijiumauma Sam akigundua ameuliza swali kwa mtoto ambaye hawezi kumjibu kiufasaha.  Akajongea nyumba ya pili akagonga mlango mara kadhaa, mlango ukafunguliwa na mama mtu mzima ambaye Sam alimfahamu pia. Hakuonekana aliyetoka kulala, manukato makali yalizisabahi pua za Sam “Shkamoo mama mkwe…..” alimsalimia na kumwita jina walilozoeana naye… yule mama akabaki katika bumbuwazi kwa sekunde kadhaa kabla ya kuijibu ile salamu na kisha kuzungumza jambo ambalo lilishtua akili ya Sam. “Bora hata angeugua tujue moja…… kweli mama Tina anakufa hata Tina hajajulikana alipo jamani…Mungu weee!! Mbona majanga mfululizo haya anatupatia waja wake sisi…..” Sam alitaka kuuliza kitu palepale lakini mdomo ukawa mzito kabisa kufunguka. Akabaki kukodoa macho yake akimtazama yule mwanamke mnene aliyesimama mlangoni. “Sam!” yule mama alimuita. Na hapo akili ya Sam ikarejea katika ufahamu wa kawaida tena!! “umesema mama amekufa?” Sam aliuliza kwa utulivu. “He! Mi nikajua wamekupigia simu……” Sam hakuweza kuhimili shinikizo lililomkumba ghafla. Akajikuta anaanguka chini na kisha akatulia tuli. Yule mama akapiga mayowe ya kuomba msaada!! Lakini kabla hajapiga kelele zaidi alinyamazishwa na wanaume wawili waliokuwa wameshika silaha za moto mikononi mwao. Kila mmoja akiwa na bunduki yake! Yule mama akatulia kimya huku akitetemeka!! Ilikuwa ni kitendo cha sekunde kadhaa, wanaume wale wenye miili iliyojengeka kimazoezi walimwinua Sam na kisha wakatokomea naye kuelekea walipopajua wao. Wanaume hawa ni walewale waliokuwa ndani ya chumba cha Sam usiku ule!! Wakikitafuta kitu ambacho hawana uhakika kama Sam anaweza kuwanacho ama hana…… Wakikitafuta kitu wasichokijua! Utata!!! ***** Asubuhi iling’ara katika namna ya kipekee!! MAGAZETI ya udaku nay ale yasiyokuwa na udakju yalibebwa na vichwa vikubwa vya habari, huku kila gazeti likiwa na picha ya marehemu Steven Marashi.  Kila gazeti lilijaribu kuipamba habari hii aidha kidaku zaidi ama kwa utafiti hafifu, machache sana yaliweza kuelezea kiuyakinifu!! Kama ingekuwepo takwimu ya jinsi magazeti yanavyouzika kwa siku moja basi hii ilikuwa asubuhi ya kukumbukwa kwa muda mrefu sana ikiipiku ile siku ambayo hayati baba wa Taifa alipoaga dunia. Hata wale wavivu wa kusoma na wao walinunua magazeti huku kila mmoja akionekana kuupokea msiba ule katika namna ya msiba wa kitaifa. Naam! Msiba wa kitaifa, Steven Marashi alijulikana kwa taifa zima. Si kila mtanzania aliyeweza kuyasoma magazeti haya mapema ama kuisikiliza taarifa hiyo gazetini. Kuna wale ambao hawakuisoma kwa sababu walikuwa wamelala. Mmoja wao alikuwa ni Samwel Mbaule ‘Sam’. Huyu alikuwa amelala usingizi nasaba ya kifo wakati wale jamaa wawili wakakamavu wakipitia magazeti lukuki waliyoyanunua. “Shit! Ona hawa wajinga wanasema Lili nd’o amemuua kwa sababu za kishirikina….” Jamaa mmoja alilalamika huku akibamiza kiti upande wa nyuma wa kiti kilichokuwa mbele yake. Mwenzake alicheka kabla hajamsomea na yeye alichokiona, “kuna hawa wapuuzi wameandika tena kuhusu Lili………oooh! My God!! Hii picha wameitoa wapi sasa?” alihamanika ghafla baada ya kukutana na picha. Steven Marashi akiwa amekumbatiana na Lulu kimahaba….. “KUMBE LILI ALIKUWA SHEMEJI NA WIFI WA TAIFA!”  Kichwa cha habari kilikejeli!! Upesi baada ya kuiona picha ile walinyanyua simu na kupiga namba ambayo ilipokelewa katika kile chumba cha siri ambacho kipo mahali flani nchini Tanzania. Aliyepokea taarifa ile alitweta kwa hofu, akakosa kauli akalazimika kukata simu bila kutoa muafaka wa nini kifanyike. Simu yake iliita tena, akaitazama na kupokea. Alikuwa ni mtu yuleyule. “Mkuu kuna kila dalili kuwa kuna kiumbe yupo hai na anafahamu siri nyingi sana za marehemu. Na kama akiendelea kuwa hai basi atatufikisha katika hatua mbaya sana ambayo hatutakiwi kufika…..” “Atafutwe mara moja na ninamuhitaji ndani ya siku mbili, nasema namuhitaji kabla hatujaruhusu mwili wa Steve kuingizwa kaburini. Sipo tayari tudhalilike makaburini, ni heri tetesi za magazetini na pale msibani kuliko fedheha msibani….” Sauti kutoka upande wa pili ilizungumza kiamri na kisha simu ikakatwa bila kupokea majibu yoyote kutoka upande wa pili. Jamaa alipokata simu ile, alimtazama Sam aliyekuwa amepoteza fahamu, akajiuliza wana haja gani naye mtu yule ambaye hakutakiwa kuuwawa kwa namna yoyote kabla hajawapa kitu wasichokitambua. Alipiga kite cha ghadhabu kisha akazungumza maneno machache kwa sauti ya chini kabla hajamnasa kofi kali Sam asiyejitambua. Akamtukania mama yake mzazi na matusi mengine kedekede! Ni kama alikuwa anajitukana mwenyewe! Sam hakusikia lolote. **

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni