Jumatatu, 14 Desemba 2015

RIPOTI KAMILI SEHEMU YA 15

SEHEMU YA KUMI NA TANO JIJINI Dar es salaam ni biashara iliyozoeleka kabisa ya vijana kuokota makopo tupu ambayo awali yalikuwa yametumika kuhifadhi maji ama vinywaji vingine baridi. Makopo haya tupu huuzwa kwa wanunuzi wa jumla ambao nao huyauza viwandani. Hivyo shughuli za misiba, harusi na sherehe nyingine jijini Dar es salaam huzungukwa na vijana ama yeyote yule ambaye anafanya biashara hii. Wahudhuriaji mkinywa maji na kutupa makopo wao wanaokota.          Hata katika msiba huu walikuwepo pia watu wa biashara hii ya makopo tupu! Ubaya wa jiji la dare s salaam, mtoto ni yule ambaye asubuhi akiamka anamsalimia mama yake na baba yake, anakula walichoamua wazazi na mchana hivyohivyo na usiku analala nyumbani. Lakini ikiwa kinyume na hapo umri wako haumaanishi wewe ni mtoto katika jiji hilo. Unaweza kuwa na miaka kumi na sita lakini kitendo cha kujitafutia kula yako basi wewe si mtoto tena, na hivi ndivyo nilivyoshuhudia katika hili pia. Watoto wadogo walikuwa wanagombania yale makopo tupu ya maji, ilikuwa inastaajabisha sana walivyokuwa wakipeana matusi ya nguoni na ikibidi kupigana kabisa. Ajabu sasa ni watu wazima wachache sana waliojali magomvi haya na kuwakanya lakini wengi walikuwa kama waliokuwa wamezoea. Kuna wakati nilitupa kopo la maji kwa madhumuni liokotwe na mtoto mmoja ambaye alikuwa na umbile dogo kuliko wenzake na alionekana mpole sana kwa tabia, ile anataka kuliokota lile kopo akawahi mtoto mwenzake na kumkwapua. Ile anajaribu kujitetea nikashuhudia jinsi mwenzake alivyomtwanga ngumi ya mgongo bila kujali.  Yule mtoto akaanza kulia huku akilaani kitendo kile. Nilijisikia vibaya sana na ninahisi nilipewa damu ya kupenda watoto japokuwa hadi wakati huyo sikujaliwa kabisa kupata wangu mwenyewe. Nilimsogelea yule mtoto na kumuita akasogea huku akifuta machozi yake, nguo yaqike chakavu iliyaruhusu macho yangu kuona idadi ya mbavu zake kwa jinsi alivyokuwa amekondeana. Nilimuuliza jina lake akanieleza kuwa anaitwa Bahati. Nikamuuliza maswali ya hapa na pale, akawa ananijibu kiufasaha nikamuuliza ni kwanini na utoto wake wote ule yupo mtaani anaokota makopo. Akanieleza kuwa anamsaidia mama yake ambaye hajiwezi kwa sababu ni mlemavu. Nilijiskia vibaya sana, nikakipa maji ili kinawe uso wake uliojichora michirizi ya machozi. Baada ya kunawa ndipo nikaanza kuona kitu ambacho kilikuwa kinanikumbusha mbali sana,niliiona kwa mbali sana sura ya Tina katika uso wa mtoto yuole ambaye alinieleza kuwa anayo miaka tisa. Nilimuuliza iwapo mama yake anaitwa Christina akasema hapana mama yake anaitwa Zawadi.  Nilijiuliza je yawezekana nimemsahau Christina hadi naifananisha sura ya mtoto huyu na yake ama ni vipi? Nikakosa jibu.... Lakini ndugu msikilizaji napenda kukusihi kitu kimoja, jifunze kuziheshimu sana hisia zako ziheshimu kwa sababu kuna wakati unaweza kuzipuuzia na kujikuta umepoteza mambo mengi sana. Hisia zangu zisizokuwa na ushahidi zilinituma kwenda kumjua mama yake kile kitoto. Na hii ilikuwa sababu ya mimi kushindwa kwenda makaburini kwa sababu ningeweza kwenda na kisha kumpoteza mtoto huyu aliyenikumbusha kuhusu mtu aliyewahi kuwa wa muhimu sana katika maisha yangu. Nilimuuliza mtoto yule kama akipata mtu wa kumsomesha atakuwa tayari kwenda shule akasema hata kama ni dakika hiyohiyo yupo tayari. Nilivutiwa sana na mtazamo wake juu ya elimu, na hapo nikakumbuka kumuuliza jina lake akaniambia jina lake ni Sarafina. Niliongozana naye kuelekea nyumbani kwao, palikuwa mbali sana lakini yeye alikuja kwa miguu kwa sababu hakuwa na namna nyingine. Majira ya saa kumi na mbili tulifika nyumbani kwao na kile kitoto, na kweli ile kufika tukamuona kwa mbali kabisa mwanamke akiwa ameketi chini. “Mama yuleee!” kikanieleza huku kikinyoosha mkono wake kuelekea alipokuwa yule mama. Nilifika na kumsalimia mama yule na kumpa pole, akaniuliza majina yangu nikajitambulisha naye akanieleza kuwa anaitwa zawadi. Nilizungumza naye juu ya maisha na nikamueleza kuwa nimempenda sana mtoto wake na sijapendezwa kumuona akihyangaika mitaani, Zawadi akanieleza kuwa hana namna kwa sababu yeye ni mlemavu na hana msaada zaidi hivyo ameshindwa kumpeleka shule sarafina. Baada ya kuzungumza mengi nikamuulizia baba wa yule mtoto ikiwa bado yupo hai. Zawadi akanijibu kuwa baba wa mtoto yupo hai lakini ndo hivyo hujitokeza mara moja moja sana siku akijisikia kuleta unga analeta na siku akiamua kukaa kimya anakaa hata miezi mitatu bila kusema lolote. Zawadi alinieleza kuwa ana mengi sana yanamsibu lakini mtoto yule ni mzigo zaidi kwake kwa sababu anamuumiza sana anapolala njaa ama anapomuulizia babayake. “Zawadi unadhani kwa nini mzazi mwenzako hamjali mtoto wake, kwanini usilipeleke hili suala ustawi wa jamii...” nilimuuliza kiutulivu. Akashusha pumzi kwqa nguvu sana na kisha akaniambia. “Ndugu yangu, ni heri basi angekuwa mtoto wangu ningeshikia bango mambo kama hayo, mama yake mwenyewe ni kama aliyeridhika na hali hii...” alinijibu huku akijilazimisha kutabasamu. “Unamaanisha kuwa Sarafina sio mtoto wako au?” nilihoji. Akatabasamu kisha akatikisa kichwa kuashiria kukubali lakini akanisihi sana yule mtoto asijue kwa sababu anajua yeye ndiye mama yake. Nikaulizia ni wapi alipo mama yake, akanieleza kuwa mama yake si mkaaji sana ni mrukaji rukaji, leo anaruka huko mara leo hapa. Akanieleza kuwa mamam yake Sarafina ni mdogo wake wa damu. “Leo alisema atakuja kumletea Sarafina nguo....sijui kama atakuja maana yeye na baba mtoto hawana tofauti linapokuja suala la kuahidi na kutotimiza ahadi..” alinijibu kinyonge. Nilimuonea huruma sana mama yule, ulemavu wake na mzigo huu nao wake. Wamiliki halali hawajali kitu!! Majira ya saa tatu usiku na dakika kadhaa hivi nilimuaga mama yule na kumsihi atamuaga Sarafina ambaye alikuwa amelala tayari. Nikajipekua mfukoni na kutoka na notimbili za shilingi elfu kumi na kumkabidhi, alinishukuru sana nikamwambia asijali sana na nitakuwa namkuja mara kwa mara kumtazama yeye na Christina. Neno moja nililomwambia ni kwamba, sikujaliwa kuwa tajiri sana lakini nayafanya yote hayo kwa sababu moyo wangu unanituma kufanya hivyo!! Nikamsihi sana asimruhusu Sarafina kwenda kuokota makopo kwani ni hatari sanakwa mtoto wa kike hasahasa wa makamo yale. Akanikubalia!! Nikaanza kupiga hatua kutoka eneo lile nikaisikia sauti kwa mbali ikiita jina la sarafina kwa fujo. Nilipogeuka yule mama akanieleza kuwa mama yake sarafina huyo amerudi!!! “Sasa mbona anamuamsha mtoto!” nilihoji huku nikipiga hatua kadhaa nyuma. “Kawaida yake huyo hapo amelewa atamuamsha atamsumbua wee hadi pombe zitakaposema imetosha!!” alinijibu huku akitabasamu. Na mara alianza kumuita mama yake sarafina. “Wewe mwanamke, hebu muache mtoto wangu amelala mbona unakuwa hivyo lakini Tina??” aliita kwa sauti ya juu katika namna ya kulalamika. Ile kuita jina hilo nilipatwa na shoti kali katika mwili wangu, mapigo ya moyo yalienda kasi sana huku nikijiuliza nitazoea lini jina lile. “Zaa wako ndo unipangie sheria...” sauti ya kilevi ya mwanamke ilijibu kutoka ndani... kisha matusi mazito yakaanza kuporomoshwa huku mtukanaji akizidi kusogea nje. Hatimaye akafika nje alipokuwa ameketi Zawadi. Looh! Macho yakanitoka gizani, licha ya mabadiliko yote makubwa katika mwili wa mtukanaji yule bado sura yake haikuweza kuyapotea macho yangu. Alikuwa ni Tina! Tina mke wangu, aliyepotea katika uso wangu miezi mingi sana iliyopita tena katika mazingira ya kutatanisha....... Midomo ilijifumba kila nilipojaribu kuifunua, miguu iligoma kupiga hatua yoyote ile mbele. Nilikuwa nimepagawa!!! Hello, nimependa na wewe mwenzangu usome hadithi hii nzuri. Utafurahi naamini. Ili usipitwe na hadithi tamu na nzuri nyingi kama hizi, unaweda download Hadithi App kutoka PlayStore kwa kubonyeza hapa: https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni