Jumatatu, 14 Desemba 2015

HADITHI RIPOTI KAMILI SEHEMU YA 12

SEHEMU YA KUMI NA MBILI MAAMUZI ni jambo ambalo huamua kesho yetu wanadamu. Kuna maamuzi ambayo huwa tunafanya huku tukiamini fika kuwa ni sahihi lakini kesho yake tunajikuta katika wakati mgumu wa kujutia maamuzi...... NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA MBILI. Kweli tulienda hadi huko aliposema ni kwa rafiki yake mkubwa  Tina lakini bado hatukufanikiwa kuambulia jambo lolote lile rafiki alikuwepo lakini hakuwa na taarifa zozote juu ya Tina. Kufikia hapo nikaamini kuwa Eric hakuwa akifahamu lolote juu ya wapi Tina yupo....  Sikuwa na haja ya kuyaendeleza mambo haya, niliachana nayo baada ya kuzungumza na mama yake Tina juu ya kilichotokea niliwaeleza mangapi niliyovumilia, walinishangaa sana nilivyowasimulia mkasa huu wa aina yake lakini hakika nilikuwa sijaongeza hata chembe ya uongo. Ulikuwa ni ukweli mtupu...... Baba yake Tina alinikumbatia kwa nguvu sana na kunieleza kuwa mimi ni mwanaume wa aina yake, laiti kama angekuwa ni yeye huenda angekuwa jela zamani na angekuwa amezoea hukumu ya kifungo cha maisha ambayo angekuwa amepewa. Niliwaeleza wakwe zangu wale kuwa nilimpenda sana mtoto wao na hata siku wakipata kuwasiliana naye wamueleze kuwa sina kinyongo naye na ninamkaribisha ikiwa yu tayari kuuvunja moyo wake na kuujenga upya!! Niliondoka nikaenda kwa wazazi wangu na wenyewe nikawaeleza yote yaliyonisibu.... na baada ya hapo nikaanza maisha mapya pasipo uwepo wa Tina wala mtoto. Na ili nisiwakumbuke wawili hawa nikaamua kuhamia jijini Mwanza...... Vitu vyote vilivyokuwa katika kile chumba cha awali niliviuza sikutaka kubaki na kumbukumbu yoyote ile zaidi ya picha ambazo nilizihifadhi mbali kabisa na nilikuwa nazitazama mara chache sana.   Jijini Mwanza niliendelea na shughuli zangu, moyo wangu ukiwa umepoa kabisa. Nikisema umepoa namaanisha kuwa wanawake niliitambua tofauti yao kwa sababu ya sauti zao na mavazi lakini vinginevyo hakuna hisia yoyote iliyoamka katika mwili wangu nilipokutana na viumbe hawa..... Nikiwa Mwanza nilijitahidi kadri nilivyoweza kuhakikisha kuwa nawasahau kabisa Tina na mtoto wake.... nililazimisha hili kwa sababu kuna aina fulani ya chuki iliyoanza kujijenga katika nafsi yangu dhidi ya wanawake, nikisikia kuna mwanamke analalamika kuwa ananyanyaswa kimapenzi nilihisi kuwa hana haki na anastahili kunyanyaswa tu.. hii ni kwa sababu ya Tina!! Aliyonifanyia yalikuwa yameacha doa kubwa sana...... Naam! Naukumbuka usiku ambao kwa mara ya kwanza niliingiwa na huruma juu ya wanawake.... Haikuwa mara yangu ya kwanza kumsikia jirani yangu mmoja mwanaume akimwadhibu mwanamke ambaye nilikuja kufahamu baadaye kuwa hakuwa mkewe wa ndoa bali walikuwa tu wanaishi kimazoea. Kama kumwadhibu yule bwana alikuwa amezidi, lakini kamwe sikuwahi kujishughulisha na ugomvi wao, nilikuwa nawasikia majirani wengine wakimsihi aache kumwadhibu mkewe kiasi hicho cha kumvimbisha kila siku. Jambo moja ambalo nilijifunza katika maisha yangu ya kupanga pale Mwanza ni kwamba yule mwanamke alikuwa jasiri haswa, hakuwa na mvuto wa kufaa kuitwa mrembo wa dunia lakini alikuwa ana hadhi ya kuvuta macho ya wanaume wawili kati ya watatu watakaopishana naye...... Mvuto wake huu angeweza kujinmilikisha kwa mwanaume mwingine lakini ajabu ni kwamba alikuwa mvumilivu... na mara kadhaa nilizowahi kushiriki maongezi ya hapa na pale na majirani nilikuwa namsikia akimtetea sana mwanaume wake... licha ya majirani kumkosoa sana mwanaume yule yeye alimtetea. Nilishangaa sana lakini sikuwahi kutia neno..... Siku moja usiku wa saa sita na madakika kadhaa nikiwa natoka katika mihangaiko yangu ya siku zote nilipita kona za hapa na pale, huku nikiwa nimetawaliwa na uoga kutokana na vitendo vya kihuni vilivyokuwa vikitendeka usiku hasahasa wizi, nilisikia sauti ya kike ikijikaza kulia. Nilishtuka lakini nikajikaza na kuendelea mbele.... uelekeo niliokuwa naenda uliifanya sauti ile ianze kufifia na kupotelea mbali.... nikajisemea kuwa huenda nimejishtukia tu hamna kitu kama hicho. Nikiwa bado natafakari hiyo sauti mara nikasikia nikiitwa jina langu. Hapo hofu ikazidi lakini sikuwa mwepesi wa kukimbia, na hapo nikaona mfano wa kivuli kikinyooka kutoka katika mkunjo na kuwa katika umbo la mwanamke. Alikuwa ni Anita. Yule mwanamke anayenyanyaswa na mwanaume wake..... Nilisogea huku nikitetemeka lakini sio sana kama nisingekuwa nafahamu anavyofanywa na bwana wake yule. Nilimfikia na kumuona akiwa antetemeka, akiwa na upande mmoja tu wa kanga. “Kaka Mjuni nakuomba kama unayo shilingi elfu tano nisaidie nitumie kama nauli niende kwa dadsa yangu huko Nyamanoro...” alizungumza kwa shida akiidhibiti midomo yake iliyopasuka huku ikivuja damu isipasuke zaidi. Nilishusha macho yangu hadi chini na kushuhudia miguuni akiwa peku huku akiwqa anavuja damu gotini. “Kwanini usilale nyumbani kwako?” nilimuuliza huku nikitambua kuwa si rahisi jibu kuwa eti ameamua tu. “Kaka Mjuni, sio nyumbani kwangu tena leo amekuja na mwanamke mwingine amesema niwapishe!!!” alizungumza kwa shida meno yake yakigongana kinywani mwake. Jibu lake na hali aliyokuwanayo nilinifanya kwa mara ya kwanza kabisa nipatwe na chembe ya huruma kwa wanawake. Nilijiona nina mengi ya kusema lakini nikajikuta linatoka moja tu. “Pole sana Anita... pole sana!!” nilimwambia huku nikijaribu kumgusa walau bega lake. Nilijipekua na kutoka na shilingi elfu kumi na tano nikampatia, na kisha nikamuuliza usiku huo itakuwaje. “Siwezi kurudi ataniua yule!! Acha tu niende hukohuko mbele....” alinijibu kisha akanishukuru huku akiondoka mguu wake ukiwa unachechemea. Nilisikitika sana lakini sikutaka kujihusisha zaidi na maisha ya wawili hawa!!! Lakini huu haukuwa mwisho bali mwanzo kabisa, tena mwanzo wenye mengi|!!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni