FSEHEMU YA KUMI KINACHOUMIZA na kutesa linapokuja suala la mahusiano ya kimapenzi basi ni kumbukumbu, ukimwona mtu anakondeana na kukosa raha kisa mapenzi ujue kinachomuumiza sio kuachwa ama kuacha, kinachomtafuna ni kumbukumbu. Laiti kama pasingekuwa na nafasi katika ubongo ya kuhifadhi kumbukumbu kamwe mapenzi yasingekuwa yanazungumzwa kama yanavyozungumzwa leo hii.... NA HII NI SEHEMU YA KUMI. Nakumbuka katika kipindi kile Tina yu mjamzito na mama yake mzazi alipatwa na homa za matumbo kiasi cha kuzidiwa na kuhitaji uangalizi wa karibu sana, nikiwa kama mkwe kwa mama yule niliguswa na hali ya yule mama. Hadi ninapoyaandika haya sina maisha ya juu sana lakini pia sipo katika maisha mabaya ya kutisha. Na hata wakati ule nilikuwa na hali ya kiuchumi ya kawaida, nilifanya maamuzi magumu sana, nikaacha kumlipia mdogo wangu ada, pesa yote nikaamua kuitumia kumuhudumia mama yule alienizalia Tina wangu. Naikumbuka sikukuu ya wapendanao, Tina aliniletea zawadi na aliponikabidhi zawadi ile alinieleza kuwa kwa yote niliyomtendea mama yake mzazi hadi kurejea katika hali yake ya awali basi hana cha kunilipa zaidi ya upendo wake wa dhati. “Tina ni upendo gani huo wa dhati uliomaanisha kwani? Kwanini ukaniletea pigo kubwa kama lile... kwanini ukanitundika katika mti wenye miiba na kisha kuniponda na makaa ya moto? Samahani Tina awali niliahidi kusikiliza kila utakalonieleza lakini sasa nakuomba sana unyanyuke ukiwa kimya kabisa... ingia bafuni osha uso wako hasahasa hayo macho yako. Kisha nitambeba mtoto na tutatoka nje kana kwamba hakuna lolote lililotokea kati yetu...... tutaongozana hadi nyumbani kwa amani tele kama tulivyoingia. Kisha utalala ukiwa kimya kabisa, ukitafakari yote niliyozungumza na wewe.. halafu upate na maamuzi thabiti kabisa. Na asubuhi ikifaa utachukua hatua ya maamuzi yako. Lolote utakaloamua as long as halimuathiri mtoto huyu nitalibariki kwa mikono miwili.” Tina anayetetemeka vibaya sana alifuata niliyomuelekeza na alikuwa ananiogopa sana, hata kupishana na mimi ili aende bafuni alinipishia mbali sana. Nilijaribu kuvaa viatu vyake na kugundua kuwa hata kama ningekuwa mimi ningekuwa katika hali ileile. Aliingia bafuni akanawa kisha akatoka......... Alinikuta tayari nikiwa nimembeba mtoto, alipotoka nikamkumbatia na kumkumbusha kuwa bado nampenda!! Tukatoweka nikaaga mapokezi........ ***** (acha nafasi kidogo) Kweli tulifika nyumbani kwa kutumia usafiri uleule wa Taksi, tukaingia chumbani Tina akiwa bado anatetemeka mno. Ni kama mtu aliyehisi muda wowote ule naweza kuchukua aidha kisu ama silaha yoyote ile na kisha kumjeruhi vibaya mno. Kosa ambalo ninakiri nilifanya ni kujilaza nikiamini kuwa maneno yangu ya kumtia moyo Tina basi na yeye atalala na kufanya tafakari kisha ataamka akiwa na maamuzi sahihi kabisa. Na hata kabla ya kulala nilimsihi sana kuwa awe na amani sana tutazungumza asubuhi. Nikapitiwa na usingizi, na nilipokuja kushtuka asubuhi nilijikuta naingia katika ulimwengu mwingine kabisa. Sio Tina wala mtoto ambaye alikuwa katika kile chumba, nilipotazama saa ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri. Nilihangahika huku na kule nijue ni kitu gani kimetokea. Nilijaribu kupiga simu ya Tina lakini ilikuwa haipatikani. Alfajiri ile ningeanzia wapi? Sikuwa na pa kuanzia...... Nilisubiri hadi palipopambazuka nikaanza kuzurura kwa ndugu wa Tina kuwauliza iwapo wamemuona Tina lakini walinieleza kuwa hawajamuona. Nilipiga simu nyumbani kwao na wao hawakuwa na taarifa yoyote. Hali ilizidi kuwa tete hadi kufikia saa sita mchana bado nilikuwa sijajua Tina alipokuwa, mbaya zaidi alikuwa ameondoka na mtoto. Naapa kwamba laiti kama Tina angekuwa amemuacha mtoto hakika nisingekuwa katika wakati mgumu kiasi kile.... niliwaza sana ndugu msikilizaji, Tina atakuwa ameenda wapi na yule mtoto..... Wazo la kwanza lililokivamia kichwa changu baada ya kujifikiria kuwa yaliyomtokea Tina yangekuwa yamenitokea mimi... wazo la kwanza ni kujiua, na kama ni kujiua basi hata kile kiumbe asingeweza kukiacha hai na chenyewe lazima angekiua tu. Hapo sasa damu yangu ilinisisimka mno na mara kwa mara nilijaribu kujiwekea hoja pingamizi kuwa yule sio mtoto wangu, lakini nikalikumbuka lile tabasamu la kile kitoto nikajisikia kama mtu ambaye nilikuwa nimewahi kuonana na malaika aletaye heri. Sasa yule malaika yananijia mawazo kuwa kuna uwezekano akafanyiwa kitu kibaya kabisa. Nilikimbia hadi mlangoni na kuufungua mlango lakini kiunyonge kabisa nikaufunga mlango ule kwa sababu sikuwa na pa kwenda kwa sababu kama ni kuuliza basi kila sehemu nilikuwa nimeuliza. Nilibaki pale mlangoni huku ikinijia picha kichwani jinsi kitoto kile kitakavyokuwa kinanyongwa na Tina kikijaribu kutupa vikono vyake vidogo katika namna ya kupambana lakini kisifanikiwe hadi pale kitakapokata roho. Niliuma meno yangu na kisha kukigongagonga kichwa changu kuzilazimisha fikra zile ziende mbali nami...... Wazo la pili baada ya kutulia niliwaza juu ya Tina kuwa ni mwanamke mwenye moyo wa huruma sana, japokuwa alinitenda vile lakini bado alizaliwa akiwa na huruma. Basi kama hatamdhuru huenda atamtelekeza katika sehemu mojawapo kati ya nyumbani kwa yule hawara wake ama nyumbani kwa mama yake.... hawezi kumtelekeza sehemu nyingine tofauti na hapo.. Basi baada ya kuwaza mambo haya nikakusudia kupambana kwa ajili ya yule malaika Sonia. Nikaamua kuanzia nyumbani kwa yule bwana, litakalotokea huko nitakuwa tayari kulipokea. Ningepata amani ya nafsi iwapo tu ningeelezwa kuwa mtoto Sonia yupo salama.... nafsi yangu ilitawaliwa na hasira sana kujipeleka mikono nyuma kwa mwanaume ambaye alikuwa akimfanya mke wangu vyovyote alivyotaka kumfanya. Lakini ningefanya nini??? Niliingia bafuni nikaoga, nikavaa na kisha nikaifunga nyumba na kuondoka zangu, uziri ni kwamba nyumbani kwa mwanaume yule nilikuwa napatambua vizuri sana.. Nilifiika nikabisha hodi nikakaribishwa na mtoto mdogo aliyekuwa anafanana pua na mtoto Sonia... hali hii iliniumiza sana kwa sababu nilizidi kuamini kwa vitendo kuwa yule bwana kweli alimzalisha mke wangu. Niliongozwa na yule mtoto hadi sebuleni, huko nikakaribishwa na mwanamke ambaye alikuwa anafanania na kuwa mama kwenye nyumba ile..... nikamsalimia akanijibu kwa furaha huku akitabasamu. Nikamuuliza mume wake kama yupo akaniuliza iwapo nina miadi naye........ Niliposema hapana, akadai kuwa hayupo. Nikafahamu kuwa hilo jibu ni la kupewa.. mume wake amemueleza akija mtu ambaye hawana miadi basi amweleze kuwa hayupo. Nilishusha pumzi kidogo na kisha nikawa katika mashauri mawili, je nimwage ukweli wote mbele ya yule mwanamke ama niondoke kwa ahadi ya kurejea tena........ **Haya sasa, Mujuni katika harakati nyingine Tina yupo wapi na mtoto je????
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni