Jumamosi, 26 Desemba 2015

HILA NO.7

SEHEMU YA 7 Kabla hajapitisha maamuzi yoyote yale, mlango wa sebuleni uligongwa…. Upesi akakimbilia deki na kuitoa mahali ilipokuwa, akaificha chini ya uvungu wa kabati huku akiwa anatetemeka sana na jasho likizidi kumtiririka. Kisha upesi akachukua kisu kidogo kilichokuwa mezani akakizamisha mfukoni, ili kama kuna hatari yoyote mbele yake akabiliane nayo.   Alipoufungua mlango alikutana ana kwa ana na mwanamke wa kazi, mcheshi na anayemzoea mtu kwa sekunde kadhaa tu baada ya kukutana kwao. Alikuwa ni MAMA LAO!! Hakuwa na tabasamu usoni na ni kama kuna mambo mazito alikuwa ameyabeba na ilikuwa ni lazima ayatue. “Karibu…” Sam alimkaribisha huku akiachia nafasi mlangoni mama yule akapenya. Sam akaufunga mlango na kisha kumkaribisha mama lao katika mojawapo ya sofa pale sebuleni huku akilazimisha tabasamu hafifu midomoni. Baada ya salamu na pole za hapa na pale. Mama lao akamueleza Sam jambo lililobadili kila kitu katika kichwa chake huku likimwacha katika namna ya kukosa maamuzi kabisa!! Huo ukawa mwendelezo wa utata!!! **** Baada ya kudumu kwa dakika takribani dakika mbili bila kuzungumza kilichomleta, hatimaye alishusha pumzi na kumweleza Sam madhumuni ya ujio ule. “Vipi mama Lao! Na wewe ni mmoja kati ya watu wanaoamini kuwa nimerukwa akili? Umekuja kuhakikisha” Sam aliuliza katika namna ya kusanifu. “Nilitaka kuamini awali….” Alijibu mama lao kisha akaketi vyema na kumtazama Sam moja kwa moja machoni. “Ikawaje hata usiamini tena kama nimerukwa na akili mama…” “Kwa sababu nahisi ni mimi ambaye nimerukwa akili….” Alijibu kwa kifupi mama lao kisha akamalizia, “Nilikutana na watekaji kabla ya tukio”.  Sam akajitoa katika kuegemea kochi na sasa akawa kama nusu anataka kusimama na nusu anataka kuendelea kukaa. “Nini…unamaanisha nini mama lao..” “Walifika katika mgahawa wangu kununua supu, nilizikariri sura zao kwa sababu walikuwa wanaongea kinyakyusa na walikuwa wakizungumzia jambo ambalo nimeupata mwanga wake sasa baada ya kuhakikisha kuwa haujarukwa na akili….. walikuwa wakikuzungumzia wewe na kwa mbali kama walimzungumzia marehemu Steven Marashi japokuwa hawakumtaja jina lake moja kwa moja….” “Sijakuelewa mama, wewe uliwaelewaje wakati wewe mzaramo?” “Wengi sana ukiwamo na wewe mnatambua hivyo lakini mimi ni mnyakyusa, nadhani zaidi ya mama lao hata jina langu haulifahamu naitwa Sekela Ambindwile, lakini mama yangu alizoea kuniita Atuganile. Mbeya wakanifupisha na kuniita Atu….. naitwa Atu. Lakini endelea kuamini kuwa mimi ni mzaramo, napenda iwe hivyo kwa sababu zangu binafsi….” Mama lao alivuta pumzi kisha akazishusha na kuendelea. “Hivyo, nilielewa kila kitu…. Kumbukumbu zimenikaa sawa baada ya kuwaona leo wakirejea na mwili wako na kudai kuwa wao ni wasamaria wema wamekuokota mbali. Kilichonivuta zaidi ni kauli yao tata kuwa hata eneo lile ni mara yao ya kwanza kufika. Wameelekezwa tu nyumbani kwako kwa sababu wewe unafahamika……. Mashaka yangu yakaanzia hapo.” Mama lao alijiweka sawa, Sam naye akazidisha utulivu zaidi, hakuamini alichokuwa anakisikia. “Sasa wanataka nini kwangu eeh! Ni nini wanataka… nieleze mama lao nieleze niwapatie” “Siwezi kusema kuwa nafahamu moja kwa moja lakini kwa maneno niliyoyasikia, nahisi hata wao hawana uhakika kama wewe ni mtu sahihi kwao…. Wanachofanya ni kubashiri tu……na inaonekana wameagizwa” alijibu mama lao. Sam akawa mkimya tu akipokea maneno yale mapya na mazito. “Kwani wanakudai kitu gani Sam…” “Sura zao tu sijui, nitajua vipi wanachotaka kwangu mama” Sam alijibu katika namna ya kughafirika. Mama lao akaligundua hilo. “Lakini ukiachana na hayo ya kutokuwa na uhakika na hicho walichokuwa wakihisia kwako….. wale jamaa ni watu wa serikalini ama la wanafahamiana na mtu serikalini, kupitia mazungumzo yao nilisikia wakimtaja waziri wa ulinzi na waziri mkuu….. bila shaka jambo hili sio dogo.”  “Whaat! Waziri mkuu…. Mungu wee ni kitu gani sasa hiki…” “Usirukwe na akili Sam, tulia sana kuna jambo hapa. Hivi wewe unaamini kuwa Steve amekufa hivihivi??” mama lao alimuuliza Sam ambaye alikuwa ameanza kuizoea ile hali baada ya taarifa. “Hivi unaweza kuamini kuwa hadi sasa ninavyozungumza na wewe sijui rafiki yangu amekufa kifo cha namna gani?” Mama lao alishangaa kwanza kabla ya kumweleza Sam kuwa Steven Marashi anasemekana ameuwawa na sio kuwa tu amekufa kikawaida. Mama lao akamweleza zaidi kwa ushahidi wa magazetini kuwa Steven Marashi alikutwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni ambayo inasemekana alikuwa amelala na mpenzi wake ambaye inasemekana ametoweka, awali ikasemekana huyu msichana alikuwa ni Lili, mara vyombo vya usalama vikakanusha na kusema hadi sasa haifahamiki huyo mwanamke alikuwa ni nani. Sam akaduwaa na kuzidi kuuona utata waziwazi. “Lili yeye amesemaje juu ya shutuma hizi?” “Lili hajasema lolote lile, simu yake haipatikani…. Nd’o magazeti yanavyosema. Sijui tu hiyo kesho itakuwaje…” “Kesho kuna nini?” “Nd’o anazikwa marehemu….. na raia wanataka kupata mustakabali juu ya kifo hicho cha ghafla cha kipenzi chao. Aliyehusika aadabishwe….” Mama lao alijibu huku akionekana wazi kuingoja siku inayofuata kwa hamu. Waliendelea kuzungumza mengi juu ya utata huo. Hatimaye wakaagana kwa makubaliano ya kukutana msibani siku inayofuata!! Amakweli hakuna aijuaye kesho, hata yule mtunzi wa kalenda!! Haikuwa nyepesi kama walivyopanga!! ***** KIKAO kizito kilikuwa kimehitishwa katika ile nyumba ya siri mahali fulani nchini Tanzania. Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa amewaka kwa hasira kali, kitendo cha jopo lake kushindwa kuambulia lolote lile kulimfanya aone ni uzembe wa hali ya juu japokuwa hata yeye mwenyewe hakujua ni kitu gani wanakitafuta kutoka kwa Sam. Hiyo ilikuwa ni siku ambayo vijana wake wa kazi walikuwa wameleta mrejesho juu ya walichokuwa wakifuatilia. Na ilikuwa ni siku hiyo ambayo walikuwa wametoa vinasa sauti na kila kitu kilichokuwa kinahusiana na upelelezi wao ndani ya nyumba ya Sam. Ni kama walivitoa wakati usiokuwa muafaka, hawakufanikiwa kutambua iwapo Sam alipata mkanda wa picha za ngono, na pia hawakuweza kuyanasa maongezi ya mama lao na Sam. Huenda hayo yangeweza kuwaletea mwangaza mkubwa sana na hatimaye na wao wakijue kile wanachokitafuta. Bahati mbaya hata wao hawakuijua kesho yao!! Baada ya mwenyekiti wa kikao kile muhimu cha siri kung’aka sana, mwishowe aliwapa nafasi ya mwisho ya kufanya wawezavyo, siku iliyofuata yaani siku ya maziko, wafuatilie hatua kwa hatua kuanzia mwili unavyotolewa mochwari hadi mipangilio ya kuaga na hatimaye kuzika waangalie iwapo wataambulia lolote la kuwasaidia kujua wasichokijua. Wakaagana huku wakiingoja siku inayofuata, vijana wawili wa kinyakyusa wakalikamata jukumu lile katika mlengo mwingine, safari hii wakataka kubadili mbinu zao. **** ULIKUWA ni msafara mkubwa sana kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania. Wananchi walijaa barabarani, wengine wakiushangaa msafara wa kutokea Muhimbili na wengine wakiwa katika sura za majonzi kutokana na tukio la kumpoteza muigizaji wao mahiri. Barabara ya Bagamoyo ilifungwa kwa muda ili kuruhusu magari yanayokwenda tu Magomeni na kuyazuia yale yanayoelekea Kariakoo yasifanye safari zake. Ulinzi uliimarishwa pande zote za barabara, vilio vilisikika huku na kule na miale ya kamera ikiwaka bila kupokezana. Kila mmoja alitaka kupata picha ya tukio lile. Ama kwa hakika lilikuwa tukio la kuteka fikra za yeyote yule!! Msafara ulienda kwa mwendo wa taratibu huku gari kubwa la muziki likipiga nyimbo za kuwakumbusha wanadamu juu ya kujiweka tayari maana hawaijui siku wala saa. Katika gari ndogo aina ya Corola, baba wa marehemu akiwa ameyaziba macho yake na miwani alikuwa katika tafakari nzito juu ya wimbi zito lililotanda katika kifo cha mwanaye. Alimini kabisa kuwa hakikuwa kifo cha kawaida bali cha kupangwa, na kuna sababu kadhaa alihisi zinaweza kuwa chanzo cha kifo kile. Kubwa zaidi aliamini tangu siku ya kwanza ni kuwa kuna hila zimefanyika ili kuondoa uhai wa mwanaye. Alitamani sana kuwa mkewe angekuwa muelewa tangu awali na kumzuia mtoto wao katika mambo kadhaa waliyodhani anaweza kuwa anajihusisha nayo, lakini mkewe akawa upande wa mtoto wake, akamuunga mkono kwa kila jambo hata yale ambayo yalionekana kuwa ya hatari kabisa. “Yaani mama Steve ni mbishi huyu mwanamke!! Ona sasa mtoto amekufa anajifanya kugalagala na kuzimia kila mara anawasumbua tu watu, nilimwambia kabisa mapema kuwa tumkanye Steve….” Alilalama mzee Marashi kimyakimya huku akiwa amekamata gazeti mkononi mwake na asilisome. Alipolitazama lile gazeti na kukutana na picha ya Lili alikumbuka mengi sana, akamkumbuka msichana yule na mengi waliyokuwa wamezungumza awali na hapo akawa amepata wazo la awali kabisa juu ya kifo cha mtoto wake. Lili lazima kuna mambo kadhaa anayafahamu tu!! Baada ya maziko nitamtafuta….. Baada ya kauli ile alitoa miwani yake na kujifuta machozi kiasi machoni pake. Alipotaka kurejesha miwani machoni alishangaa kumuona dereva akiwa anahangaika na usukani, na hapo akasikia makelele mengi kutokea nje. Ile anageuka kutazama ni kitu gani kinatokea katika msafara wao akakutana na mpasuko mkubwa wa kioo ukiambatana na mlio mkubwa sana. Hakuweza kusikia jambo lolote tena. ***** Edson Mayagi ‘Ninja’, alikuwa akimalizia kipande cha sigara yake wakati macho yake yalipokutana na namba za gari ambazo alielezwa kuwa gari mbili nyuma yake ndipo alipanda baba mzazi wa Steven Marashi. Upesi akakitupa kile kipande cha sigara, akajiweka tayari katika kutimiza alichokuwa ameagizwa kwa malipo makubwa. Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana, hakuamini kama ataweza kutoka salama ama ndo atakuwa amefanya kwa ajili ya familia yake ambayo ilikuwa imejazwa pesa nyingi sana kwa ajili yake. Hawakujua ni pesa kwa ajili gani bali walijazwa pesa tu!! Ni Edson pekee aliyekuwa akilitambua hilo. Palepale akafanya maombi kwa Mungu wake aweze kufanikisha alichopanga kukifanhya. Na hapo akaliachia ghafla lori lililokuwa katika mteremko wa kuelekea Kariakoo, moja kwa moja likawa linaelekea katika gari aliyopanda mzee Marashi. Baada ya kuhakikisha kuwa lazima lori lile litajikita katika gari alilopanda Marashi, upesi akaruka na kujichanganya katika umati uliokuwa umetaharuki. Amakweli Mungu wetu ni wa ajabu sana…. Sala za Edson zikasikilizwa akatoka salama, na mzee Marashi akaupoteza uhai palepale. Kizaazaa kikaendelea!! *** KIFO cha mzee Marashi kilizagaa upesi sana hata kabla mwili wa mwanaye haujaingizwa katika nyumba ya milele…… pande kadhaa zikakijadili kifo hiki katika namna wazijuazo. Huku wakisahau kabisa juu ya vifo vya raia wema wengine ndani ya ile gari.  Lakini tabasamu zito kabisa lilikuwa katika midomo ya mzee Matata, tajiri maarufu kabisa nchini Tanzania mwenye asili ya kiasia lakini aliyekifahamu Kiswahili vyema na aliyeijua Tanzania. Tabasamu lile lilikuwa la mafanikio makubwa mno kutokana na kunyamazishwa kwa mzee Marashi kabla hajaropoka lolote lile. Amani ikatawala moyo wake!! Kwa upande wa wale vijana wawili wa kinyakyusa, walipagawa kutokana na tukio lile ambalo halikuhitaji jicho la tatu kutambua kuwa limepangwa maksudi kabisa kwa nia flani. Nia gani? Hilo likawa swali zito kabisa ambalo lilizua utata mpya!! UPANDE wa tatu ulikuwa na faida ya ziada, huyu alikuwa ni Sam. Ambaye alikuwa amejichanganya pia katika umati akifuatilia kwa ukaribu zaidi tukio hili ili aweze kupata mwangaza wa kitu gani kinachotokea katika ukungu huu. Kama ilivyo kawaida ya waandishi, Sam alikuwa na kamera yake akirekodi vitu kadhaa bila kujua ni kwa nini alikuwa anarekodi. Ni kawaida ya waandishi wa habari!! Kamera ya sam ilivutika kumrekodi kijana ambaye alikuwa akivuta sigara kwa fujo, mara aimalize mara asiimalize, mara aizime mara aiwashe. Sam akatambua kuwa mtu yule alikuwa na hofu kuu….. Ana hofu ya nini sasa? Kuchelewa anapoenda, kukamatwa na trafiki ama? Sam alijiuliza peke yake huku akipendezwa kupata walau picha mbili tatu za yule bwana mfupi mwenye kichwa kikubwa kilichoongezewa ukubwa na nywele zake kichwani. Macho yake hayakubanduka katika sura ya yule bwana, hata alipopanda garini alimshuhudia…. Awali alikuwa akipiga picha za mnato lakini wakati anabadili na kuamua kurekodi picha zinazotembea ndipo alipomshuhudia yule kijana akiliachia lori lake, Sam akazidisha umakini katika kamera yake akarekodi kila kitu na nzuri zaidi akainasa picha ya yule kijana akijirusha na kujichanganya kagtika umati wa watu. Sam akaizima kamera yake na papo hapo akauhitaji msaada wa mtu katika kulifuatilia hili, hakutaka kujihangaisha na ile ajali, alitaka kumpata msababishaji wa ile ajali. Angemuhitaji nani zaidi wa kuweza kumwelewa zaidi ya mama lao. Kidogo aache klumshirikisha katika hili kwa kuhofia kuwa mama lao hawezi kuwa na msaada wowote ule. Lakini nafsi nyingine ikamweleza kuwa usikihukumu kitabu kwa kulitazama jalada lake tu…..ni heri kuzama ndani na kusoma kilichomo. Sam akamvuta mama .lao kando na kumweleza kijuu juu kuhusu alichokiona, akamwelekeza mama lao ageuke nyuma aangalie chini ya mti fulani. Akafanya hivyo na kufanikiwa kumwona yule mtu mfupi mwenye kichwa kikubwa akiwa anavuta sigara na ,kupuliza moshi mwingi hewani. “Una uhakika…..” “Asilimia zote na nimemrekodi…” “Twende…” mama lao akamwambia Sam na kwa mwendo wa kawaida kabisa wakalifikia eneo ambalo yule kijana alikuwa pale Sam alitangulia mbele kabisa na mama lao akabaki kwa mbali. Sam akahisi kuwa mama yule ni muoga kwa kitendo chake kile cha kusimama mbali. Sam hakujua…na hakumjua mama lao…. Wakati akidhani kuwa ni jambo jepesi kufika na kumhoji yule kijana alikumbana na mshtuko baada ya kijana yule kufyatuka ghafla akitimua mbio baada ya Sam kufanya kosa kubwa kwa kujitambulisha kuwa yeye ni mwandishi wa habari. Bahati ilikuwa mbaya kwa yule kijana kwani alikimbilia upande ambao mama lao alikuwa ametanda. Ni huko alikutana na shubiri….. Sam hakuamini macho yake……..  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni