Jumatatu, 14 Desemba 2015

RIPOTI KAMILI SEHEMU YA 13

SEHEMU YA KUMI NA TATU KUNA mambo yanakera sana duniani, kila mmoja anayo kero ambayo kwake anaiona kubwa kupita zote. Fikiria kuhusu kusingiziwa, tena bora usingiziwe katika jambo ambalo halina madhara. Tatizo linakuja pale unaposingiziwa jambo ambalo linaharibu kabisa munekano wako katika jamii... Unaweza kujikuta unatenda dhambi kwa sababu ya kusingiziwa!! NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA TATU..... Niliingia ndani nikaoga uzuri ni kwamba kila chumba kilikuwa kinajitegemea upande wa choo na bafu.  Baada ya hapo nikajilaza kitandani na kuikumbuka sauti ya kusikitisha ya Anita na ule mwendo wake wa kuchechemea. Usiku ule mnene msichana kama yule anatembea peke yake gizani!!!  Niliyasikia maumivu waziwazi moyoni mwangu yakifukuta, napenda kukukumbusha mpenzi msikilizaji kuwa baada ya siku nyingi sana kupita hatimaye nilikuwa nimeumia moyo wangu kwa sababu ya mwanamke. Lakini niliapa kuwa pakipambazuka siwezi kujihusisha zaidi na jambo lile ili nisije kujizulia maumivu yanayoepukika. Kweli palivyokucha sikutaka kujihangaisha na jambo lile niliendelea na shughuli zangu, hadi zilipopita siku takribani nane ndipo nikakutana na kizaazaa kingine. Usiku huu nilikuwa nimewahi sana kurejea nyumbani, kichwa changu kilikuwa kinauma kiasi fulani hivyo nikaona si vibaya nikimeza dawa na kisha kutulia nyumbani. Hivyo majira ya saa mbili usiku nilikuwa tayari nimelala!! Ilikuwa saa tano na nusu usiku kwa mujibu wa saa yangu ya mkononi niliposikia mlango wangu ukigongwa. “Aaargh! Rose huyu naye...” nilijisemea nikiamini kuwa ni jirani mmoja aliyeitwa Rose. Dada mmoja ambaye tangu alipogundua kuwa ninaishi mwenyewe alikuwa analazimisha maozea, kila akirejea usiku lazima aniite kwa sauti na kisha kunisalimia. Sikuwa napendezwa na hali hii lakini ningefanyaje sasa?? Lakini hii ya siku hii ilikuwa tofauti hii ilikuwa hodi ya kimyakimya. Nilisikilizia kabla ya kujipachika taulo yangukiunoni na kwenda mlangoni nikauliza anayegonga ni nani.... sauti ya kike ikajitambulisha. Alikuwa ni Anita. Mapigo yangu ya moyo yalipiga kwa kasi sana, mke wa mtu mlangoni kwangu usiku ule kufanya nini. Niliachana na saa yangu ya mkononi kwa kuamini kuwa huenda inaniongopea nikaitazama saa katika simu yangu, mambo yalikuwa yaleyale..... Ilikuwa usiku sana, huku nikiwa natetemeka kiasi fulani mikono yangu niliufungua mlango.... nikatangulia kutoa kichwa ni hapo nilipozidiwa na hofu zaidi alikuwa amesimama pamoja na mwanaume wake akiwa amevalia pensi akiwa kifua wazi, Anita alikuwa analia na kama kawaida alikuwa amejeruhiwa. “Haya sasa si huyu hapa aliyekurudisha kwa wazazi wako, naomba uingie ndani kwake mjadiliane ili kesho akakutambulishe kwa wazazi wake na akuoe kabisa, si mnajifanya wajanja.” Alizungumza yule mwanaume kwa sauti isiyokuwa na masihara ndani yake. “Lakini Fred huyu kaka alinipa nauli tu! Hakunielekeza wapi pa kwenda!!” Anita mnyonge kabisa alimweleza yule mwanaume, hapohapo nikashuhudia anavyonaswa kibao kikali sana usoni. Damu ilinisisimka sana, nikatamani kusema neno lakini nikajizuia. “Anita nitakucharanga viwembe huo uso wako we mwanamke..... naomba tusijibishane ingia humu na nguo zako zitafuata!!” alimwambia kana kwamba pale mlangoni hapakuwa na mtu amesimama. Na mara akamshika ili amsukume aingie chumbani kwangu...... hapo nikauweka ukimya wangu kando. “Bro vipi mbona sielewi ni kipi unataka kufanya hapa!” nilimuuliza kwa sauti ya kushangaa kiasifulani.. Badala ya kunijibu swali nililouliza eti akanitukana tena tusi zito tu!! Nilishtuka mno.. huyu bwana tangu nianze kuishi pale sijawahi hata kutukanana naye zaidi ya kusalimiana mara moja moja leo hii badala anieleze kinachojiri ananitusi tena tusi zito kabisa. “Anita... sielewi kinachoendelea....” nilimgeukia Anita. “Waone Malaya wakubwa nyie, ujue mimi sio mjinga mnajifanya eti hamjuani si ndo hivyo, na siku ulipompa nauli anede kwao saa nane za usiku mlikuwa hamjuani si ndo hivyo!!” alihoji kisharishyari.. ile sauti yake ya juu ikasababisha majirani waamke mmoja baada ya mwingine. Sikuamini kitu kile kilikuwa kinatokea lakini haikuwa ndoto bali uhalisia. Mimi si muongeaji sana na sikutaka eti siku hiyo ndiyo nianze kuwa muongeaji, na wala si mpenzi wa kutukana hasahasa matusi mazito ya nguoni... na sikupenda kutukanwa vilevile..... Ili kuepusha lolote ambalo lingeweza kujiri nikaamua kuingia ndani, ile nataka kufunga mlango yule bwana akafika na kuuzuia. Nikatumia nguvu kidogo nikafanikiwa kuufunga...... “Aaah umemkimbia mwenzako eeh sasa utaukuta mwili wake hapa ukitoka....” niliisikia sauti yake ikionya. Na kweli haikuwa utani kilio cha Anita kilianza kusikika na milio ya mikanda ikiambatana na kilio hicho. Niliwasikia majirani wakimsihi huyo bwana aache kumpiga mkewe lakini alichojibu ni hiki. “hadi huyo Malaya mwenzake amfungulie mlango ndo ntamuacha!”  Majibu ya huyu bwana yalinikera sana, nini cha kufanya usiku ule?? Nikaishughulisha akili yangu upesi na kumkumbuka rafiki yangu aitwaye Tito ambaye ni askari, nilichukua simu yangu na kumpigia nikamueleza kuwa aje nyumbanikwangu usiku ule kuna tatizo la kiusalama nikamuomba sana. Kwa sababu na yeye hakuwa ameoa kama mimi alilalamika lakini mwisho wa yote alikubali kuja, nikamsihi achukue pikipiki. Akakubali!! Ukimya wangu uliendelea, na bila shaka ukimya huu ulimkera yule bwana wa Anita, alinitukana sana na alipoona matusi yamemuisha na amechoka kumpiga Anitha alianza kugonga mlango wangu na kisha akasemamkuwa kama sitoki anauvunja mlango ule!! Kama masihara vile akaanza kugonga kwa nguvu, majirani wengi wakiwa kinamama walimsihi asifanye hivyo, lakini kiburi kikampanda na mara akageuza usiku ule kuwa usiku wa fumanizi akasema mimi natembea na mkewe!! Ebwana eeh! Nilikuwa si mwepesi sana wa hasira nd’o maana niliweza kumuandalia Tina ripoti lakini kitendo alichofanya huyo bwana kudai mi natoka na mkewe na amenifumania nilijikuta nachemka vibaya sana..... Nikaitoa taulo ile na kisha nikavaa suruali ambayo nilitokanayo katika mihangaiko yangu ya siku hiyo...... Baada ya hapo nikiwa kifua wazi niliufungua mlango! Wacaha wee! Majirani walikuwa wengi na kila mmoja akingoja kuona nini kitatokea. “Nakuomba sana bwana kaka, kuwa mbali na chumba changu. Simjui mkeo zaidi ya usiku ule aliomba nauli nikampatia na sijawahi hata kuzungumza naye nakuonba sana sitaki matatizo na mtu...” nilimweleza kiukarimu sana, majirani wengi sana walikuwa wananiheshimu hata Rose alikuwa ananiambia mara kwa mara kuwa majirani huwa wananizungumza kwa mema na wanapenda jinsi ninavyoishi!! Hata nilipoongea pale wengi walitikisa vichwa kuniunga mkono. Lakini yule bwana ambaye hakuwa amelewa alikuwa an akili timamu akajifanya hana cha kunielewa, hapo sasa aanitukania mama yangu tena mara mbili!!! Akili yangu ikatulia kwa muda, sekunde mbili nikamtazama Anita akiwa anavuja damu akiwa ameketi chini akiugulia, sekunde iliyofuata nikamkumbuka Anita usiku ule wa giza akiwa hana msaada wowote na sekunde iliyofuata nikamkumbuka Tina na maasi yote aliyowahi kunifanyia hadi alipokuja kupotea akiwa na mtoto ninayempenda sana! Yote yalinipandisha mori lakini hili la Tina lilinipandisha hasira kuu... Nilikwambieni awali kuwa mimi si muongeaji sana.. hivyo sikuweza kuzungumza neno la ziada. Badala yake nilimvamia kwa kasi kubwa sana nikiwa nimeikunja ngumi yangu lakini sikuitumia badala yake nilimtandika teke kali sana mbavuni, akaanguka chini na hakuweza kuamka upesi kabla sijafika na kumkalia tumboni, na hapo kilichofuata ilikuwa ni kama filamu, nilikuwa naulenga uso wake na kupiga ngumi kalikali. Ndugu zangu, sikuwahi kuwa mgomvi mimi.., sikuwahi kumchokoza mtu ili tupigane tangu udogo wangu sijui hata hizi ngumi nilizitolea wapi. Ninachokumbuka kuwa nilikuwa napiga ngumi huku nikitukana, kila ngumi ilivyokuwa inatua ilisindikizwa na tusi. Baadhi ya matusi ninayoyakumbuka ni, mbwa kasoro mkia, mjinga mkubwa, mpuuzi, mnyanyasaji mkubwa.... lakini katu sikumtuykania mama yake wala tusi lolote la nguoni. Hakika nilimnyoosha sio siri!  Sauti za majirani wakinisihi nimuache nilizisikia lakini zilikuja kama kichina sikuelewa wanamaanisha nini.  “Sasa leo nakuua mbwa koko wewe!!” hili lilikuwa neno la mwisho kabisa kumweleza yule bwana kisha nikamtandika kichwa kimoja hadi mimi mwenyewe nikakumbwa na kizunguzungu!!! ***Haya nd’o yamefika huku, mwanamke hujawahi hata kumbusu unaambiwa eti unmefumaniwa naye.... hata ungekuwa wewe usingeweza kuwa na subira zaidi ya hapo...... Usikose muendelezo!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni