SEHEMU YA KUMI NA MOJA MUNGU na akutie nguvu ewe uliyempoteza mama yako, ama wewe usiyemjua mama yako kabisa. Mungu ni kimbilio la yote lakini mama ni kimbilio la mengi sana..... ukipatwa na jambo ambalo unahisi kwa kiasi fulani linaizidi akili yako tafadhali mkimbilie mama mueleze pasi na kumficha chochote!! Niamini mimi, hautaondoka kama ulivyoenda..... hautakosa chembe za matumaini. Kama ulikuwa umeanguka utasimama tena........ NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA MOJA. BAADA ya kutafakari kwa kina ni ni kitu gani ambacho naweza kufanya kwa wakati ule nikiwa katika nyumba ile nikaona hapo la kufanya ni kuondoka bila kuamua chochote. Nikamuaga yule mama nikamueleza kuwa nitarejea tena, akaniuliza mimi ni naniili mumewe akirejea amueleze nikamueleza kuwa naitwa Steven lakini mumewe hanifahamu kabisa mpaka nijieleze zaidi. Akaniaga nikaondoka!!! Nilipofika nje ya uzio ule nikaichukua simu yangu nikatafuta sehemu imetulia nikaingiza namba za mama yangu na kumueleza kuwa iwapo anayo nafasi ninahitaji sana kuzungumza naye. Akaniambia nimpigie bada ya nusu saa, tukaagana hivyo. Nikaondoka hadi nyumbani nikajirusha kiotandani, ile nusu saa ilikuwa imemalizika tayari na sasa ulikuwa wakati wa kumueleza mama kile ambacho kilikuwa kinanisibu kwa wakati hu. Nilimueleza mama hatua kwa hatua niliyopitia hadi hapo nilipokuwa, nilimwambia kuwa nilitamani sana nizungumze naye ana kwa ana maneno haya lakini wakati unanitupa mkono nahitaji ushauri wake ni kitu gani nifanye ambacho ni sahihi kwa wakati huo. Mama alishusha pumzi zake kwa nguvu sana, kisha akaniita jina langu la utotoni jina la Nshomile. Nikaitika kwa utulivu akanieleza kuwa na yeye ana mengi ya kuzungumza lakini akasema tumweke kando Tina na sasa tuzungumze kuhusu mtoto. Akaongezea kuwa yupo tayari kuniunga mkono kwa lolote jema ambalo litanifanya mimi nifurahi, na kwa hili pia akanieleza kuwa ni jema kwa sababu mtoto nimemlea na ninampenda basi huyo ndiyo furaha yangu, isitoshe hata kliniki jina aliloandikwa ni jina langu.... hivyo cheti chake cha kuzaliwa kinamtambulisha kama mtoto wangu. Mama akanieleza kuwa. Yeyote aingiaye katika vita kwa pupa huishia kuangukia pua lakini yule aingiaye kwa tahadhari kubwa anazo asilimia nyingi sana za ushindi. Akaendelea kunieleza kuwa hii ni vita na sehemu kubwa tayari nilikuwa nimeipigana tena kwa ushindi mnono sana, hivyo kuimaliza si kazi ngumu, mama akanishauri niende kuonana na mgoni wangu, huyo aliyekuwa akimfanya Tina vile alivyokuwa anapenda kumfanya. Akanieleza kuwa nikishakutana naye nisiwe na papara bali mpole na niliyekubali kujishusha kabisa. Dah! Ushauri wa mama niliuona mzito lakini akanieleza kuwa kama nilijishusha mbele ya Tina huku najua kila alichofanya, nashindwa vipi kumalizia kwa huyo mwanaume ili nijue kipi kinaendelea. Nikamuelewa mama na nikajipanga jioni ya siku hiyo kwenda kuonana na huyo bwana wa kuitwa Eric. Maneno ya mama yalikuwa yamenitia nguvu sana.... Na sikutaka siku hiyo ipite kabla ya kuonana naye, nikahairisha mpango wangu wa kulala na badala yake nikaamua nifunge safari kwenda nyumbani kwake tena lakini safari hii sifiki ndani ila nitajiweka nje na kutazama kila anayeingia na kutoka, akiingia tu na mimi naingia ama akitoka tu na mimi namfuata...... Wazo hili nikaliona ni wazo stahiki, nikavaa viatu vyangu kisha nikaufikia mlango wangu nikaufungua. Moyo wangu ulipiga kwa nguvu sana yaani ilikuwa kama filamu fulani hivi isiyokuwa na ukweli ndani yake. Filamu ambayo mwandishi wake ameunda tukio la mimi kufungua mlango na wakati huohuo mtu ambaye naondoka kwa ajili yake akiwa amesimama mlangoni kwangu akijiandaa kubisha hodi. Alikuwa ni Eric akiwa amesimama huku mikono yake ikiwa inatetemeka, sijui kama na yeye aliuona mshtuko wangu lakini mimi niliuona mshtuko wake vyema kabisa. “Karibu bwana!” nikamkaribisha..... “Tafadhali bwana Mjuni nakuomba sana unipe nafasi ya kunisikiliza nakuomba Mjuni!!” alinisihi nikabaki kushangaa... lakini hapohapo hofu ikaanza kuniingia kutokana na wasiwasi wake yule bwana. Na wasiwasi wa kwanza kabisa ulikuwa ule wa kupokea taarifa za msiba wa Tina na mtoto wake, nilikuwa tayari kupokea taarifa yoyote ile lakini sio taarifa hii. Niliamini kuwa nitakatishwa tamaa mno klulisikia jambo kama hili kwa masikio yangu. “Karibu ndani bwana Eric... karibu tafadhali...” nilimsihi akaingia ndani nikafunga mlango. Akaketi katika kochi mojawapo sebuleni na mimi nikaketi mkabala naye, nikawa namtazama kwa nukta jinsia livyokuwa akijiumauma kuzungumza... alikuwa anarudia rudia maneno sabna na hadi dakika tano zinapita nilikuwa sijaelewa lolote alilokuwa akisema zaidi ya kusisitiza kuwa anahitaji sana msamaha wangu. “Tina yupo wapi?” hatimaye nilimuuliza, na kabla hajanijibu nikaliboresha swali, “Tina na mtoto wapo wapi kwanza kabla ya yote?” nikasita na kumpa nafasi azungumze. “Kaka, ni mimi niliyetaka kukuuliza hilo swali.... nipo tayari umuite Tina na mtoto niwaombe radhi wote kwa pamoja....” “Hah! ina maana hujaonana na Tina ama?” nilimuhoji. “Nina zaidi ya wiki moja sijawahi kuwaona....” alinijibu, sasa alikuwa anatulia kiasi fulani.... “Na ni kipi hasa chanzo cha wewe kuja hapa?” nilimuuliza. Akanieleza kuwa nilipoenda nyumbani kwake alikuwa ndani na aliweza kufuatilia baadhi ya maongezi kati yangu na mkewe na kwa sababu alikuwa ananitambua alijua pia nini dhumuni langu la kwenda kwake. Akaendelea kunisihi kuwa mkewe ana matatizo ya moyo na laiti kama akigundua jambo hili la mimi kwenda kushtaki kuwa yeye ana mahusiano na mke wangu basi anaweza kufa palepale. Nilimsikiliza na kuuona udhaifu wa hoja yake ya kujitetea, alinikasirisha sana, yaani alikuwa anamuonea huruma mkewe lakini katu hakuwahi kufikiria ni uchungu kiasi gani ninapitia mimi kwa kutambua kuwa anahusiana na mke wangu tena mara kwa mara wanakutana na kisha kunisema watakavyo. Niliidhibiti hasira yangu lakini ikashindikana. “Eric unasema kwamba..... yaani unamuonea mkeo huruma lakini mimi haujali uchungu wangu si ndo hivyo....” nikaenda mlangoni na kuufunga mlango vyema na kutoa funguo. “Sasa Eric nahitaji tufahamiane vizuri kuwa nani ni mwanaume... umenitesa sana mwanaharamu mkubwa wewe....” Sasa ni hasira ilikuwa inaniongoza, nilimvamia Eric na kumkaba shingo yake, kilichosababisha hasira ipungue makali kidogo nmi kile kitendo chake cha kutopambana na mimi bali kuniacha nifanye nifanyavyo....... Mwishowe nilimuachia na kuruhusu machozi yanitoke..... na hapo nikaendelea kuzungumza. “Eric, nimeumia sana... umeniumiza sana... na bado unataka kuendelea kuniumiza. Yuko wapi Tina na mtoto....” nilikuwa nasita kila mara kumalizia mtoto wangu kwa sababu nilitambua kuwa aliyekuwa mbele yangu alikuwa baba halali. “Mjuni.. nielewe tafadhali... sijui na sina taarifa yoyote juu ya hili....” alizungumza huku akisihi haswa na nikaamini kabisa kuwa alikuwa haongopi..... “Sasa atakuwa wapi labda, ok! Tuachane na haya ya kale kwanza tuyaweke kiporo... tafadhali sana Eric nadhani waweza kuwa na mawazo walau mawili matatu ni wapi Tina anaweza kuwa.” Nikamueleza Eric huku nikimueleza pia kwa ufupi juu ya kilichotokea kabla Tina hajaondoka. Akafikiria kwa muda na kisha akanieleza kuwa huenda ameenda kwa shoga yake fulani hivi, akanielekeza mahali anapoishi, tukakubaliana kwenda wote. Tukafanya hivyo..... ITAENDELEA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni