Jumanne, 15 Desemba 2015

RIPOTI KAMILI SEHEMU YA 19

SEHEMU YA KUMI NA TISA Tina alikataa kata kata na bila shaka alikataa kwa sababu aliamini labda Sonia ataamka baadaye..... Katika purukushani za hapa na pale Tina alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea Sonia alikuwa amezikwa tayari... Kilio cha Tina kiliendelea kudumu zaidi na zaidi hadi siku alipomuomba rafiki yake nauli ili aende mbali na ardhi ya Kilindi kwa sababu kamwe hatakoma kulia.... Na hakutaka kuliona kaburi la mtoto wake kabisa, alipoulizwa sababu hakuwa na sababu alichoomba ni kuondoka tu!!! Ikawa kama alivyohitaji... rafiki yule akamsaidia nauli na kumtakia mema popote atakapokuwa. Tina aliondoka na kufanya safari hadi jijini Dar es salaam. Ilikuwa ni safari ambayo hakuelewa hata ina maana gani hasa  na ilibaki kidogo tu wazo la kujiua limpitie kichwani mwake kwa sababu alijiona ni mtu asiyekuwa na thamani yoyote ile katika dunia. Lakini wazo hili likaingiliwa na wazo jingine akamkumbuka sarafina mtoto wake. Akaona kuna namna fulani ya kutomtendea haki yule mtoto iwapo ataamua kumuacha duniani akiteseka pamoja na dada yake mlemavu. Alipofikiria jinsi maisha yalivyo magumu na baba wa mtoto bado anaishi akajiapiza kuwa atafika jijini Dar Es salaam na kumshurutisha yule mwanaume aanze kumuhudumia mtoto wake. Tina akajikuta kwa mara ya kwanza akiwa na roho mbaya kabisa dhidi ya yule mwanaume.  “Mjuni.. nilikuwa nipo tayari hata kuua kama ingebidi... ni huyo aliyeanzisha njia mbaya katika maisha yangu na kisha kunitelekeza pasi na msaada madhubuti...” alizungumza Tina kwa hasira sana. Mimi nilikuwa mtulivu nikichukua neno kwa neno huku nikiendelea kuichambua ripoti yangu kichwani. Hasahasa vile vipande vya ripoti ambavyo nilikuwa sijamsomea Tina..... lakini sikutaka kumuingilia kwa sababu alikuwa yu katika morali nyingine kabisa. Tina aliendelea kusimulia juu ya safari yake na hapa akafikia kuelezea jambo ambalo lilinifanya nimuonee huruma na kuyasahau kwa muda mengi aliyonikosea. Tina alinieleza kuwa kweli alifika jijini Dar es salaam na kwa sababu hakuwa mgeni wa jiji hilo alifanikiwa kuwapata marafiki kadhaa wa mzazi mwenzake. Wakamuelekeza anapopatikana na kweli akafika kwa mwanaume huyo. Mapenzi acha yaitwe mapenzi, hasahasa mtu ambaye mmechangia naye damu tayari na kuwa na kiunganishi cha mtoto, Tina alimkuta yule bwana akiwa anaishi na mwanamke mwingine. Hakutaka kuleta vurugu zozote zile kwa sababu hata yeye alikuwa ameolewa tayari, tatizo lilikuwa ile hali ya yule mwanaume kumkana Tina na kusema kamwe hajawahi kuzaa naye. Hapo Tina akavumilia akaondoka, lakini ajabu yule mwanamke ambaye alikuwa ni halali kwa wakatio ule kwa yule mzazi mwenzake Tina akaropoka jambo la kidhalilishaji kwa Tina. Tina aliyevurugwa na maisha tena aliyetoka kumpoteza mtoto wake mdogo akaona isiwe tabu ni heri amnyooshe kidogo yule dada. Na kweli akafanya vile akifanikiwa kumnasa vibao vitatu vikali kabla yule mwanaume hajaingilia kati kisha kumpeleka Tina hadi kituo cha polisi kuwa amekuja kumfanyia vurugu nyumbani kwake. Tina akaingizwa rumande alipokaa kwa siku tatu kabla ya kuachiwa baada ya mashemeji zake wa zamani kufanya mpango hilo jambo likapita. Kwa sababu hakuwa na pa kwenda akalazimika kwenda kuishi kwa siku hizo kwa hao waliomtoa rumande. Walikuwa ni vijana waliokuwa wanaishi maisha ya kibachela al maarufu kama ‘maisha ya geto’. Angefanya nini Tina na hakuwa na pa kuelekea, ikawa siku ya kwanza ikawa ya pili na hatimaye siku saba zikapita akiwa anahudumiwa na mashemeji hao wawili ambao usiku walikuwa wanalala chumbani huku yeye Tina akilala sebuleni. Moyoni alitambua wazi kuwa ni hatari sana kwa sababu kuwa shemeji haibadilishi mihemko ya kiume.  Akili yake haikuwa imepata njia mbadala ya kufanya hadi usiku ule wa manane ambapo mashemeji wale waligeuka kuwa viumbe hatarishi kwake. Walikuja wakiwa wamelewa na bila shaka walikunywa kwa ajili yake..... “Mjuni mume wangu.... nilitetemeka sana na kuwasihi sana wasifanye wanachotaka kufanya lakini hawakuwa wakinielewa... japokuwa walikuwa wamelewa lakini walikuwa na nguvu sana. Na tatizo kubwa ni kwamba nilikuwa nimelala nikiwa na nguo nyepesi tu, kwa sababu nguo zangu nilikuwa nimezifua. Nilijaribu kupiga kelele lakini haikusaidia kitu... mashemeji zangu zamu kwa zamu walisaidiana kunibaka... niliumia sana Mjuni niliumia moyo wangu.....” alishindwa kuendelea kusimulia Tina na kuanza kububujikwa na machozi huku akitokwa na kilio. Nikaingia katika jukumu la kumbembeleza Tina aliyekuwa anaugulia katika hali inayogusa moyo sana. Nilipomkumbatia Tina niligusana na mbavu zake, alikuwa amekonda sana... sio Tina yule niliyekuwa namkumbatia enzi zile!! Tina baada ya kutulia aliendelea kunisimulia kuwa alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea alijikuta  yupo jalala asilolifahamu na watu wachache wakiwa wanamshangaa. “Mjuni kama uliniombea mikosi naomba sana msamaha wako, nimelaaniwa Mjuni.... nimelaaniwa.....” alilalamika Tina huku akiendelea kulia. Nilimueleza kuwa hakuna baya lolote nililowahi kumuombea. Tina akatabasamu na kisha akaelezea kuwa kwa aliyoyapitia haiwezekani hata kidogo kuwa yametokea bila sababu. Kuna jambo moja ambalo nilitamani sana Tina anielezee ili niweze kuufunga ukurasa wa Ripoti yangu lakini niliona hajanieleza. Nikamueleza kama ananiruhusu na mimi nizungumze, akasema nimwachie kwanza amalize yote kisha ataniachia nafasi..... Na hapo akaelezea juu ya safari yake ya kutoka Dar kuelekea jijini Mwanza...... akaniambia kuwa anajisikia vibaya sana kunieleza alipata vipi nauli lakini nielewe tu kuwa alifika jijini Mwanza na kumkuta mtoto wake akiwa salama katika uangalizi wa mama yake mkubwa yaani Zawadi dada yake. Chuki yake kwa yule mtoto ilikuwa inakuja pale alipokuwa akiiona sura ya baba yake katika uso wake... lakini anakiri kuwa hakuwahi kuacha kumpenda mtoto wake kamwe kwa sababu ilikuwa ni damu yake. Lakini chuki dhidi ya wanaume ndiyo iliyomfanya awe kama nilivyomkuta..... “Tina.. ni nini hasa kilikusibu ulipokuwa Mwanza hadi ukaanza kunywa pombe na yote haya mapya ninayoyaona kwako....” nilimuuliza kiutulivu. Tina akaniuliza swali. “Mjuni una moyo mgumu sana natambua lakini sidhani kama upo tayari kulisikia na hili nqa kulipokea!! alijibu huku akinitazama. Nikamsihi sana kuwa nipo tayari kusikia jambo lolote lile... Tina akaniuliza mara mbilimbili kama nitaweza kuvumilia!! Swali hili la kujirudiarudia lilinitia mashaka kidogo japokuwa nilijiaminisha kwake kuwa nipo tayari kusikia na kupokea lakini kiukweli nilikuwa naogopa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni