SEHEMU YA KUMI NA NANE Baada ya mimi kuamua kutulia na kumweleza Tina kuwa sitaingilia akizungumza ni hapo alianza kuelezea lile tukio la usiku ule mnene. Haikuwa mpango wake lakini majuto yalimuongoza kufanya kile alichokifanya, kunyata usiku mnene wakati mimi nimelala hoi nikiwa nakoroma akamchukua mtoto wake nanguo chache za mtoto pamoja na zake, akaichukua pochi yake iliyokuwa na akiba kiasi ya pesa na hapo akanitazama nikiwa nimelala usingizi akanipungia mkono huku akinitupia busu la hewani kisha akaondoka zake dhamira ikiwa inamsuta kabisa kuwa halitakuwa jambo la heri hata kidogo kuendelea kuishi na kunitazama usoni wakati amenitendea mambo mengio mabaya,. Safari yake hii haikumuhusisha mtu mwingine zaidi ya yeye kuwa mratibu wa kila kitu, alipoutoa mguu wake nje alijenga chuki rasmi dhidi ya wanaume wengi. Historia yake ilimuonyesha jinsi wanaume walivyosaidia kuyaharibu maisha yake, huku wawili kati yao wakimuachia kumbukumbu ya maisha yote. Walimzalisha watoto..... Mtoto wa kwanza akitelekezwa huku huyu wa pili akiiharibu ndo kati yake na mtu aliyempenda yaani mimi Mjuni. Tina akajiondokea kinyongea hadi kituo cha mabasi akapanda basi linaloelekea wilaya ya Kilindi huko Tanga. Huko alikuwa anaishi rafiki yake wa kibiashara waliyefahamiana wakati ule anafanya biashara ya kuuza nguo.... ni huyu ambaye alimweleza kuwa anahitaji ampokee huko, japokuwa hakumueleza ni jambo gani linampeleka huko. Ilikuwa safari ndefu sana iliyogubikwa na wimbi kubwa la mawazo kichwani mwa Tina, yote yaliyotokea alikuwa hajayasahau na yalikuwa yanamsulubu. Alifika Kilindi na kupokelewa na huyo rafiki yake, hakumueleza kiundani sana yaliyojiri lakini alimueleza kuwa anaomba apumzike walau kwa siku kumi kisha atapata uelekeo mwingine. Rafiki yule hakuwa na hiyana akamuhifadhi Tina, lakini siku mbili tu zilitosha kufahamu fika kuwa baridi kali kupitiliza katika wilaya ya Kilindi lilikuwa ni tatizo kwa mtoto Sonia. Kifua kilianza kumbana mara ikawa kikohozi na akawa anashindwa kupumua vyema. Wataalamu wa afya wakamshauri Tina amwondoa mtoto upesi katika wilaya hiyo kwani hali ile ya hewa ni hatari kabisa kwa usalama wake. Wakati huo Tina hana pesa na rafiki yake yule alikuwa amesafiri kibiashara. Alijaribu kuwasiliana naye kwa njia ya simu na kumuo9mba msaada wa upesi lakini rafiki hakuwa akipatikana kwenye simu na pale nyumbani alikuwa amebaki na msichana wa kazi tu. Tina angefanya nini angali alikuwa mgeni katika mji huo?? Alilazimika kuendelea kusubiri, lakini ukaja usiku ule ambao Sonia alizidiwa sana. Alikuwa anatetemeka sana na alionekana dhahiri kuwa hawezi kupumua vyema... haya yalitokea majira ya saa nne usiku. Tina hana pesa, hana mtu amjuaye pale na rafiki hapatikani kwenye simu... msaidizi wa kazi hakuachiwa pesa ya kutosha zaidi ya shilingi elfu tano tu ya dharula kwa sababu ndani kila kitu cha kupika kilikuwepo. Elfu tano ingesaidia kitu gani...... Hakiuweza kufaa kitu... Mzazi hawezi kukubali kumtazama mtoto wake akiteseka atajaribu kufanya kila kitu ili kuweza kuitafuta nafuu ya mtoto.... Tuina akaona suluhu ni kuwasha jiko la mkaa ilimradi tu kulitafuta joto kiasi... Unaweza ukawa umeishi mikoa na wilaya nyingi zenye kusifika kwa baridi... lakini kama haujaishi Kilindi.. huko kuna baridi haswa!!! Kweli jiko likawashwa, na joto likapatikana walau. Na kitoto kikapunguza kutetemeka... sasa hata kutabasamu kilitabasamu... Tina akapata tumaini jipya akaendelea kumbembeleza mtoto hadi akalala. Tina akaingia katika dimbwi la mawazo, aliwaza siku za usoni za mtoto yule zitakuwaje na yeye pia akajiuliza baada ya siku kumi alizoomba ni wapi ataipeleka aibu yake?? Mawazo haya yakamtesa sana Tina hata akajikuta anasinzia bila kujua alisinzia saa ngapi...... Majira ya saa sita usiku alikuja kugutuka kutoka usingizini huku akipigania pumzi zake, alihema juu juu sana......na hakujua ni kitu gani kilisababisha hali hii. Alipoipata nafuu akarejea kukinyanyua kitoto chake.... Naam! Hapa ikatokea taswira inayoumiza isiyofaa kusimuliwa mara kwa mara, Sonia alikuwa amekauka kau kama kipande cha mti mkavu.... alikuwa wa baridi kabisa.... Sonia hakuwa na uhai!! Lile jiko waliloliacha linawaka liliendelea kuitumia hewa ya oksijeni ambayo Sonia na mama yake pia walikuwa wanaivuta usiku ule. Tafadhali mpenzi msikilizaji wa mkasa huu, kamwe usije kuthubutu kulala na jiko la mkaa ndani na likiwa limewashwa... mkaa unatumia hewa ya oksijeni kuendelea kuwaka na wewe unatumia hewa ya oksijeni ili uendelee kuishi..... Vita kati ya jiko la mkaa na mwili wa mwanadamu siku zote jiko la mkaa hushinda na mwanadamu huambulia mauti!!! Asalaale! Tina akawa ameuchoma na kuupondaponda moyo wangu, kwani kati ya kila kitu nilichotaka kusikia kutoka kwake basi kimojawapo ni juu ya Sonia kupoteza uhai... sikuwa tayari kabisa kwa jambo hili hata kidogo. Lakini sasa Tina alikuwa amenieleza kuwa Sonia hakuwa anaishi tena alikuwa mfu!!! Nilitaka kusema neno lakini ningesema neno gani la kubadili ukweli huu... sikuwa na neno lolote lile la kusema. Nikabaki kulia kama mtoto mdogo, Tina akafika na kunikumbatia mabega yangu na kisha akaniomba sana msamaha... “Kwa hiyo Sonia mlimzika wapi? “ nilimuuliza Tina kwa utulivu huku nikiyafuta machozi yangu. Tinaakazishusha pumzi zake kwa nguvu na kisha akaendelea kunisimulia.... USIKU ule ulikuwa mrefu sana kwake aliomboleza sana kifo cha mtoto wake, msaidizi wa kazi aliamka na kusaidia kuomboleza na hatimaye majirani kadhaa walifika katika tukio hili lakini hawakuwa wakaaji sana walipita kutoa pole kisha wakamuacha Tina na maiti yake. Hali hii ilimuonyesha Tina waziwazikuwa huu mzigo wote ulikuwa wake... Alipoteza fahamu na kuja kustuka alfajiri akiwa bado yu na mwili wa mtoto wake alianza upya kumuita Sonia ili aamke na kumkumbatia lakini haikuwa kama alivyotaka iwe... Majira ya saa nne rafiki yake alifika kutoka katika safari yake ya kibiashara.... alimweleza Tina kuwa akiwa safarini alipoteza simu hivyo hakuweza kufanya mawasiliano ya aina yoyote ile. Akamtia sana moyo na kishaakashauri kuwa siku hiyohiyo Sonia apumzishwe kaburini!! Tina alikataa kata kata na bila shaka alikataa kwa sababu aliamini labda Sonia ataamka baadaye..... Katika purukushani za hapa na pale Tina alipoteza fahamu na zilipokuja kurejea Sonia alikuwa amezikwa tayari... Kilio cha Tina kiliendelea kudumu zaidi na zaidi hadi siku alipomuomba rafiki yake nauli ili aende mbali na ardhi ya Kilindi kwa sababu kamwe hatakoma kulia.... Na hakutaka kuliona kaburi la mtoto wake kabisa, alipoulizwa sababu hakuwa na sababu alichoomba ni kuondoka tu!!! Ikawa kama alivyohitaji... rafiki yule akamsaidia nauli na kumtakia mema popote atakapokuwa. **Ni nini kilifuata baada ya kuingia jijini Dar es salaam?? Na nini hatma ya Ripoti hii kamili... Usikose sehemu inayofuata Mamlaka ya kuhukumu si yetu wanadamu... na kama yangekuwa yetu basi dunia isingekuwa sehemu salama ya kuishi. Hakuna mwanadamu mwenye utashi kiasi cha kufahamu huyu ni mwema na huyu si salama. Wanadamu tunaongozwa na hulka, kama utamuhukumu mwenzako kwa hulka na mitazamo yako binafsi kumbuka na wewe wapo watakaokuhukumu hivyohivyo... Ukihitaji kuhukumu hakikisha kwanza umeiandaa ripoti kamili. Na je utajuaje kuwa ripoti yako ni kamili????
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni