Jumapili, 3 Januari 2016
HILA NO.13
SEHEMU YA KUMI NA NNE
MAMA lao alichepuka mitaa kadhaa ya Kinondoni, akiwa amejitanda juba jeusi. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa. Na alipanga iwe hivyo ili aweze kujichanganya na waumini wa dini ya kiislamu hata likitokea lolote baya dhidi yake.
Alitembea hadi uwanja wa Biafra, akakitazama kikaratasi mkononi mwake akaisoma ramani kama ilivyochorwa na Gama.
Akaifuata na kuielewa, akahesabu nyumba nne nyuma ya jingo la ghorofa ambapo zamani ilikuwa shule ya Biafra.
Nyumba ilikuwa pweke sana lakini kwa mbali ulisikika mziki wa mwambao ukikata mawimbi.
Mama lao mwenye roho ya paka akafika mlango na kubisha hodi. Aliita mara kadhaa, lakini hakupata majibu. Lakini wakati anataka kuondoka zake akasikia hatua nyuma yake.
“Karibu dada!”
“Asalaam aleykum..” mama lao akasalimia. Yule dada akamjibu vyema na kumkaribisha.
“Samahani sijui nimepotea ama nipo sahihi, hapa nd’o kwa Mariam…” aliuliza mama yao ilihali akiwa amemtambua yule dada kuwa ndiye Mariam.
“Ni hapa kulikoni…”
“Ooh! Asante… kumbe sijapotea…” mama lao akaketi kwenye kibaraza. Kisha hakumpa nafasi ya kuuliza yule binti.
“Kwanza pole sana kwa msiba japo ni wetu wote! Naitwa Sekela..” alijitambulisha. Mariam akatambua yule dada alikuwa akizungumzia msiba wa Steven Marashi lakini alilazimika kuuliza ili kupata uhakika.
Mama lao akajieleza kuwa yeye ni mama yake mdogo na Steven Marashi.. hayati Steven Marashi. Na alikuwa na ujumbe mzito wa kuzungumza na Mariam.
Yule binti aliikunja sura yake kumaanisha kuwa amekerwa na taarifa ile.
“Ni kitu gani hicho… na kwanini asiende kuulizwa Lili mnakaa tu kuniumiza mimi kichwa…” Mariam akaanza kuongea kwa hasira.
Mama yao akacheka kimoyomoyo, huku akitambua kuwa yule binti alikuwa haujui ule usemi wa usizungumze iwapo una hasira.
“Familia yetu.. ama niseme mimi hapa nakutambua wewe kuwa ni wifi yangu, sijui lolote kuhusu Lili, kwanza Lili ni nani?
“Mpenzi wake!” alijibu kwa kiburi huku akibetua midomo yake.
“Mariam!” mama lao aliita kiutu uzima kisha akamsihi Mariam aketi chini.
“Nani mwingine amekuja kukuuliza juu ya Steve sasa. Jamani kaka yangu mimi….” Aliuliza kwa kulalamika.
“Kuna mwingine amejifanya sijui askari sijui mwandishi nani ameniuliza maswali kedekede mwisho wa siku wamekuja maaskari wa kweli wamemsomba hapa….. bora akome maana alikuwa na maswali huyo!” Mariam akazidi kufunguka.
Mama lao akaguswa na pointi ya mwandishi wa habari, akahoji zaidi. Akaelezewa juu ya muonekano wa mwandishi huyo.
Alipoelezewa akatambua kuwa hakuwa Sam.
Mama yao akaendelea kumuuliza Mariam na hatimaye akafikia lengo. Alitaka kujua iwapo Mariam angeweza kujua chochote juu ya kifo cha Steve.
Mariam alikataa kata kata na mwisho akazirusha lawama zote kwa Lili. Mbaya zaidi hata alipokuwa akikaa hakuweza kupajua.
Alichojua ni kwamba Lili ni muigizaji wa filamu na walikutana na Steve hukohuko kwenye filamu.
Mamalao akafikiria kwa kina kisha akaichezea akili ya Mariam.
“Ujue wifi, tuna mashaka kuwa kaka yetu alinyweshwa sumu, madaktari hawajasema lolote lakini alinyweshwa sumu kisha akaporwa vifaa vyake vya kazi.”
“Nini.. au ule mkanda aliokuwa akitembea nao mara kwa mara… halafu hata sikuwa najua kazi yake ni nini….” Mariam akaropoka.
Mama lao akamsifu Yakubu Gama kimya kimya kwa sababu alimwelezea Mariam kama alivyo na tabia zake za kuropoka bila kujua lipi jema na lipi sio jema.
“Ndio huo mkanda na vifaa vingine……”
“Mh! Labda Lili wake alitaka ajiachie vyema na waziri nd’o maana akamwekea sumu tutajuaje sie tulioachwa!!” akaongea kifedhuli kama anayeshushua!
“Waziri? Ina maana Lili hakuwa mwaminifu kwa kaka yangu ama..”
“Wanajua wenyewe.. mi sijui kwakweli, basi tu marehemu hasemwi vibaya, ila Steve hajui tu nilimpenda kiasi gani… akaenda kwa hicho ki Lili chake… haya yapo wapi laana tupu…” aliendelea kuropoka mambo mazuri Mariam. Mama lao akayahifadhi katika kichwa chake.
Baada ya mazungumzo marefu akaaga!
Huku akikiri kweli ile ilikuwa komborela.
Wakati anaondoka akajisemea kimoyomoyo, KOMBOLERA Mariam!!
Kisha akatabasamu!!
****
Wakati mama lao akitabasamu baada kuanza kucheza komborela vizuri. Tina mchumba wa Sam alikuwa katika kilio kikubwa.
Kwa mara nyingine alikuwa akikabiliana ana kwa ana na mzee Matata, mzee ambaye kabla ya matatizo hayo aliwahi kuwa mtu wake wa karibu sana. Ukaribu huu ulikuwa wa sababu maalumu sana ambayo sasa ilikuwa imegeuka shubiri!
Ukaribu huu ulianzia kwa Lilian ambaye alikuwa rafiki wa Tina wa muda mrefu kudhaminiwa akafanya filamu, msimamizi wa kila kitu akawa ni mzee Matata na kampuni yake.
Kama hili halitoshi filamu ikasambazwa na mzee Matata. Kisha akamnunulia gari ya kutembelea Lilian.
Magazeti yakamtaja Lilian kama msanii wa filamu mwenye umri mdogo lakini mafanikio makubwa, hawakujua ambacho kilikuwa kinaendelea.
Tina aliingiwa na wivu lakini hakuuweka wazi kwa sababu Lili alikuwa akimpatia pesa mara kwa mara na kumsaidia mambo mengi yaliyohitaji pesa kutatuliwa.
Raha ziliendelea na Tina akazidi kuwa karibu na Lilian na mzee Matata. Wakicheka kunywa na kufurahi pamoja.
Siku moja Lilian alimwomba ushauri Tina juu ya jambo ambalo alikuwa ameshirikishwa na mzee Matata. Lilikuwa likihusiana na mambo ya filamu. Hakika lilikuwa dili kubwa ambalo Lilian hakuwahi kulipata tangu aanze kucheza filamu.
Lilian alitakiwa kucheza filamu na wazungu lakini atatakiwa kufanya busu la mdomo kwa mdomo ambalo kitanzania waigizaji wake hawaruhusiwi kufanya vile.
Kwa kucheza filamu ile angelipwa kiasi cha dola za kimarekani laki moja ambazo ni zaidi ya milioni mia moja za kitanzania.
Tina aliposikia juu ya dau lile, mate yakamtoka kwa tamaa akatamani mchumba wake Sam angemruhusu na yeye kujiingiza katika masuala ya filamu. Lakini Sam hakutaka kabisa mambo hayo!!
Tina kwa kutambua kuwa Lilian atampatia kiasi fulani cha pesa baada ya kulipwa, akajikuta akimpa ushauri wa kukubali.
“Kwani kubusu nd’o nini, mbona kina Angelina Jolie wanafanya makubwa zaidi ya hayo. Cha msingi filamu sio ya bongo basi… huo nd’o uigizaji bwana watu wanapata pesa kama hivyo. Shoga!! Usiache” Tina akamshauri Lili
Umri wa Lilian ulikuwa mdogo na uwezo wake wa kufikiri ulikuwa mdogo vilevile. Akasahau ule usemi wa akili za kushikiwa changanya na za kwako.
Akajipeleka kuusaini huo mkataba huku akitabasamu na kujitapa katika vyombo vya habari kuwa muda si mrefu atakuwa kama nyota wa ‘Hollywood’.
Kilichokuja kutokea pale ikabaki kuwa siri ya watu watatu!
Lilian muhusika mkuu, Tina mshauri na Mzee Matata mzalishaji wa hiyo filamu.
Liliani akaleweshwa madawa asiyoyajua na kisha kuchezeshwa filamu ya ngono!!
Filamu ambayo ilikuwa na maana kubwa sana katika kubomoa na si kujenga. Filamu ambayo mkono wa mtu mzito serikalini ulisimamia ifanyike ili kulisulubu tabaka fulani.
Baada ya filamu ile, Lilian akaanza kuishi kama mtumwa!
Kila aliloambiwa alitakiwa kulitii, kwa nje alionekana mrembo na mwenye tabasamu muda wote lakini ndani ya moyo wake alikuwa katika kifungo kibaya mno.
Alikuwa anateketea.
Angefanya nini wakati kuna mkanda ambao ameigiza filamu ya ngono, alitishiwa kuwa akikataa jambo lolote lile mwisho wa siku mkanda ule utasambazwa Tanzania nzima.
Onyo lile likamtetemesha Lili na kuondoka na uhuru na amani yake. Hakutaka hata kidogo kuchafuliwa jina lake, alitamani kurudisha siku nyuma ili akatae dili lile lakini neno ninge huja mwisho wa safari.
Lili alikuwa mwishoni!
Tina aliijua ile siri, akapewa onyo na Lilian kuwa ajitahidi mtu asijue juu ya jambo lile.
Wasichana na siri wapi na wapi?
Tina naye akamshirikisha mama yake juu ya jambo lile!!
Wakadhani siri inaweza kutunzwa na watu wawili.
Baada ya Lilian kutambua kuwa yu kifungoni basi akaamua kuwa mtumwa safi. Kila alichotakiwa kufanya alitii ilimradi kuwafurahisha wanaoshikiria mkanda ule.
Safari hii akatakiwa kumshawishi muigizaji mwenza Steven Marashi hadi ajikute katika penzi lake. Hakujua ni kwa nini anatakiwa kuanzisha mahusiano na kijana yule ambaye alikuwa akimzidi miaka mingi.
“Lakini jamani ananizidi sana mbona mnanionea…” alilalamika Lili baada ya kupewa mtihani ule.
“Anakuzidi, wewe umelala na mababa wangapi leo hii unasema Steve mkubwa kwako…”
“Noo Matata sio kama unavyodhani lakini naheshimiana naye kama kaka yangu tena kaka mkubwa…”
“Ok! Kwa hiyo umekataa…” Mzee Matata akamuhoji huku akitabasamu.
Lili akajua mzee Matata amekasirika tayari. Akampooza na kukubali kuwa atayaanzisha mahusiano.
Utumwa ukaendelea!!!
Hatua kwa hatua, mara ikaundwa filamu wakacheza pamoja. Mara ghafla wakatakiwa na kampuni moja nchini Ghana, Lili kaambatana na Steven marashi wakiwa wasanii pekee kutoka Tanzania.
Ni huko ambapo uvumilivu ulimshinda Steve na kujikuta akiibanjua amri ya sita na kisha kuyaanzisha mahusiano ya siri na Lili ambaye kiumri alikuwa mdogo wake sana.
Mapenzi kikohozi hayafichiki hata kwa dawa!
Hatimaye uhusiano ukawa wazi, Steve na Lili. Lili na Steve.
Steve Marashi naye akasahau kuwa mapenzi kitovu cha uzembe. Akajisahau ni kwa nini alijiingiza katika uigizaji, akajisahau kuwa yeye ni mwanausalama wa taifa na katika filamu alikuwa chini ya mwamvuli ule ili aweze kuyafanya mambo yake vyema.
Penzi la Lili likamkolea, hakujua kuwa Lili alikuwa akitumiwa ili aweze kumpeleleza.
Mpelelezi yule akaanza kupelelezwa!!
Lilian akawa anategea wakiwa chumbani, anamuandalia mambo ambayo hakuwahi kufanyiwa na wasichana wake wa huko nyuma. Kisha kumchimba hapa na pale.
Yale mambo yakasababisha Steve aachane na Mariam, msichana aliyedumu naye penzini kwa muda mrefu kiasi. Ikawa Lili na Steve, Steve na Lili. Magazeti ya udaku yakabaki kuwaandika kila kukicha.
Shambulio baya ambalo Steve hakujua kama ni shambulio lilifanyika nchini Uganda. Kama kawaida Steve na Lili waliitwa kwa ajili ya kufanya filamu.
Shambulio lenyewe nalo liliandaliwa kama filamu ya pili isiyokuwa na mpiga picha wala muongozaji.
Kwanza ilianza shughuli iliyowapeleka Kampala, kutwa nzima wakashinda mbele ya kamera wakitengeneza filamu. Kazi ikakamilika.
Usiku wakakutana wasanii wote pamoja na wawezeshaji wa filamu ile kukamilika. Walikutana kwa ajili ya kupata chakula.
Pia wakacheza mziki kidogo.
Lili alimuona msichana mmoja akimkumbatia Steve wakawa wanacheza mziki. Lili akaipata sababu.
Ni hapo ambapo Lili aliianzisha filamu ya pili. Filamu isiyokuwa na wahusika wengi sana, bali wawili tu. Akaacha kunywa kinywaji chake, akatafuta meza nyingine akahamia hapo na kujiinamia.
Mwanamke akauvuta mdomo!
Steve alipomuona akagundua tayari Lili wake amekerwa na jambo. Alipoenda kumsemesha Lili hakujibu kitu zaidi ya kuzidi kuuvuta mdomo. Kisha ili kuifikisha ile filamu sehemu nzuri zaidi, Lili akamponyoka Steve na kukimbilia chumbani.
Hakujua kuwa Lili alikuwa kazini.
Akamfuata huko na kuanza kumbembeleza. Lili akaanza kumlalamikia Steve kuwa amemuacha yeye amekaa halafu akaenda kucheza na watu wengine.
Steve ndani ya moyo wake alilipuuzia jambo lile lakini kwa nje alilazimika kumbembeleza Lili. Alitambua kuwa hata umri nao ulichangia.
Katika kubembeleza mara amguse hapa mara kule.
Lili akaanza kuyajibu mashambulizi!
Alimfinyafinya Steve mgongo wake kabla ya kuanza kumshambulia kwa ulimi mkali katika kona mbalimbali za mwili wake huku machozi yakimtoka na kilio cha kwikwi kikisindikiza.
Kila Steve alivyojaribu kujibu mapigo alikutana na pigo jingine jipya kabisa kutoka kwa Lili.
“Ni kitu gani unataka nikufanyie Steve mpenzi wangu.. unaitaka roho yangu eeh!” alilalamika Lilian.
Ama! Wanawake ni sumu kali hakika!
Steve akalegea kabisa, akaanza kuweweseka na kujibu kila kitu ambacho Lilian alikuwa akimuuliza.
“Baby… kwani we ulisomea filamu ulipokuwa uingereza… niambie ukweli mpenzi wangu. Mbona mimi wanijua kwa kila kitu…”
“Hapana mpenzi sema nikikwambia kazi yangu mi utaniacha… lakini huwezi amini Honey mimi mtu safi kabisa.”
“Mh! Kazi gani sasa hiyo hadi isababishe kuondoka na penzi langu kwako…” Lilian alinong’ona katika masikio ya Steve, kisha akauingiza ulimi katika sikio la Steve.
Wacha wee!! Steve akasisimka mwili mzima. Na palepale Lili akaupenyeza mkono wake na kuzikamata ikulu za Steve.
Naam! Mwanaume akasalimu amri na hapo mpelelezi yule akageuka chiriku. Akajieleza hata ambavyo hajaulizwa.
Steve akaelezea hadi nia yake ya kujiingiza katika filamu na hapo akayasema mashaka aliyonayo dhidi ya raisi mtarajiwa bwana Mathias Obhare.
“Yaani mpenzi wanguu… oooh! Huyu Mathias huyu naamini kabisa amemfanyia mtimanyongo Msele na ile kesi ya kutekwa ni ya kuundwa tu… ninachohisi raisi na Mathias Obhare wanao mpango fulani wa kubebana, na lazima kuna kitu wanaficha nd’o maana…..aaah!” hakuweza kuendelea Lili alikuwa ameshalipata jibu alilokuwa ameagizwa na mzee Matata. Na palepale akamrukia kifuani kwake wakiwa uchi wa mnyama kisha…. Kisha………..mkono ukazikamata ikulu…………
Asubuhi kila mmoja alikuwa hoi!!
Mpelelezi akawa amepepelezwa!
Baada ya tukio hili mambo yakaanza kubadilika kwa kasi ya ajabu.
Naam hata kabla ya mwezi kumalizika, sasa Tina shahidi wa tukio lote hili ni adui mkubwa wa mzee Matata, hajui Lili alipo, hajui nini kilimuua Steve, hajui Sam wake kama yu hai ama amekufa.
Alichojua ni kwamba yeye ni mateka wa mzee Matata na hajui hatma yake.
SASA mzee Matata alikuwa amesimama mbele ya Tina, hapakuwa na urafiki tena bali uadui mkubwa mno.
Tina alikuwa amekonda sana kutokana na mateso. Alitakiwa aseme ni wapi ambapo ule mkanda wa ngono aliocheza Lilian ulikuwa ukipatikana.
Tina alikataa katakata kuwa hajui lolote juu ya uwepo wa mkanda ule na alipinga vikali kuwa Sam alikuwa na mkanda ule.
“Baada ya masaa arobaini na nane nitaigawanya shingo yako mbali kabisa na kichwa chako iwapo utaendelea kuficha siri juu ya wapi ulipo mkanda…. Ni aidha uuseme ukweli ama ufe.” Mzee Matata alimfokea Tina kisha kumzaba kofi kali mgongoni na kuubamiza mlango kisha akaufunga kwa nje.
Tina alibaki kuikumbuka siku ya kwanza kukutana na mzee Matata akatamani siku zirudi nyuma siku hiyo isijitokeze maishani mwake.
Akaijutia na siku ambayo aliruhusu kinywa chake kumshauri Lili juu ya dili lile haramu.
*****
KIJIJI CHA MAFISA, HANDENI TANGA.
Mwanaume ambaye umri wake ulikaribia miaka hamsini alikuwa amejikita katika kulima bustani ya wastani ambayo ilikuwa jirani na nyumba ndogo ya tofali za kuchoma.
Mwili wake ulikuwa umenawiri na alikuwa akitokwa jasho hivyo kusababisha kipara chake kiweze kuonekana vyema.
Kila alivyokuwa akinyanyua jembe na kulikita katika ardhi alikuwa akisindikiza na wimbo wa kabila lake.
Alionekana kufurahia wimbo ule na hivyo kasi yake katika kulima ikaongezeka maradufu.
Hatua zilizosikika nyuma yake zilimsimamisha kulima, akageuka na kukutana na sura ambayo haikuwa ngeni sana machoni pake, lakini hakujua ni wapi walikwahi kukutana ama bwana yule alimuona wapi hapo kabla.
“Habari kiongozi..shkamoo” kijana alimsalimia yule mzee kwa nidhamu ya hali ya juu.
“Marahaba bwana.. wewe si mgeni machoni pangu lakini sidhani kama ni kijana wa hapa kijijini kwetu….” Alijibu yule mwanaume mtu mzima.
“Mheshimiwa tumeonana kama mara tatu hivi, niliwahi kukutembelea ofisini kwako… nilikuwa nikiandika makala miaka minne sasa imepita…”
“Ahaaa ni Samweli ama ni Samson…. Kama sijakosea…”
“Samwel Mbaule mheshimiwa…..” alijibu yule kijana huku akifurahia kutambulika mapema tofauti na alivyodhania
Mbele yake alikuwa ni John Masele, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na nje ambaye kipindi cha miaka mitatu iliyopita alitangaza nia ya kugombe uraisi lakini yakatokea mambo ya ghafla na hatimaye kuvuliwa vyeo vyote alivyokuwanavyo, mwishowe akaamua kulikimbia jiji na kurejea kijijini kulima.
“Sura yako haibadiliki Sam…. Ni kipi kimekuleta huku kijijini kwetu ambapo hatujui hata Tanzania inaendaje.”
“Ni wewe mzee nimekuja kwako…. Nimehangaika sana lakini kupitia ile makala nliyofanya na wewe nimeweza kukumbuka ulisema juu ya kijiji cha Mafisa kuwa ukistaafu utakuja kulima huku. Naam! Nimefanikiwa kukupata…nimejaribu tu kama pata potea kwa sababu bila kukuona wewe mambo yanaweza kuendelea kuniwia magumu”
“Sam, mbona unahatarisha maisha yako sana…. Hapa si mahali salama hata kidogo. Ni watu wachache sana wanaoweza kuonana na mimi kisha wakaendelea kuishi kwa amani…. Wewe si mwandishi wa kwanza kufika huku… waandishi wangapi umewasikia wamekufa kwa ajali za gari, wangapi umewasikia wamepigwa risasi na jeshi la polisi kwa kisingizio kuwa ni bahati mbaya… hao wote wamekufa na siri zao Sam”
“Natambua sana mzee wangu lakini tayari nipo hatarini sitakiwi kurudi nyuma mzee. Hata nikisema nikomee hapa nilipoishia sanasana nitaishia kumpoteza mchumba wangu ambaye yu mikononi mwa watu wabaya”
“Sam ondoka sasa hivi kama hujaonana na mimi kisha saa mbili na nusu usiku njoo tukutane eneo hilihili, na baada ya kukutana huko naomba uishi na kauli moja kichwani mwako ya kwamba hujawahi kukutana na mimi popote pale. Sahau kabisa kama tulionana…. Hata ukibanwa vipi nakusihi jibu lako liwe hujawahi kuonana name, na mimi nikiulizwa nitasema sijawahi kukutana na kiumbe kama wewe maishani”
Sam akatii na kuaga!!
Majira ya saa mbili na nusu ndani ya giza kali wakakutana shambani kuzungumza!!
Walizungumza kwa utulivu wa hali ya juu wakiamini kuwa walikuwa wao peke yao.
****
BAADA ya mazungumzo mafupi lakini mazito na John Masele waziri wa zamani wa mambo ya ndani na nje. Sam alichukua pikipiki ambayo ilimfikisha Handeni Tanga.
Ulikuwa mwendo mrefu lakini kwa ushauri aliopewa na John kuwa eneo lile halikuwa salama basi ilimlazimu kufanya vile.
Saa nne usiku alikuwa akitetemeka kutokana na baridi kali maeneo ya Handeni kwa kipindi kile.
Alikuwa amejifunika shuka zito katika nyumba ya kulala wageni ambayo ilikuwa pembeni kidogo na mji.
Akiwa ndani ya blangeti, Sam alitoa faili alilokabidhiwa na John Masele, kisha akakitoa na kile kinasa sauti chake ambacho alikuwa amekitega katika kile chumba ambacho Gama alilipukiwa na bomu.
Alianza kwa kusikiliza tena upya harakati zote zilizofanyika katika chumba kile tangu alipokitega kinasa sauti kile.
Ukimya ulidumu kwa muda mrefu hadi pale alipoyasikia mapigano makali ndani ya chumba huku matusi yakitawala ugomvi ule.
Baadaye akaisikia sauti ikihoji kwa ghadhabu juu ya nani aliyewaagiza na amewaagiza nini katika kile chumba.
“BVB” akalisikia lile jibu.
Na hapo akakumbuka maongezi yake na mama lao. Mama yule alimweleza kuwa aliyepo nyuma ya mambo hayo alikuwa ni BVB.
Sam akakizima kinasa sauti kisha akalifungua faili na kuanza kusoma. Kadri alivyozidi kusoma ndivyo baridi lilivyouacha mwili wake na kisha kutawaliwa na joto kali.
Hii ni baada ya kukutana na jina la mtu ambaye alidhamini kampeni za chama tawala wakati raisi aliyepo madarakani alipokuwa akiwania kiti hicho.
Ndugu Benson Van Bronchost raia wa uholanzi.
Sam akarejea kulisoma mara mbilimbili lile jina na kujikuta akizinasa herufi B.V.B.
Naam! Hatua moja mbele katika kulitafuta jibu.
Kisha akayakumbuka mazungumzo mafupi na John Masele juu ya hila alizofanyiwa ilimradi tu asiingie ikulu.
John Masele alimweleza Sam kuwa ni maslahi binafsi yaliyosababisha awekewe zengwe na kubwa zaidi ni uswahiba kati ya raisi aliyepo na mtarajiwa raisi.
“Uliwahi kumfahamu hayati Steven Marashi…” lilikuwa swali kutoka kwa John Masele.
Sam akakubali kuwa anamfahamu kama muigizaji wa filamu.
“Alikuwa zaidi ya hapo, na laiti angeendelea kuwa hai mambo yangekuwa mengine wakati huu. Yule kijana alikuwa mpinga maovu sana, na hata wenzake katika jopo la vijana wa usalama wa taifa walikuwa wakimchukia. Tatizo alikuwa makini sana, hivyo hawakuweza kuzigundua nyendo zake. Steven alikuwa amefikia hatua nzuri sana alikuwa na picha za video za watu hawa wabaya. Huu ushahidi ungekufaa sana katika kufanya ukombozi…”
Mzee Masele akasita kidogo kisha akawa mwenye kuzungumza mwenyewe, “Tatizo mapenzi, haya mapenzi haya nilitamani sana kumkanya lakini hakuwa mtu wangu wa karibu sana hasahasa katika mambo binafsi”
Sam akayakumbuka mazungumzo hayo na kutambua kuwa bado safari ilikuwa ndefu hadi kuupata ukweli. Lakini kitendo cha kutambua kirefu cha BvB basi alijua ni hapo anapoweza kuanzia.
Akaendelea kuyafungua yale mafaili akakutana na baadhi ya picha zilizochongwa kutoka kwenye magazeti kadha wa kadha, baadhi ya picha zilimwonyesha John Masele enzi zake za uwaziri akiwa pamoja na raisi na waziri wa nishati na madini bwana Mathias Obhare.
Picha nyingine zilimwonyesha raisi akiwa ikulu pamoja na wazungu watatu wote wakiwa katika tabasamu zito.
Picha nyingine, hii ilikuwa picha ya rangi kabisa na haikunokena kuwa ya kukatwa kutoka katika gazeti. Hii ilimwonyesha raisi akiwa hoteli ambayo kwa mtazamo tu wa kijografia ilionekana si ya afrika. Alikuwa na wazungu wawili wakitabasamu Picha zote hazikuwa na maelezo yoyote yale.
Mara akakutana na picha nyingine, hii sura haikuwa ngeni hata kidogo machoni pake.
Alifumba macho na kukigongagonga kichwa chake ili aweze kukumbuka ni wapi aliwahi kuiona sura ile kwa mara ya kwanza.
Akavutia picha mikutano kadhaa aliyowahi kuhudhuria, hakuipata sura ile. Akawakumbuka baadhi ya wanasiasa bado haikuja ile sura.
Labda sijawahi kuiona! Alijisemea… lakini mara jicho lake likatua katika mkoba wake, akakumbuka kuwa ndani ya kile kimkoba palikuwa na filamu ya ngono.
Hapohapo akaikumbuka sura ile…. Ile sura ilikuwa miongoni mwa walioshiriki kufanya ngono na Lili huku wakirekodiwa.
“Ni nani mtu huyu.. eeh ni nani wewe mwanaharamu usiyekuwa na haya wewe… ni nani wewe ukaenda kucheza ile filamu bila aibu.
Tazama upo ikulu, hukujua kama ikulu ni sehemu takatifu we uliyelaaniwa… “
Akaigeuza ile picha kwa nyuma kutazama kama kuna maelezo yoyote lakini hakuambulia kitu.
“Mzee Masele nawe mbona wataka kunitia uchizi sasa eeh! Mbona mtihani unazidi kuwa mgumu, halafu hata namba ya simu hukunipatia we mzee… hivi unataka nije tena huko kijijini ama?” Sama alizungumza peke yake, kichwa kikiwa kinamuuma haswa.
Akapekua kibegi chake na kutoka na tembe maalumu kwa maumivu ya kichwa akameza!!
Akalala huku akijipangia ratiba kuwa asubuhi na mapema atatafuta kibanda chenye huduma za internet aweze kumchimba huyo BvB na atambue ni wapi pa kupiga hatua nyingine.
Pia aliamini kuwa akiwa kwenye mtandao atatafuta muafaka wa zile picha nyingine.
****
MAJIRA ya saa nne asubuhi Sam alikuwa katika kibanda chenye huduma za internet jirani na kituo kidogo cha mabasi Handeni, alilipia huduma ile kwa saa zima ili aweze kufanya mambo yake kwa utulivu. Akatwaa nafasi yake, dada mfupi muhudumu wa pale akafika na kutazama saa na dakika ambayo Sam alikuwa ameanza kutumia huduma ile.
“CD Rom inafanya kazi eeh” Sam akamuuliza yule dada.
“Nini?” akauliza badala ya kujibu.
“Huu mlango wa kompyuta unafanya kazi…” Sam akalainisha lugha kidogo.
“Yes of course..” alijibu yule dada kwa madoido, kisha akatoweka na kwenda kwa mteja mwingine.
Alianza kwa kuliandika jina la Benson van Bronchost kwenye GOOGLE. Yakatokea majibu mengi sana, majina ya wacheza soka, wanamuziki wa kiholanzi na mengineyo mengi.
Akaghairi na kuandika ‘Benson van Bronchost Tanzania’
Alipolitafuta jina lile akaambulia majibu kuwa ‘no match found’. Akatazama huenda amekosea herufi japo moja lakini hakuwa amekosea chochote.
Hapakuwa na kitu kama hicho nchini Tanzania!!
Sam akashusha pumzi kwa nguvu na kulegea mwili. Matumaini yakaanza kufifia tena.
Iwapo mtandao umeshindwa kumng’amua BvB yeye ataanzia wapi kufanikisha hilo kwa kutumia akili yake ya kawaida.
Alibaki akiikodolea macho kompyuta, alipotazama dakika aligundua kuwa alikuwa ametumia dakika kumi tu na alikuwa na dakika hamsini za ziada. Kichwani akakiri kuwa huyo wa kuitwa BVB alikuwa makini sana na mambo aliyokuwa anayafanya. Na kile kitendo cha mtandao kushindwa kumtambua maana yakea likuwa akiyafanya mambo yake kwa uangalifu.
Baada ya hapo akaingiza tena jina la raisi wa Tanzania, kisha akachagua kuona picha za raisi akiwa na wawekezaji wan je.
Zikatokeza picha nyingi sana, akapekua kibegi chake na kuanza kufananisha picha alizonazo na zile za kwenye mtandao.
Picha moja tu nd’o ilipata ufanano wake. Sam akategemea kukutana na maelezo juu ya picha ile lakini akakutana na hali kama ile ya picha aliyokuwa ameishikilia.
Duh! Sam akaguna!! Kisha akajilazimisha kucheka ilihali macho yalitaka kumtoka kwa hasira.
Sam akatamani kuomba arudishiwe pesa yake lakini aliamini kuwa hataeleweka.
Akaamua kutumia muda ule kufanya mambo ambayo hakupanga kuyafanya. Kwanza alitaka kuitazama ile CD ya ngono ili aweze kuitambua ile sura iwapo ni yenyewe ama la akaitoa cd yake, mara akasita. Wingi wa watu katika kibanda kile Sam akajisikia aibu kuitazama na pia kujulikana sana la Lili kungezua maswali kwa wale ambao wangetupia jicho na kutambua kinachoendelea.
Heri nusu shari kuliko shari kamili! Sam akajiepusha na hilo.
Moja kwa moja akaona ule haukuwa wakati muafaka kufanya vile.
Sam akaingia katika anuani yake ya barua pepe. Yote hii ni kupoteza muda ilimradi tu asiondoke huku nafsi yake ikimuuma sana, kutokamilisha lengo na pia kupoteza pesa bure.
Alikuta akiwa na takribani barua pepe tisa ambazo hazijasomwa.
Alitaka kuzipuuzia na kufanya mambo mengine lakini akavutiwa na moja iliyoandikwa.
‘MUHIMU SANA SOMA’
Haikumshtua sana barua pepe ile, kwani hilo lilikuwa neno la kawaida tu la kusisitiza. Ni vile tu muda ulikuwa unaruhusu nd’o maana Sam akaisoma.
Kwa sababu muda uliruhusu alijikuta akiifungua ile barua, akakutana na maelezo marefu kiasi lakini ambayo yalikuwa yanasisimua.
“SAM, bila shaka utaipata barua hii ukiwa katika harakati zako za kizalendo.
Nimekuandikia wewe haya ili ubaki na ushahidi huu hata nikiuwawa ama nikifungwa maisha jamii ibaki na shuhuda wewe wa kuwaeleza ukweli. Nimekuandikia wewe kwa sababu sijawahi kukuona ukiogopa, na kubwa zaidi u mtetezi wa wanyonge.
Sam, nchi hii imegawanwa, sio ya kwetu watanzania. Tunatawaliwa upya kisirisiri, uhuru wetu ni wa bendera tu!
Raisi, makamu wake, mkuu wa majeshi na wengineo wote wakubwa wamekuwa vibaraka. Wanawalamba miguu wazungu, wanawasikiliza kwa kila jambo hata kama ni kuhusu kuua watanzania wenzetu. Waone wanavyopendeza na suti zao kwa nje lakini ni watumwa walioozea katika utumwa. Wanatabasamu mbele yetu weusi, wanalia kwa weupe.
Kisa wanawalamba miguu weupe basi wanataka na sisi tuwalambe wao! Hali inatisha kijana wangu.
Mzee Matata nd’o raisi wako Sam, huyo raisi jina anamtetemekea mno na hana la kusema dhidi yake.
Ninakuambatanishia ushahidi wa simu nilizozungumza na IGP najua ni hatari lakini nakuamini wewe, sikiliza anavyomnyenyekea mzee Matata. Halafu ujiulize je hii nchi imeuzwa?
Mzee Matata ni nani katika nchi hii hadi atutawale, kuna HILA hapa Sam si bure. Wewe ni mwandishi kijana na mwanamapinduzi amka sasa!
Steven Marashi ana roho kama yako, ya kiukombozi. Tazama wamemuua, Yakubu Gama alivyojaribu kufuatilia na yeye wamemuua. Kuna nini hapo unadhani.
Sam ni wewe unayesadikiwa kuwa una nyaraka za marehemu Steven Marashi, kama ni hakika basi zifanyie kazi sasa kabla nchi haijamezwa na wakoloni wenye roho mbaya za kiuaji kuliko wale wakoloni wa kijerumani.
Nakutakia utendaji mwema!!
Usijihangaishe kujibu barua hii maana haitasomwa!”
Sam alisisimka mno, damu ikachemka na akili ikachangamka upya.
Upesi akanunua ‘flash disk’ akaipachika katika tundu la kompyuta na kupakua ile barua pamoja na zile sauti ambazo zilikuwa zimerekodiwa na mtu ambaye hakujitambulisha jina.
Sam alitumia akili ya ziada sana maana hakutaka kumuamini mtu kwa asilimia zote. Hata hii barua hakutaka kuamini kwa asilimia zote inatoka kwa mtu mwema.
Baada ya kupakua (download) na kuweka katika flash disk yake alitoweka na kuchukua chumba katika nyumba ya kulala wageni nyingine kabisa. Aliingia nyumba isiyokuwa na hadhi ya juu.
Alikuwa na maana yake!
Alikumbuka kumuuliza yule dada iwapo mida ya jioni ofisi yake itakuwa wazi, yule dada akajibu kuwa atakuwepo.
Sam akaondoka!!!
*****
Hello, nimependa na wewe mwenzangu usome hadithi hii nzuri. Utafurahi naamini. Ili usipitwe na hadithi tamu na nzuri nyingi kama hizi, unaweda download Hadithi App kutoka PlayStore kwa kubonyeza hapa: https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi
HILA NO.12
SEHEMU YA KUMI NA TATU
YAKUBU Gama alijisikia kuwa yupo fiti kiasi cha kuanza rasmi harakati zake za kuusaka ukweli. Lakini mwili haukuwa imara, miguu bado ilikuwa dhaifu na alitakiwa kutembea hatua chache na kisha kupumzika. Sumu iliyokuwa katika bomu lililolipuka ilikuwa imemuathiri.
Gama hakutaka kupumzika zaidi, hivyo akaamua harakati hizi azifanye huku akiwa na wasaidizi. Alihitaji watu wa kufanya kazi kwa niaba yake. Alihitaji watu wachache na ikiwezekana hata mmoja tu mwenye roho ya paka isiyoogopa kifo na kifua cha chuma cha kutunza siri.
Ni wapi atawapata? Hili nd’o lilikuwa swali alilojiuliza kabla hajaamua kuwasiliana na mrakibu msaidizi Robert Masawe ambaye nd’o alifanikisha mipango ya kuokoa uhai wake. Huku akitilia mkazo suala la mwili feki wa Gama kuzikwa bila kuagwa kwa sababu ulikuwa umeharibika.
Mpango huo ukahitimishwa na ripoti ya daktari Macho ambaye lake lilikuwa moja na bwana Robert Masawe.
Robert Masawe, akitumia gari ya mkewe aliendesha usiku mnene, hadi Morogoro ambapo alikutana na Gama.
Baada ya salamu Gama alimweleza mambo kadhaa na kisha kumwomba amtafutie mwanamke mwaminifu mwenye kifua cha chuma na roho ya paka ambaye anaweza kushirikiana naye kwa ukaribu zaidi.
“Gama… huhofii kwamba mwanamke anaweza kutuharibia”
“Mwanamke mwenye kifua cha chuma ni zaidi ya mwanaume jasiri….” Alijibu Gama huku akiwa amemkazia macho Robert.
“Basi nipe siku ya leo nifikirie kwa kina maana hili jambo tunaloshiriki lina matokeo mawili…”
“Ni ama kufa kwa mateso ama kupona na majina yetu kudumu katika vitabu milele na milele” Gama alimalizia ile sentensi kabla hata Robert hajamalizia.
Robert akatabasamu na kujisikia fahari kuzungumza na kuwa katika mpango ule madhubuti na kijana machachari kama Gama.
“Laiti kama usingekuwa umejeruhiwa naamini hili jambo ungelimaliza mwenyewe tena upesi sana.” Robert alisema huku akisikitika.
Maongezi yao yakamalizika kwa ahadi ya kupata muafaka ndani ya masaa machache yajayo.
Njia nzima akiwa anaendesha gari bwana Masawe alijiuliza ni kwanini Gama alikuwa akihitaji mwanamke katika shughuli ile.. lakini hakutaka kuumiza kichwa sana kwani alikuwa na mtihani wa kumtafuta huyo mwanamke anayeweza kushirikiana na Gama.
Alifikiria sana juu ya watumishi wa jeshi la polisi ambao anaweza kuwaamini lakini nafsi haikutulia kwa yeyote. Akafikiria kwa kina sana hata watu kadhaa aliowahi kukutana nao maishani. Akafikiria na kukosa jibu.
Hapakuwa na yeyote wa kuweza kuaminika katika hili!
Hofu ya kuyakoroga mambo na mwisho kuishia kitanzini ilikuwa imemtawala Robert. Lakini maji alikuwa ameyavulia nguo, hivyo iwe isiwe sharti lilikuwa lazima ayaoge tu.
Alipofika mzani wa Mikese kuondoka kutoka Morogoro, mara kama radi vile akili yake ikawaka na kukumbuka kitu. Akamkumbuka dada yake lakini kutoka tumbo la mama mwingine.
Ilikuwa ni miaka mingi imepita bila kuonana naye. Lakini moyo ukajiachia kabisa kuwa iwapo hakubadili tabia zake basi ni yule alikuwa akimfaa kwa kazi iliyokuwa mbele yake.
Alikuwa na kifua cha chuma, jasiri asiyeyaogopa maisha.
Alikuwa na uwezo wa kuitunza siri kadri awezavyo, alikuwa muongeaji sana lakini bahati mbaya alikuwa hayasemi yaliyo siri kwake.
Hili jambo lilimfanya Robert amshauri dada yake aende jeshini. Lakini hilo likagonga mwamba, dada alikuwa na siri zake lukuki. Hatimaye akaondoka nyumbani pasi na kuaga.
Robert akaingia jeshini na ikapita miaka mingi sana bila kuonana.
Ssa alikuwa akiuhitaji msaada wake ndugu huyo!
Wapi pa kumpata? Alijiuliza.
Jibu lilikuwa jepesi tu, ni mtu mmoja tu ambaye angeweza kujua.
Huyu alikuwa ni mdogo wao wa mwisho ambaye alitokea kuivana sana na dada yao. Lakini na yeye alikuwa na tabia zilezile.
Roho ya paka na kifua cha chuma! Huenda nd’o maana wakapendana.
Akaitazama saa yake, ilikuwa ni saa nane usiku. Hakutaka kusubiri zaidi akaegesha gari pembeni, akaichukua simu yake na kubofya namba za mama yake mzazi.
Bahati nzuri mama hakuwa amelala, alikuwa kwenye sherehe fulani na nd’o ilikuwa inaisha.
“Haujambo…” aliuliza.
Mama tayari amelewa looh! Robert alijisemea baada ya kumsikia mama yake. Alimjua vyema alivyo rafiki wa pombe. Lakini uzuri ni kwamba hakuwa mtu wa kupoteza kumbukumbu hata akilewa.
“Mama unayo namba ya Subira… ninahitaji sana namba yake sasa hivi.”
“Amefanyaje mwanangu tena mnataka kumfunga”
“Aaah! Mama hapana….”
“Hana simu… nikifika nyumbani nipigie nitampa simu yangu mzungumze.”
Kweli baada ya nusu saa Robert akapiga simu, mama alikuwa nyumbani tayari na simu ikapokelewa na Subira. Mdogo wao wa mwisho.
“Shkamoo kaka.”
“Marahaba, Subira hivi mmefunga shule ama?”
“Ndio tumefunga.”
“Nahitaji kesho uje Dar…”
“Mbona ghafla kaka, mi nataka kusoma twisheni…”
“Ndio ni ghafla lakini nahitaji uje, unakuja na kuondoka baada ya siku chache tu…”
“Aaah! Mi na wifi hazipandi kaka, sitaki tugombane.”
“Hautafikia nyumbani kwangu, nitakupokea tutazungumza na utalala mahali na kisha kuondoka. Nakutumia pesa kwenye simu ya mama, usije ukamwacha akatoa yeye ataenda kunywa pombe pesa yote. Nenda ukatoe mwenyewe halafu asijue kama unakuja huku, si unamjua mama tena.?”
“Sawa kaka! Kama usemavyo itakuwa hivyo” alijibu kwa ufupi. Robert akakiri kuwa hakika alikuwa anazungumza na roho ya paka.
****
DAR-ES-SALAAM, Tanzania saa tano usiku!
Katika mgahawa mdogo ambapo chipsi huuzwa hadi majira ya saa tisa usiku. Robert alikuwa ameketi na mdogo wake wa mwisho, Subira ambaye alikuwa ametokea jijini Mbeya siku hiyohiyo. Na kuingia jijini Dar majira ya saa kumi na mbili jioni. Lakini waliamua kukutana majira hayo ya saa tano usiku kwa sababu za kiusalama zaidi. Alikuwa ni Robert aliyetoa ushauri ule.
Mgahawa ulikuwa na watu wachache sana, licha ya hayo walijitenga mbali kabisa na mwanga.
Kwa kuwatazama upesi ungeweza kudhania kuwa yule likuwa ni mtu mzima amechepuka katika ndoa yake na hapo yupo na mwanafunzi wanayeishi naye katika mapenzi ya siri. Na kule kukaa kwao gizani ni kuendelea kuipalilia siri yao kwa maua ya miiba.
Robert alikuwa mtulivu, lakini Subira alikuwa mtulivu na makini sana. Alipiga funda moja la soda yake kisha akamtazama kaka yake machoni, ikiwa ni ishara ya kumtaka aanze kuzungumza.
“Subira mdogo wangu, nia yangu ya kuonana na wewe ni kwa ajili moja tu. Kwa ajili ya kukomboa mamia ya watanzania kutoka katika maisha magumu wanayoishi.”
“Lakini mimi bado mwanafunzi! Unataka nijiunge na siasa ama” alijibu huku akimkazia macho.
“Natambua na nd’o maana nikaamua kuonana na wewe. Wanafunzi nd’o mzizi wa ukombozi” Akasita kisha akaendelea, “Hivi shuleni kwenu kuna waalimu wangapi?”
“Sidhani kama umeniita Dar ili kujua maendeleo yangu shuleni…” Subira alimkatiza.
“No! anyway, tuachane na hayo lakini nimekuita hapa nahitaji msaada wako mkubwa kupita yote.”
“Upi kaka..”
“Nahitaji kuonana na Sekela.”
“Dada Sekela?” Subira akahoji. Robert akatikisa kichwa kukubaliana na mdogo wake.
“Unafahamu alipo ama, maana ni miaka sasa hajarudi nyumbani. Naamini yupo Dar!” Subira alitoa jibu ambalo Robert alilitarajia.
Hivyo ikamlazimu kusimulia kila kitu kilivyo na ni kwa jinsi gani msaada wa Subira ulikuwa unahitajika ili Sekela aweze kupatikana. Alitambua wazi kuwa licha ya umri mdogo wa binti yule hakuwa akitekwa kirahisi kwa maswali ya mitego.
Robert akasimulia mkasa juu ya serikali inavyoendeshwa kihuni huku wenye haki wengi wakiishi kama digidigi katika nchi yao ambayo inajitamba kuwa ni nchi huru kwa watu huru.
Alipomaliza kusimulia juu ya ugumu anaokutana nao hasahasa imani ya IGP na raisi juu ya mtu mbaya mzee Matata machozi yalikuwa yanamlenga Subira.
“Mzee Matata.. sura yake siku ambayo ameleta msaada wa vitabu shuleni kwetu haikunivutia kabisa kuamini kuwa eti amefanya vile kwa sababu ya huruma kwa watanzania. Walinibishia sana wenzangu lakini sasa naanza kupata imani na kila nilichokuwa nawaza siku ile…” Subira alizungumza kwa sauti ya chini huku akitikisa kichwa juu na chini.
Maelezo ya kaka yake yalikuwa yamemgusa haswa na kuamua kumuamini na kumfungukia kile akijuacho.
“Kaka, kumbuka yule ni dada yako, hata kama baba zenu ni tofauti anabaki kuwa dada yako tu. Nakumbuka uliwahi kusema kuwa polisi hana ndugu, kama umeamua usemi huo uzidi ule wa damu nzito kuliko maji basi amini kuwa mateso atakayopata dada yatakuwa juu yako na laana ya mama itakuangukia kwa sababu nitamweleza iwapo mambo yataenda kinyume. Mimi nitakukutanisha na Sekela, ila uyashike hayo niliyokueleza….”
“Subira, niamini mimi siwezi kufanya ujinga kama huo hata siku moja….”
“Sekela yupo Morogoro, nitawasiliana naye na kukutanisha naye. Kesho usiku… naomba unipeleke nikalale sasa…” alimaliza Subira na kusimama, Robert naye akasimama.
Wakaondoka hadi nyumba ya kulala wageni ambayo Robert alikuwa amemuandalia mdogo wake.
Usiku ule ukapita!!
****
MOROGORO, Saa mbili usiku.
Subira alikuwa katika nyumba ya wageni tayari alikuwa amewasiliana na dada yake juu ya kuonana kwao.
Hakumweleza kabisa juu ya ujio wa bwana Robert. Hivyo Sekela hakutilia mashaka yoyote na majira hayo alikuwa amekaribia katika chumba kile.
Walipeana mambo kedekede ya hapa na pale huku mdogo mtu akiwa mwingi wa maswali ya hapa na pale huku akihitaji kujua nini hatma ya dada yake katika kuusaka uhuru wake tena.
Kabla hii mada haijafika mbali mlango wa chumba kile ukagongwa. Subira alijua nini kinaendelea, mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana lakini alijikaza asionekane mwoga. Akauendea mlango na kuufungua. Na hapo akaingia Robert Masawe.
Ana kwa ana na Sekela ama maarufu kwa jina la mama lao. Dada yake kutoka kwa baba mwingine lakini mama yao akiwa ni mmoja.
Mama lao hakuonyesha mshtuko wa aina yoyote lakini jicho lake liliwaka haswa kumaanisha kuwa yu katika hasira kali mno.
Moyoni alijua tayari amekamatika, alitaka kumvamia Robert ili akabiliane naye lakini akashangazwa na upole wa yule bwana.
“Dada nisamehe bure, lakini amini kuwa hautajutia litakalozungumzwa maana hata wewe linakuhusu… kaka kama ulikuwa hujafahamu huyu hapa anaitwa mama lao, sahau kuhusu Atuganile au sekela. Bila shaka kila mmoja anamuhitaji mwenzake iwapo uliyonieleza ni ya ukweli”
“Sijabadili chochote katika maelezo yangu ya awali…”
“Basi mimi nawapisha!” Subira akasimama na kutoweka.
Mama lao akazungumza kwa kina na Robert, hatimaye akaondoka naye wakati huohuo wa usiku.
Akaenda kukabidhiwa kwa Yakubu Gama!
Naam! Kikosi kazi kikaanza kujengeka!
Baada ya kumwona mama lao na umbile lake, Yakubu alitaka kumpuuzia lakini walipoanza kuzungumza tu. Ile hali ya kujiamini ya mama lao ikamfanya aanze kuamini anazungumza na mwanamke wea shoka.
Mama lao akamueleza Gama juu ya kutekwa kwake na kuponea chupuchupu kufa mbele ya mikono ya wanaume wa kinyakyusa, Gama naye akamweleza mkasa wake uliotaka kuondoka na uhai wake.
Katika maelezo yao, kila mmoja akajikuta katika fumbo la nani ni BVB.
Yakubu Gama akawa kiongozi wa huu mchezo, mama lao akawa mtekelezaji. Kikosi kazi kikawa kinamkosa jemedari mmoja tu, huyu alikuwa ni Sam. Alikuwa akihitajika sana ili kuweza kukamilisha huu mchezo. Mchezo ambao Yakubu Gama aliubatiza jina la Kombolera
Mama lao alihoji nini maana ya Kombolera katika jambo hili zito. Lakini Gama akamwambia aelewe kuwa hiyo ni kombolera tu na mwishowe hatauliza tena kwa nini yaitwa kombolera. Bali atajiona mwenyewe akicheza kombolera
“Haya kombolera yetu inaanzia jijini Dar es salaam.” Gama akaagiza kisha usiku ukawa mwingi wote wakalala.
Hello, nimependa na wewe mwenzangu usome hadithi hii nzuri. Utafurahi naamini. Ili usipitwe na hadithi tamu na nzuri nyingi kama hizi, unaweda download Hadithi App kutoka PlayStore kwa kubonyeza hapa: https://play.google.com/store/apps/details?id=com.developict.hadithi
Jisajili kwenye:
Maoni (Atom)